Jubilei ya Miaka 800 ya Madonda Matakatifu ya Mt. Francisko wa Assisi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 5 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Ndugu Wadogo wa La Verna na wale wanaotoka Kanda ya Toscana, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka mia nane tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipobahatika kupewa Madonda Mtakatifu mwilini mwake. Hii ilikuwa ni tarehe 15 Septemba 1224, yaani miaka miwili kabla ya kifo chake. Ndugu Wadogo wamemwonesha pia Baba Mtakatifu masalia ya damu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi yanayotembezwa sehemu mbalimbali za dunia, ili kuwakumbusha umuhimu wa kuimarishwa katika Kristo Yesu, Maskini na Mteswa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa katekesi juu ya maana ya Madonda Matakatifu katika maisha ya Wakristo na katika maisha ya Mfranciskani. Baba Mtakatifu anasema, kwa usahihi kabisa kufanana huku kwa Mdonda Matakatifu ni ishara fasaha ambazo Mwenyezi Mungu amewajalia watu wake katika hali ya imani, hadhi na asili mbalimbali katika muda wa karne zote hizi nane. Hii ni kumbukizi kwa watu wote watakatifu wa Mungu mateso na maumivu ambayo Kristo Yesu aliyapata kwa ajili ya upendo na wokovu wa binadamu. Hii pia ni ishara ya ushindi wa Pasaka. Ni kwa njia ya Madonda Matakatifu rehema ya Msalaba wa Kristo Mfufuka inapitia na kutiririka kuwaelekea watu watakatifu wa Mungu. Kwa mfuasi wa Kristo Yesu katika Madonda Matakatifu ya Mtakatifu Francisko anapata kioo cha utambulisho wake kwa kumtambua Kristo Yesu katika mwili wake hai, yaani Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.
Mkristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo anawekwa chapa ya Pasaka ya Bwana, kielelezo cha ushirika wa upendo wa Kanisa na kwamba, kila mwamini anajigundua upya jinsi alivyo mtoto mpendwa wa Baba aliyebarikiwa na aliyepatanishwa; Mtoto anayetumwa kutangaza na kushuhudia maajabu ya neema za Mungu na hivyo kuwa ni chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, Mkristo, anaitwa kuyaangalia kwa namna ya pekee kabisa Madonda ya Kristo Yesu, anayokutana nayo. Hawa ni watu wanaoteseka katika maisha na hivyo kubeba ndani mwao makovu ya mateso na ukosefu wa haki pamoja na makosa aliyotenda mwenyewe Katika utume huu Mtakatifu wa La Verna, yaani Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mwandani wa safari anaye waunga mkono na kuwasaidia ili wasikandamizwe na shida, hofu na migongano yao wenyewe sanjari na ile ya wengine. Hivi ndivyo Mtakatifu Fransisko alivyojitahidi kufanya tangu siku ile alipokutana na mkoma na kuendelea kuzama katika karama na huduma kiasi hata cha kujisahau kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumiziwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, akatekeleza dhamana na wajibu wake kwa ujasiri na unyenyekevu katika njia mpya, tulivu katika Bwana na jirani zao. Mtakatifu Francisko katika ufukara wake wa maisha ya kiroho sanjari na kujikabidhi kwake kwa Mwenyezi Mungu, amewaachia ndugu zake ushuhuda wa Injili ya daima. Baba Mtakatifu anasema, Madonda Matakatifu katika maisha na utume wa Mfranciskani ni wito wa kujenga na kudumisha umoja katika maisha yao wenyewe na katika historia yao, changamoto na mwaliko wa kukumbatia na kuambata toba na wongofu wa ndani, akiwa na lengo la kukarabati Kanisa la Kristo Yesu.
Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mtu aliyepata amani katika Msalaba alioutumia kuwabariki ndugu zake katika Kristo Yesu na kwamba, Madonda Matakatifu yanaonesha yale mambo msingi, mwaliko kwa Wafranciskani kurejea tena na tena katika malezi, shughuli za kitume, uwepo wao kati pamoja na watu wa Mungu. Wakitambua kwamba, wamesamehewa dhambi zao na hivyo wanakuwa ni vyombo vya msamaha na upatanisho; wameponywa na hivyo wanatakiwa pia kuwaganga na kuwaponya wengine, watu wenye furaha katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa nguvu ya upendo unaobubujika ubavuni mwa Kristo Yesu unakuwa ni kichocheo cha kujibidiisha kukutana na Kristo Yesu, kila siku ili kupyaisha ule upendo unaowaka kutoka moyoni. Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 ya Madonda Matakatifu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika jumuiya, Kanisa na katika ulimwengu katika ujumla wake, wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa Kristo, hata ikiwabidi kupoteza maisha yao. Wawe wanyenyekevu, washikamane, watu wenye furaha daima wakichuchumilia yale mambo msingi: Waupende Msalaba, maskini na kwamba, wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani, manabii wa matumaini katika ulimwengu ambao umesheheni dalili za ukanimungu. Wafranciskani wawe ni alama na mashuhuda wa Ufalme wa Mungu ulioko kati ya watu wa Mungu, unaoendelea kukua kwa njia ya maisha yao ya kitawa.
Katika sala ya Mtakatifu Francisko, inamwonesha kuwa ni mtu aliyeshikamana na upendo wa Kristo Yesu katika mwili na roho yake; Madonda Matakatifu yawasaidie watu kujifunza kumpenda Kristo Yesu, pamoja na jirani zao. Wajifunze kumtafakari na kumfuasa Kristo Yesu maskini na Mteswa. Imani, matumaini na mapendo ya Mtakatifu Francisko, yawasaidie kubeba mizigo ya maisha, ili hatimaye, waonje huruma ya Baba na faraja ya Roho Mtakatifu. Madonda ya watu wa Mungu yagangwe na kuponywa na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili hatimaye, waweze kama Mtakatifu Francisko wa Assisi mashuhuda wa huruma ya Mungu, huku wakiendelea kuganga, kuponya na kupyaisha maisha, kwa wale wote wanaomtafuta Kristo Yesu katika ukweli. Madonda Matakatifu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi yawe ni mng’ao wa maisha na ufufuko yanayoelekeza njia mpya za amani na upatanisho.