Tafuta

Ni katika muktadha wa kumbukizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria, mahujaji kutoka Hungaria, Alhamisi tarehe 25 Aprili 2024 walikutana na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria, mahujaji kutoka Hungaria, Alhamisi tarehe 25 Aprili 2024 walikutana na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.   (Vatican Media)

Kumbukizi ya Hija ya Papa Francisko Nchini Hungaria 28-30 Aprili 2023

Budapest mji mkuu wa Hungaria unasifika kwa uzuri na kwamba, mji huu ni daraja na mahali pa watakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu nchini Hungaria kusali kwa ajili ya kuombea mchakato wa ujenzi wa amani Barani Ulaya, sanjari na kuwapatia vijana fadhila ya matumaini, kinyume kabisa na falsafa ya vita, kwa kujikita katika ujenzi wa familia na wala si ujenzi wa kuta zinazowatenganisha watu wala vita inayosababisha maafa makubwa kwa watu na mali

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 41 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Aprili 2023 ilinogeshwa na kauli mbiu “Kristo ndiye wakati wetu ujao.” Ni hija ambayo ilijikita katika mihimili mikuu mitatu: Baba Mtakatifu Francisko kama hujaji wa amani katikati ya Bara la Ulaya, ambako misimamo mikali ya utaifa na kampeni za vita zikiendelea kupamba moto! Hii ni hija iliyopania pamoja na mambo mengine: kukoleza ari na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni hija ambayo ilipania kuwaimarisha watu wa Mungu nchini Hungaria katika imani, matumaini na mapendo, kwa kukazia dhamana na wajibu wa familia na ukarimu unaopata chimbuko lake katika maisha ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria, mahujaji kutoka Hungaria, Alhamisi tarehe 25 Aprili 2024 walikutana na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, alikumbushia kwamba, Budapest mji mkuu wa Hungaria unasifika kwa uzuri na kwamba, mji huu ni daraja na mahali pa watakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu nchini Hungaria kusali kwa ajili ya kuombea mchakato wa ujenzi wa amani Barani Ulaya, sanjari na kuwapatia vijana fadhila ya matumaini, kinyume kabisa na falsafa ya vita, kwa kujikita katika ujenzi wa familia na wala si ujenzi wa kuta zinazowatenganisha watu wala vita inayosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zilindwe
Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zilindwe

Baba Mtakatifu Francisko amewakaribisha mahujaji kutoka Hungaria wakati huu wanapofanya hija ya maisha ya kiroho, kuonesha ushirika wao na Khalifa wa Mtakatifu Petro, tayari kuungama imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, hususan katika kipindi hiki cha Pasaka, ambapo Kristo Mfufuka anawaangazia waja wake mwanga wa matumaini yasiyodanganya kamwe. Baba Mtakatifu anasema, uwepo wa mahujaji hawa mjini Vatican unamkumbusha hija yake ya kitume nchini Hungaria alikokwenda kama hujaji kati ya watu wa Mungu nchini Hungaria, na kama ndugu na rafiki. Akiwa mjini Budapet, Baba Mtakatifu alishiriki katika sala kwa ajili ya kuombea Bara la Ulaya, ili liweze kujikita katika ujenzi wa amani, kwa kuwapatia vijana wa kizazi kipya leo na kesho inayosheheni matumaini na wala si makaburi, kuwashirikisha katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na wala si kuta za utengano. Baba Mtakatifu anakaza kusema, akiwa Hungaria, nchi iliyorutubishwa kwa tunu msingi za Kiinjili, alisali na kuwaombea ili waweze kurejea tena na tena kwenye mizizi mintarafu historia ya nchi yao, kwa kufuata mifano bora ya watakatifu na wenye heri wa Hungaria.

