Jukwaa la Kikristo Ulimwenguni: Imani, Umoja na Ushuhuda wa Wakristo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Jukwaa la Kikristo Ulimwenguni “The Global Christian Forum, GCF” ni mkusanyiko wa kipekee wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo kimataifa yanayoleta pamoja mikondo yote mikuu ya Ukristo wa ulimwengu. Jukwaa la Kikristo Ulimwenguni ni nafasi wazi ambapo Wakristo wote wanaweza kukutana ili kukuza umoja na kuendelea: kuheshimiana na kuelewana na pia kushughulikia changamoto za pamoja za Wakristo ulimwenguni. Jukwaa la Kikristo Ulimwenguni kwa mwaka 2024 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuasisiwa kwake na mkutano wake kuanzia tarehe 15 – 19 Aprili 2024 huko Accra, Ghana unanogeshwa na kauli mbiu “Ili Ulimwengu Ujue.” Yn 17: 23. Hii ni sehemu ya Sala ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake ili wawe wamoja. “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” Yn 17:21-23.
Huu ni mkutano unaoadhimishwa mara baada ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Upembuzi yakinifu unaonesha kwamba, kumekuwepo na madhara makubwa yaliyosababishwa na UVIKO-19 hasa katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kiikolojia. Pale inapowezekana watoto waliowapoteza wazazi na walezi, ikiwezekana wabaki na kuhudumiwa kwenye maeneo ya kifamilia. Watoto, wazazi na walezi wasaidiwe ili kukabiliana na changamoto hii inayohitaji ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ikumbukwe kwamba, watoto na vijana ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Dhuluma, nyanyaso na ukatili dhidi ya watoto wadogo ni kinyume kabisa cha tunu msingi za Kiinjili, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watoto wanapaswa kulindwa na kuendelezwa, kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kifamilia. Kumbe, Kanisa na jamii katika ujumla wake, halina budi kuwekeza katika mchakato wa kuimarisha familia kadiri ya mpango wa Mungu. Serikali na watunga sera watoe kipaumbele cha kwanza kwa familia. Wakati wa maambukizi makubwa ya UVIKO-19 mikutano mingi imefanyika kwa njia ya mitandao ya kijamii, leo hii kuna shauku kubwa ya wajumbe kukutana mubashara.
Mkutano huu ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Jukwaa la Kikristo Ulimwenguni “The Global Christian Forum, GCF” na changamoto ya kuweka mpango mkakati kwa miaka ijayo. Hii pia ni fursa kwa wajumbe 250 kutembelea mji wa Cape Coast, nchini Ghana ili kujionea wenyewe madhara ya biashara ya utumwa ulimwenguni. Kumbe, hii ni fursa kwa wajumbe kufanya hija ya maisha ya kiroho, ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapewa kipaumbele cha kwanza. Hii ni hija ya kiroho inayowaalika wajumbe, kutubu na kumwongokea Mungu; hii ni Ibada ya maombolezo na upatanisho wa ndani, tayari kuomba uponyaji kutoka kwa Kristo Yesu. Ni katika muktadha wa maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia wajumbe ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Flavio Pace, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo “Dicastery for Promoting Christian Unity.” Baba Mtakatifu anakaza kusema, kauli mbiu “Ili Ulimwengu Ujue.” Yn 17: 23 pamoja na mambo mengine unakazia zaidi umoja na upendo kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili Wakristo katika maisha yao waweze kuyatolea ushuhuda ulimwenguni kwa kuondokana na migawanyiko na uadui usiokuwa na mashiko wala mguso. Umoja ni muhimu sana katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa Ulimwenguni.
Jukwaa la Kikristo Ulimwenguni “The Global Christian Forum, GCF” tangu kuanzishwa kwake miaka ishirini na mitano iliyopita limechangia kwa kiasi kikubwa kuragibisha umoja wa Wakristo kwa kutoa fursa kwa wanachama kukuza na kudumisha kifungo cha upendo; kwa kuheshimiana, ili hatimaye kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu unaowawezesha kukutana katika Kristo Yesu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka ishirini na mitano tangu kuanzishwa kwa Jukwaa la Kikristo Ulimenguni itakuwa ni fursa ya kupyaisha na kukuza imani; kuboresha upendo wa kidugu pamoja na kubadilishana historia, tayari kujikita katika kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo, ili siku moja, Kanisa liweze kutangaza na kushuhudia umoja kamili. Kwa upande wake, Monsinyo Flavio Pace, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika hotuba yake amekazia umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda, utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kupinga kwa nguvu zote mifumo yote ya utumwa mamboleo. Jukwaa hili ni chombo muhimu sana cha kukuza na kudumisha uekumene, kwa kutafuta suluhu za matatizo, changamoto na fursa za kujenga na kudumisha uekumene na usawa. Ni wakati wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kuganga na kuponya makovu ya utengano, ili Wakristo wawe wamoja, kama Sala ya Kristo Yesu inavyokazia: Umoja katika maisha ya kiroho, Sala, ushuhuda wa nguvu za Kiinjili; udugu, upendo, heshima pamoja na kushirikishana tunu msingi za Kiinjili; upendo na ukweli. Ameonesha umuhimu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene yanayopania pamoja na mambo mengine, safari ya pamoja katika umoja na imani.