Jubilei ya Miaka 50 ya Mfuko wa “Sant'Angela Merici wa Siracusa": Machozi ya Huduma!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mfuko wa “Sant'Angela Merici wa Siracusa” ni asasi inayojishughulisha na ulinzi na usaidizi kwa walemavu na watu dhaifu, hasa wale walioko hatarini, ili kuwakirimia matumaini, amani na utulivu wa ndani, iliyoanzishwa takribani miaka 50 iliyopita na mwaka 2024 inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Mfuko huu uko chini ya Jimbo Katoliki la Siracusa, lililoko Kusini mwa Italia. Kumbe ni taasisi inayotekeleza majukumu kadiri ya kanuni maadili na utu wema. Ilikuwa ni mwaka 1953 Picha ya Bikira Maria ilianza kutoa machozi kwenye familia Iannuso kutokana na mateso na mahangaiko ya watoto wake, kielelezo cha ukaribu na mshikamano wa Bikira Maria na watu wanaoteseka. Huu ni mwaliko pia wa kuonesha upendo na mshikamano na wale watu wanaoteseka, dhidi ya uchoyo, ubinafsi na hali ya kutoguswa na mahangaiko ya watu wengine. Ni mwaliko wa kuamsha dhamiri, ili kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani, tayari kuwasaidia, kuwainua na kuwasindikiza. Hii ndiyo amana na utajiri Mfuko wa “Sant'Angela Merici wa Siracusa” unaotangazwa na kushuhudiwa katika shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na mfuko huu kila siku ya maisha yao.
Ni utume unaojikita katika taaluma, weledi, sadaka na majitoleo binafsi, kama njia ya kushuhudia machozi ya Bikira Maria, tayari kuwapangusa watoto wake wanaoteseka; kwa kuonesha ujirani mwema kwa maskini, na kuendelea kutoa huduma kwa watu dhaifu, kwa kuwakaribisha na kuwahudumia watu wanaoishi katika umaskini. Kiini cha maisha na utume wao ni Injili, ambayo wanapaswa kujishikamanisha nayo. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 6 Aprili 2024 alipokutana na wanachama wa Mfuko wa “Sant'Angela Merici wa Siracusa” kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo. Injili ya Kristo Yesu ndiyo chemchemi ya maisha na utume wao kama ilivyokuwa kwa Yesu aliposikia kuhusu habari za Lazaro ambaye alikuwa hawezi. “ Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake.” Yn 11:33. Kumbe, wanachama wa Mfuko wa “Sant'Angela Merici wa Siracusa” ni mashuhuda hai wa sehemu hii ya Injili, kwa kuonesha huruma katika maisha na utume wao wa kuwasindikiza wale wanaoomboleza na kulia kutokana na machungu moyoni.
Na Kristo Yesu alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Kristo Yesu anakazia upendo kwa Mwenyezi Mungu na jirani, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanakumbushwa kwamba, siku ya mwisho watahukumiwa kwa kutumia kipimo cha upendo, kama mafuta ya faraja waliotumia kupaka majeraha ya jirani zao. “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” Baba Mtakatifu amewatia shime kuendelea kufuata njia hii na kwamba, anawaombea neema ya kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kuweza kulia na wale wanaolia na hivyo kuepukana na hali ya kutowajali watu katika shida na mahangaiko yao pamoja na uchoyo na ubinafsi uliokithiri, kiasi kwamba, moyo unashindwa kuwaonea huruma watu wanaoteseka kutokana na hali ngumu na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo. Waoneshe huruma kwa watu dhaifu na maskini kwani watu kama hawa ni ufunuo wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu amewatia shime wasonge mbele pasi na kukata tamaa na kwamba, huduma hii inahitaji ukimya na inapaswa kutendwa kila siku ya maisha kama mbegu iliyozikwa ardhini itakuja kuzaa matunda kwa wakati wake.