Kristo Ndiye Wakati Wetu Ujao
Kristo Ndiye Wakati Wetu Ujao

Kristo Yesu Mfufuka aliwakirimia wafuasi wake zawadi ya amani, inayotekelezeka kwa kuanzia katika sakafu ya moyo wa kila mmoja wao, katika malango ya makazi yao hata kabla ya kutoka nje na hapo wanapaswa kufanya maamuzi magumu katika maisha yaani ikiwa kama wanataka kuishi kwa amani pamoja na watu wengine. Amani ya kweli inapata chimbuko lake katika msamaha, ingawa si rahisi sana kuweza kusamehe na kusahau, kwa sababu kwa njia ya msamaha wa kweli, moyo huweza kujaa furaha. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, alipenda kuliweka Kanisa nchini Hungaria chini ya ulinzi na maombezi ya watakatifu wa Hungaria: Mtakatifu Stefano, Mtakatifu Ladislaus, Mtakatifu Elizabeth; watakatifu na wenyeheri kutoka Hungaria, watakatifu hawa wawaimarishe ili hatimaye waweze kuwa ni mashuhuda wa utakatifu wa maisha na wenye furaha katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Baba Mtakatifu anasema hija yake ya kitume ilimwezesha kwenda nchini Hungaria kama ndugu yao katika Kristo Yesu, changamoto ni kutenda kadiri mtindo wa Mungu unaofumbatwa katika: upendo, ukaribu na huruma, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha; kwa kusimama na kutetea haki msingi za wanawake wakimbizi na wahamiaji; kwa kuwatunza na kuwafariji wagonjwa; kwa kukuza na kudumisha: sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; faraja na huruma kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, alifurahi sana kukutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya; na kuwataka wazee kuendelea kukita maisha yao katika mizizi, huku wakilinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kijamii, daima wakiwa na imani, matumaini na mapendo ili kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; umoja na amani, kwani kuna heri kutoa kuliko kupokea!

Hujaji wa imani, matumaini na mapendo
Hujaji wa imani, matumaini na mapendo

Kama rafiki wakati wa hija yake ya kitume nchini Hungaria, Baba Mtakatifu Francisko anasema, alikutana na kuzungumza na watu wanaoteseka; wakimbizi na wahamiaji; maskini pamoja na wahitaji. Baba Mtakatifu anawashukuru watu wa Mungu nchini Hungaria kwa huduma wanazotoa miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji kutoka nchini Ukraine pamoja na mchakato wa kuwaingiza katika maisha na utamaduni wa watu wa Hungaria. Baba Mtakatifu anaendelea kuwapongeza kwa ari na mshikamano, kielelezo kwamba, wao ni mahujaji katika kipindi hiki cha Pasaka; wanapaswa kumwona ndani mwao Kristo Yesu Mfufuka katika kuumega mkate, yaani katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, pamoja na kuwalisha wenye njaa na kuwanyweshwa wenye kiu. Watambulikane katika kusikiliza, kutafakari na kimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao. Wawe kweli ni mashuhuda amini wa imani katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni, huku wakionesha upendo unaothubutu kuwapokea hata wale ambao wako tofauti na wao, kwa kuheshimu: haki msingi za binadamu, ut una utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kumbukizi ya hija ya kitume ya Papa Francisko Hungaria 2023
Kumbukizi ya hija ya kitume ya Papa Francisko Hungaria 2023

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 25 Aprili 2024 alikutana na kuzungumza kwa faragha na Rais Tama’s Sulyok wa Hungaria ambaye alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Viongozi hawa wawili wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Wamepongeza mchango wa Kanisa Katoliki nchini Hungaria katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Baadaye wamejikita katika mada nyeti mintarafu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, vijana wa kizazi kipya pamoja na kuendelea kujikita katika Jumuiya za Wakatoliki zinazonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia. Baadaye, kwa pamoja wamefanya rejea kuhusu vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi na madhara yake katika ustawi, maendeleo na uchumi sehemu mbalimbali za dunia. Wamesema kuna haja ya kuongeza nguvu katika kulinda na kudumisha amani sehemu mbalimbali za dunia.

Hungaria
26 April 2024, 15:30