Kundi la Miji ya Urithi wa Dunia Nchini Hispania: Rithisheni Pia: Imani, Matumaini na Mapendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) limetoa tamko la kutambua baadhi ya miji kuwa ni sehemu ya urithi wa dunia na hivyo kupewa heshima kubwa na kutambuliwa Kimataifa. Heshima hii inawawaka wenyeji wa miji hii kuhakikisha kwamba, miji yao inalindwa na kuhifadhiwa kimaadili na kiutu kwa ajili ya vizazi vijavyo. Hii ni pamoja na kutunza vituo vya kihistoria, kwa kuendelea kujikita katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kusimama kidete kulinda urithi wa kumbukumbu kwa kulinganisha kati ya usanidi wa maisha ya zamani na maisha katika ulimwengu mamboleo. Kama sehemu ya mbinu mkakati wa kukabiliana na changamoto hizi, kunako mwaka 1993 Kundi la Miji ya Urithi wa Dunia Nchini Hispania “Grupo Ciudades Patrimonio de la Humanidad” liliundwa, likiwa na lengo la kufanya kazi kwa pamoja katika mchakato wa ulinzi wa urithi wa kihistoria na kitamaduni wa miji hii na katika kudumisha na kuimarisha njia za maisha ambazo vituo hivi vya kihistoria vinahitaji, kwa kuanzisha sera na mbinu mkakati wa kushughulikia matatizo na changamoto za kila siku.
Katika kipindi cha miaka ishirini na mitano iliyopita Kundi la Miji ya Urithi wa Dunia Nchini Hispania, “Grupo Ciudades Patrimonio de la Humanidad” limejipatia uzoefu katika medani mbalimbali za maisha na suluhu ambazo zimewasaidia kusonga mbele katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya kila moja ya miji hii pamoja na kutambua kwamba, utajiri wa kihistoria unapatikana katika umoja wake. Ni katika muktadha huu, Kundi la Miji ya Urithi wa Dunia Nchini Hispania, Jumamosi tarehe 13 Aprili 2024 limekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, ambaye ameonesha furaha yake kwa kuwakaribisha mjini Vatican, Mji ambao unahifadhi urithi mkubwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ndiye mlezi wao, jukumu kubwa, lakini pia ni wito mzuri.
Kumbe, masilahi katika urithi huu hayana budi kuwa na mtazamo mpana zaidi kwa kujikita katika uadilifu wa mtu anayepokea urithi huu na watu ambao katika maisha na utume wao, wameurithisha urithi huu na hivyo kuwa ni somo la maisha na sehemu ya makumbusho. Hii ni sehemu ya mateso na matamanio ya watu ambao wamejenga miji yao kwa wakati, mchanganyiko wa tamaduni na ustaarabu ambao umefanikiwa kila mmoja kwao, na bila shaka imani yao kwa Mungu, ambayo hufanya mioyo yao kupiga kwa shauku inaendelea. Baba Mtakatifu analitaka kundi hili pamoja na mambo mengine kusambaza na kurithisha imani, matumaini na mapendo kwa watu wao, kwa kuendelea kutafakari makaburi, busara na nguvu ambazo zilisaidia kuwezesha na hatimaye, kukamilisha uumbaji wake. Wachangamotishwe na somo la haki ambalo kila historia inalikumbatia na kulitambulisha.