Kumbukizi ya Miaka 70 ya Kamati ya Kipapa ya Sayansi ya Historia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Kamati ya Kipapa ya Sayansi ya Historia: “Il Pontificio comitato di scienze storiche” (Kwa Kilatin “Pontificius Comitatus pro Scientiis Historicis” ni sehemu ya Sekretarieti kuu ya Vatican. Kamati hii ilianzishwa na Papa Pio XII kunako tarehe 7 Aprili 1954. Wajumbe wa Kamati ya Kipapa ya Sayansi ya Historia, Jumamosi tarehe 20 Aprili 2024 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, aliwasihi wajumbe kujizatiti zaidi katika ujenzi wa diplomasia inayowakutanisha watu, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana badala ya utamaduni wa watu kupigana. Taasisi hii inaadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake na miaka 60 ya Jarida la Nyaraka na Hati.
Baba Mtakatifu amewakaribisha wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, anawashukuru kwa kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa karama zao: Tafiti na Tahariri ambazo zimeiwezesha Taasisi hii kuadhimisha Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, kielelezo makini cha majitoleo katika fani mbalimbali za kihistoria zenyewe mwelekeo wa kidunia. Hii ni dhamana inayotekelezwa kwa kuzingatia ari na mwamko wa kimajadiliano mintarafu maeneo ya kijiografia pamoja na Mapokeo. Ni dhamana inayowawezesha kushirikiana na watafiti wengine, ili kukuza na kudumisha mahusiano ya kisayansi na kiutu kati yao; ili kukuza utamaduni wa kusikilizana na kuheshimu ukweli.
Mikutano na ushirikiano na watafiti kutoka tamaduni na dini mbalimbali unaweza kuwa ni mchango wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo na kimsingi mwelekeo huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa diplomasia inayowakutanisha watu ili kujenga utamaduni wa watu kukutana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, sanjari na kuepuka kinzani na migogoro inayosababisha vita. Lengo ni kuwa vyombo na wajenzi wa matumaini ambayo hayatahayarishi. Rej. Rum 5:5. Mtakatifu Paulo VI katika maisha na utume wake, alikazia sana kati ya Kanisa na tafiti katika ukweli; tafiti na huduma. Hapa ni mahali ambapo wajumbe wa Kamati ya Kipapa ya Sayansi ya Historia wanapoweza kukutana na watu wa Mungu. Huu ni kweli wa kidini na ukweli wa kihistoria na kwamba, wao ni wahudumu wake.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, miundo mbinu ya Ukristo: Mafundisho tanzu ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema, Ibada na Liturujia ni mambo ambayo yamesimikwa katika ushuhuda wa Mitume wa Yesu; ni mambo ambayo wameyasikia na kuyashuhudia na kwamba, ni wajibu wao kuhakiki ukweli wake wa kihistoria. Mama Kanisa anafanya hija katika historia, akiwa anaandamana na watu pembeni mwake; hawa ni watu wa nyakati zote na kwamba, Kanisa haliwezi kumilikiwa na utamaduni wa watu fulani tu, na kwa njia hii, Kanisa linapania kujikita katika mchakato wa kuwakutanisha watu, kinyume kabisa na utamaduni wa kutupa. Katika kipindi cha miaka 70 ya uhai wake Kamati ya Kipapa ya Sayansi ya Historia imejitahidi kukwepa kinzani na migogoro na kwa njia ya tafiti makini, wamejizatiti na kuendelea kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa umoja na utulivu kama ilivyokuwa siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume wa Yesu. Mama Kanisa pia anafanya kumbukizi ya miaka 70 tangu maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ambamo Mtakatifu Paulo VI aliwakumbusha Mababa wa Mtaguso kwamba, Mama Kanisa anakaa kati ya Kristo Yesu na kwamba, Jumuiya ya binadamu haipaswa kujitafuta yenyewe, bali Kanisa linapaswa kuwa ni kwa ajili ya Kristo na ndani ya Kristo na kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 70 tangu Kamati ya Kipapa ya Sayansi ya Historia ianzishwe, wamekuwa ni waalimu katika ubinadamu na wahuduma katika ubinadamu.