Kumbukizi ya Miaka 40 tangu Vijana Walipokutanika Mjini Vatican: Mwanzo wa WYD
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mama Kanisa anaendelea kujiimarisha katika mchakato wa utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake kwa njia ya utume wa vijana katika: Parokia, Majimbo, Kitaifa na Kikanda pamoja na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Hili ni tukio ambalo linawakusanya vijana kutoka pande mbali mbali za dunia ili kusali, kutafakari na kufurahia zawadi ya maisha ya ujana huku wakijitahidi kumzunguka Kristo Yesu, anayepaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni cheche ya mwanga wa imani, matumaini, mapendo na zawadi kubwa ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa na kwamba, matunda ya maadhimisho haya ni juhudi za sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kabla, wakati na baada ya maadhimisho haya! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake! Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi. Hili ni Kanisa ambalo limewasukuma vijana kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wamekuwa kweli ni wadau wa Heri za Mlimani, Manabii wa nyakati hizi na vyombo vya ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake; mahali ambapo vijana wanaweza kuchota tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni na kijamii.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni chombo muhimu sana cha unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa kwa kujishikamanisha na: huruma pamoja na upendo wa Kristo Yesu. Hili ni Jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande hizi mbili anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kusikilizana kwa makini. Hii ni Epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa vijana. Hii ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake! Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, tarehe 22 Aprili 1984 mara tu baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Ukombozi, yaani kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, aliwakabidhi vijana Msalaba, alama ya Mwaka Mtakatifu, lakini zaidi kama kielelezo cha upendo na huruma ya Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni ushuhuda unaoonesha kwamba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, mwanadamu ameweza kukirimiwa ukombozi. Tangu wakati huo, Msalaba huu ukajulikana kuwa ni Msalaba wa Vijana, ambao umezunguka na kuzungushwa na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa kipindi cha miaka yote hiyo!
Ni katika muktadha huu, Dominika tarehe 14 Aprili 2024 Mama Kanisa amefanya kumbukizi ya Miaka 40 tangu vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia, walipokutana kwa mara ya kwanza, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi kuanzia tarehe 25 Machi hadi tarehe 22 Aprili 1984 na huo ukawa ni mwanzo wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni. Kardinali José Tolentino de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu ndiye aliyeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu muhimu sana ya kumbukizi ya Miaka 40 tangu vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia walipokusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na hiyo ikawa ni chemchemi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ambayo yamesimamiwa na kuongozwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Benedikto XVI na sasa Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho haya ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa na yameendelea kuwa ni chemchemi ya matumaini, imani, mapendo na ujana wa Kanisa, tayari kuwawezesha vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Vijana wanayo dhamana na wajibu wa kuwainjilisha vijana wenzao; vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na kumwangalia Bikira Maria, Mama wa Kanisa na nyota ya uinjilishaji mpya. Kwa hakika vijana ni furaha ya Kanisa na wanaitwa na kutumwa kuwa ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kushikamana na wale wote wanaoteseka na kuhuzunika moyoni mwao; kufurahi na wale wanao furahi katika maisha, sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na la Kimisionari. Maadhimisho haya yamehitimishwa kwa: Sala, Ibada ya Kuabudu Msalaba na Katekesi ya kina kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni.