Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Aprili 2024 amemteuwa Kardinali Angelo De Donatis kuwa Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Aprili 2024 amemteuwa Kardinali Angelo De Donatis kuwa Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume.  (Vatican Media)

Kardinali Angelo De Donatis Mhudumu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Aprili 2024 amemteuwa Kardinali Angelo De Donatis kuwa Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume na hivyo kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Kardinali Mauro Piacenza. Kardinali De Donatis anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwamini na kumkabidhi madaraka ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu tangu tarehe 9 Novemba 2015. Jimbo kuu la Roma ni familia inayopaswa kupendwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Aprili 2024 amemteuwa Kardinali Angelo De Donatis kuwa Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume na hivyo kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Kardinali Mauro Piacenza. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Angelo De Donatis alizaliwa kunako tarehe 4 Januari 1954 huko Casarano, Jimbo Katoliki la Nardo-Gallipoli nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 12 Aprili 1980 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na kuanzia tarehe 28 Novemba akahamia Jimbo kuu la Roma. Tangu wakati huo ametekeleza utume wake kama Paroko usu, mwalimu wa dini shuleni; Afisa katika Sekretarieti ya Jimbo kuu la Roma; Mtunza nyaraka wa Baraza la Makardinali; Mkurugenzi wa Ofisi ya Wakleri, Jimbo kuu la Roma; Baba wa maisha ya kiroho, Seminari kuu ya Jimbo kuu la Roma. Kuanzia mwaka 2003 akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Marko, Mwinjili na Msaidizi wa Chama cha ndugu na wazazi wa Wakleri Jimbo kuu la Roma. Kunako mwaka 2014 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuongoza mafungo ya Kipindi cha Kwaresima kwa Baba Mtakatifu Francisko na waandamizi wake wakuu. Tarehe 14 Septemba 2015 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma na kuwekwa wakfu tarehe 9 Novemba 2015. Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anamweka wakfu Askofu mkuu mteule Angelo De Donatis wa Jimbo Kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko alisema, Kristo Yesu katika utekelezaji wa utume wake hapa duniani aliwachagua Mitume pamoja na waandamizi wao ili kuendeleza mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote, wakiwa chini ya Mchungaji mmoja pamoja na kuendelea kuwatakatifuza, kuwafundisha na kuwaongoza watu wa Mungu kuelekea kwenye uzima wa milele.

Papa akiwa na Baraza la Kichungaji Jimbo kuu la Roma
Papa akiwa na Baraza la Kichungaji Jimbo kuu la Roma

Dhamana hii imeendelezwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Daraja takatifu, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika Kanisa lake hadi nyakati hizi. Kwa njia ya Maaskofu, Yesu Kristo anaendelea kuwatangazia watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu; kuwatakatifuza watu kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kupata watoto wapya wa Kanisa; mambo yanayopaswa kujionesha katika hekima na unyenyekevu wa Askofu anayewaongoza watu wake kuelekea kwenye furaha ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma kumpokea Askofu mpya miongoni wa urika wa Maaskofu, kwa kumpatia heshima anayostahili kama mtumishi wa Kristo na mgawaji wa mafumbo ya Kanisa, ambayo anapaswa kuyatolea ushuhuda wa maisha. Baba Mtakatifu alimkumbusha Kardinali Angelo De Donatis kwamba, ameteuliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya mambo yamhusuyo Mungu; kwa ajili ya huduma kadiri ya mfano wa Kristo mchungaji mwema na wala si kwa ajili ya kuwatala watu. Alimtaka kutangaza na kushuhudia Injili na Mafundisho ya Kanisa. Mahubiri yawe ni chemchemi ya neema kwa watu wa Mungu, ili waweze kuwa wema na watakatifu zaidi. Awe ni mchungaji na mlezi mwema wa Mapadre na Majandokasisi pamoja na kuendelea kuonesha upendo kwa waamini wote, hususan maskini, wagonjwa na wote wanaohitaji msaada wa Kanisa.

Kardinali De Donatis Ameongoza Njia ya Msalaba kwa mwaka 2024
Kardinali De Donatis Ameongoza Njia ya Msalaba kwa mwaka 2024

Baba Mtakatifu aliwaalika waamini wa Jimbo kuu la Roma kuonesha ushirikiano mkubwa kwa Kardinali De Donatis ambaye atapaswa kuwasikiliza kwa makini na katika hali ya uvumilivu sanjari na kuendeleza majadiliano ya: Kitamaduni, kidini na kiekumene. Awe ni mfano wa ukarimu wa Kanisa la Roma, kwa kuwasaidia maskini na wote wanaohitaji msaada wa hali na mali. Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, Kardinali De Donatis alichangamotishwa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, anakuwa kweli mtu wa huruma, kwa kuwafundisha wengine njia inayowaelekeza kwenye huruma bila kubagua. Awalinde na kuwahudumia waamini kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu: Mwalimu, Kuhani mkuu na Mchungaji mkuu na kwa njia ya Roho Mtakatifu analijalia Kanisa maisha mapya pamoja na kuwaimarisha viongozi wa Kanisa licha ya udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anamtaka Kardinali De Donatis kuwa mlinzi na mtetezi wa familia.

Kardinali De Donatis
Kardinali De Donatis

Kristo Yesu “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.” Yn 21: 18. Hii ni changamoto kwa wafuasi wa Kristo Yesu kumfuasa Kristo Yesu kila wakati katika maisha na utume wao, daima wakitambua kwamba, Kristo Yesu yuko mbele yao, kuwaonesha njia ya kufuata. Ukomavu wa Kikristo anasema Kardinali De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume ni utii pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume; dhamana inayotekelezwa katika maisha ya mwamini kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kardinali De Donatis anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwamini na kumkabidhi madaraka ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu tangu tarehe 9 Novemba 2015. Katika kipindi chote hiki, Kardinali De Donatis anasema, amegundua kwamba, hii ni familia inayopaswa kupendwa na kuendelea kukua na kukomaa katika utii na udugu wa kibinadamu. Kipaumbele cha pekee ni: Kulisikiliza, Kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kufanya mang’amuzi katika ngazi ya mtu binafsi na yale ya kijumuiya, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu Jimbo kuu la Roma. Hii ni sehemu ya ujumbe uliotolewa na Kardinali De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, baada ya uteuzi huu mpya, tayari kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ni katika muktadha wa uteuzi huu, Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 8 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na Baraza la Kichungaji Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu amewaambia Maaskofu wasaidizi wa Jimbo kuu la Roma kwamba, itachukua muda mrefu kidogo ili kufanya uteuzi wa Makamu Askofu wa Jimbo kuu la Roma mintarafu Katiba ya Kitume ya “In Ecclesiarum communione” iliyochapishwa tarehe 6 Januari 2023.

Kardinali De Donatis

 

09 April 2024, 14:27