Maadhimisho ya Siku ya 100 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Cha "Sacro Cuore"
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Kunako mwaka 1919, watu watano mashuhuri akina Padre Agostino Gemelli, Ludovico Necchi, Francesco Olgiati, Armida Barelli pamoja na Ernesto Lombardo walianzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” “L'Università Cattolica del Sacro Cuore (UCSC) Jimbo kuu la Milano. Kilianza kufanya kazi rasmi tarehe 7 Desemba 1921 ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na matokeo yake Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa! Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Kuna wanafunzi zaidi ya 43, 302 wanaopata elimu bora na makini inayokidhi viwango vya soko la ajira Barani Ulaya. Ni Chuo kikuu ambacho kimewekeza sana katika tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati na hivyo kujibu kilio cha watu wa Mungu. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu mkubwa unaotolewa na Mama Kanisa. Elimu ni njia makini ya kujenga utu wa binadamu. Huu ni urithi mkubwa wa kiutamaduni na maisha ya kiroho unaotoa utambulisho wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.” Kuelimisha maana yake ni kuwasha moto wa elimu unaoweza kushuhudiwa na mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake. Hii ni historia ya miaka 100 inayong’arishwa na imani, elimu, ujuzi na maarifa, tayari kujielekeza kwa siku za usoni na matumaini ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, huo ni utamaduni wa kutupa. Chuo kikuu ni mahali pa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini sanjari na mchakato wa malezi mtambuka unaotekelezwa na wadau mbalimbali ndani ya jamii.
Hii ni dhamana ya majaalimu wa Chuo kikuu, wanaopaswa kuhakikisha kwamba, moto huu unaendelea kuwaka hadi kieleweke. Elimu isaidie kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, ili kujibu maswali msingi yanayotolewa na jamii, bila woga wala makunyanzi. Ukweli, uwazi na ukarimu ni amali za kijamii zinazopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maridhiano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbalimbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine. Jubilei ya Miaka 100 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” ni fursa ya kukua, kukomaa na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Chuo kikuu ni mahali pa kuwafunda vijana wa kizazi kipya kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma. Huu ni ushuhuda unatolewa na wadau mbalimbali chuoni hapo katika tafiti makini, dhamana na wajibu kitaifa na kimataifa bila kuwasahu wafanyakazi wote wanaojisadaka ili kuhakikisha kwamba, maisha na shughuli mbalimbali chuoni hapo zinasonga mbele, sawa na vyombo vya muziki vinavyounganishwa na kutoa muziki unaopendeza. Chuo kikuu cha Kikatoliki hakina budi kujikita katika diplomasia kwa ajili ya ujenzi wa misingi ya haki na amani duniani.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Siku ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Swali la siku zijazo. Vijana kati ya kukata tamaa na tamaa." Kwa Umombo linasomeka: “Question of the future. Young people between disenchantment and desire", Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 14 Aprili 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini pamoja na wageni waliohudhuria Sala ya Malkia wa Mbingu kwamba, Dominika tarehe 14 April 2024, kwamba, nchini Italia, Kanisa limefanya kumbukumbu ya Siku ya Mia Moja kwa ajili ya kuombea Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.” Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kukutia shime ili kiweze kusonga mbele na huduma yake muhimu katika kuwafunda wanafunzi, wawe waaminifu kwa maisha na utume wao, makini kwa kusikiliza na kujibu hitaji hili msingi miongoni mwa vijana sanjari na wadau wa elimu.
Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Mario Delpin wa Jimbo kuu la Milano, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku ya Mia Moja ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” anakazia umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Katika kipindi cha miaka mia moja cha uwepo wake, kimechangia sana ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Vyuo vikuu vya Kikatoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia vinaendelea kutoa mchango mkubwa katika kutafuta, kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Vyuo hivi vimekuwa ni majukwaa ya tafiti za kisayansi, malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya, mahali ambapo upendo na ukarimu vinakutana. Dominika tarehe 14 Aprili 2024 Mama Kanisa amefanya kumbukizi ya Miaka 40 tangu vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia, walipokutana kwa mara ya kwanza, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi kuanzia tarehe 25 Machi hadi tarehe 22 Aprili 1984 na huo ukawa ni mwanzo wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni. Leo hii Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” ni kati ya vyuo vikuu vyenye umaarufu mkubwa sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Yohane Paulo II akawakabidhi vijana Msalaba, alama ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, maisha na utume wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kwa kikatoliki katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Naye, Askofu Claudio Giuliodori, Mratibu mkuu wa Masuala ya Kikanisa nchini Italia ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kumbukizi ya Siku ya Mia Moja ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.” Katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa waamini kuendelea kuboresha, kuitangaza na kuishuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Waamini waboreshe maisha yao ya kiroho kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, zawadi kubwa ya Kristo Mfufuka. Ikumbukwe kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacra cuore” ni matunda ya majadiliano katika ukweli na uwazi, kati ya waalimu na wanachuo, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika mshikamano na haki. Hapa ni mahali ambapo Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI linataka pawe ni mahali pa kurithisha ujuzi, maarifa, stadi za maisha; imani, matumaini na mapendo thabiti. Ni mahali pa kuwafunda vijana wa kizazi kipya ili wawe ni wadau katika ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi; inayokita mizizi yake katika ustawi na maendeleo; udugu, haki na amani. Ni jukumu la watu wa Mungu kutoka katika medani mbalimbali za maisha kuwasaidia vijana wa kizazi kipya, waweze kukutana na Kristo Mfufuka katika uhalisia wa maisha yao, ili hatimaye, waweze kuwa wabunifu na mashuhuda hai wa Kristo Mfufuka. Hiki ni chuo ambacho kinabeba jina la Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na msamaha. Chuo katika ujumla wake, kinapaswa pia kuwa ni shuhuda wa Kristo Yesu Mfufuka, mahali pa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya; chemchemi ya matumaini na jukwaa na ushirikiano na mshikamano wa kitamaduni na huduma kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake.