Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Watoto Ulimwenguni 25-26 Mei 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Kristo Yesu katika maisha na utume wake alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto ambao wanapaswa kujifunza na kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Mshikamano wa upendo, umewawezesha watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao kiasi cha kujinyima na kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao! Leo hii, haki msingi za watoto sehemu mbalimbali za dunia zinaendelea kuvunjwa, kiasi kwamba, watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa; wanapokwa haki yao ya utoto kwa kufanyishwa kazi za suluba; kwa kusumbuliwa na: umaskini, magonjwa, ujinga, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; kwa vita na majanga mbalimbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu! Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari, mwamko na moyo wa kimisionari, kwa kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya. Wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kuu akatangaza kwamba, tarehe 25 na 26 Mei 2024 itakuwa ni Siku ya Watoto Ulimwenguni, “World Children’s Day, WCD” itakayoadhimishwa kwa mara ya kwanza mjini Roma. Baba Mtakatifu alikuwa anajibu ombi lililotolewa na Mtoto Alessandro Lomonaco kutoka Italia, aliyemwomba Baba Mtakatifu kufikiria kuanzishwa kwa Siku ya Watoto Ulimwenguni.
Maadhimisho haya yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Ni shauku ya Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inakirithisha kizazi kipya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake kwa kutoa kipaumbele cha kwanza watoto, Mama Kanisa naye katika maisha na utume wake anataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto, kwa kuwapatia malezi makini, kwa kuwalinda na kuwaendeleza. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni Kwa Mwaka 2024 anawakumbusha watoto kwamba, wao wana thamani kubwa sana machoni pa Mungu na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kaulimbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5. Baba Mtakatifu anawaalika watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuguswa na historia ya watu mbalimbali katika maisha yao, bila kuwasahau watoto wanaoteseka kwa magonjwa, watoto ambao wamepokwa utoto wao na kwa sasa wanateseka sana. Hawa ni watoto wanaoathirika kutoka na vita na kinzani za kijamii; watoto wanaoteseka kwa baa la njaa na kiu; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto wanaolazimishwa kwenda kwenye mstari wa mbele kama chambo cha vita; watoto wanaokimbia kutoka kwenye familia zao kama wakimbizi na wahamiaji; watoto wanaotenganishwa na familia zao, kiasi cha kukosa fursa ya kuendelea tena na masomo; watoto wanaotumbukiwa kwenye magenge ya uhalifu Kitaifa na Kimataifa; watoto wanaoathirika kwa matumizi haramu ya dawa za Kulevya, Watoto wanaotumbukizwa kwenye mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.
Hawa ni watoto wanaopaswa kusikilizwa, ili kutolea sauti yao ushuhuda na hivyo kuonjeshwa tena huruma na upendo. Baba Mtakatifu anawatia shime watoto hawa kuwa na furaha kwa sababu wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Wajenge na kudumisha urafiki kwa kushirikishana na wengine, katika uvumilivu, ujasiri, ubunifu, hali ya kufikirika bila woga wala maamuzi mbele. Siri kuu ya maisha inasimikwa katika sala, ambayo Kristo Yesu amewafundisha wafuasi wake, ile Sala kuu, Sala ya Baba Yetu, itakayo wachangamotisha kuwa ni wajenzi wa dunia inayosimikwa, katika utu, haki na amani. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni, Dominika tarehe 14 Aprili 2024 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba Mtakatifu amewakumbuka watoto wote wanaoathirika na vita pamoja na misigano ya kijamii, kutoka Ukraine, Palestina, Israel, Myanmar pamoja na sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwaombea watoto hawa pamoja na kuombea amani ya kudumu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 25 na 26 Mei 2024, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa litakuwa linaadhimisha pia Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni inayonogeshwa na kaulimbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote na watu wenye mapenzi mema kusindikiza hija hii kwa sala na sadaka na kwamba, anawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho haya. Baba Mtakatifu anawaambia watoto kwamba, anawasubiri wote kabisa kwa hamu na shauku kubwa, kwa sababu Kanisa na jamii katika ujumla wake, ina kiu ya furaha ya watoto, shauku na hamu ya kuwa na ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika msingi wa haki, amani na maridhiano. Tayari watoto kutoka katika mataifa 80 wamekwisha kujiandikisha ili kuhudhuria Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni kuanzia tarehe 25 Mei 2024 kwenye Uwanja wa Michezo wa Olimpico, Roma na maadhimisho haya yatahitimishwa tarehe 26 Mei Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.