Tanzia: Kardinali Pedro Rubiano Sàenz Amefariki Dunia 15 Aprili 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Salam za rambirambi alizomwandikia Kardinali Luis José Rueda Aparicio, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bogotà, nchini Colombia, anasema, amesikitishwa sana na taarifa za kifo cha Kardinali Pedro Rubiano Sáenz, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Bogotà, anapenda kutoa salamu zake za rambirambi kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito, uliotokea, Jumatatu tarehe 15 Aprili 2024, akiwa na umri wa miaka 91, huko kwenye mji mkuu wa Bogotà. Baba Mtakatifu anatolea sala na maombi yake kwa ajili ya mchungaji mkuu Kardinali Pedro Rubiano Sáenz, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Yesu. Anamkabidhi Hayati Kardinali Pedro Rubiano Sáenz, mikononi mwa Bikira Maria wa Chiquinquirá ili aweze kumsindikiza katika usingizi wake wa amani, kama ishara ya imani na mtumaini kwa Kristo Yesu Mfufuka.
Kardinali Pedro Rubiano Sáenz, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Bogotà alizaliwa kunako tarehe 13 Septemba 1932. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 8 Julai 1956 akapewa daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 2 Juni 1971 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Cùcuta na kuwekwa wakfu tarehe 11 Julai 1971. Tarehe 26 Machi 1983, Mtakatifu Yohane Paulo II, akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Cali na kusimikwa tarehe 7 Februari 1985. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 27 Desemba 1994 akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bogotà nchini Colombia na kusimikwa tarehe 11 Februari 1995. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 21 Februari 2001 akamteuwa kuwa ni Kardinali na hatimaye, kusimikwa tarehe 25 Februari 2001. Ilipogota tarehe 8 Julai 2010, Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI akaridhia ombi lake la kutaka kung’atuka madarakani. Tarehe 15 Aprili 2024 akaitupa mkono dunia akiwa na umri wa miaka 91 ya kuzaliwa.