Jumatano tarehe 10 Aprili 2024 Maaskofu kutoka Sardegna, wakiwa wameandama na watu wa Mungu kutoka Sardegna wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Jumatano tarehe 10 Aprili 2024 Maaskofu kutoka Sardegna, wakiwa wameandama na watu wa Mungu kutoka Sardegna wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.  (Vatican Media)

Maaskofu Katoliki Italia Wanafanya Hija ya Kitume Mjini Vatican

Papa anawaalika waamini kila mtu ajitahidi kuishi kadiri ya wajibu na utume wake ndani ya Kanisa na kwamba, mchakato wa malezi, makuzi na elimu uendane na tunu msingi za Kikristo. Waamini wawe mstari wa mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, amani ya waja wake, na kwamba, amewakirimia fadhila ya nguvu na wala si woga ili kupambana na maadui wa ndani, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kanisa hili la Kristo Yesu, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Mtakatifu Petro, ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kondoo na wanakondoo wake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili na yanayojitegemea na ya jumla kwa ajili ya huduma ya roho za watu “Curam animalum.” Hivyo basi, kwa kuwa amewekwa kuwa Mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote na ya Kanisa zima na pia ya Makanisa mahalia, anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote. Kwa upande mwingine na Maaskofu wamewekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya Mamlaka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Rej. Christus Dominum, n. 2-3.

Papa Francisko anawaalika waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka
Papa Francisko anawaalika waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka

Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Kwa busara yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani. Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Hija hizi ni za manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.”

Maaskofu Katoliki Italia wanafanya hija ya kitume mjini Vatican, 2024
Maaskofu Katoliki Italia wanafanya hija ya kitume mjini Vatican, 2024

Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia katika muktadha wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Baba Mtakatifu Francisko anakazia zaidi utamaduni wa kusikiliza na kujifunza kutoka katika Makanisa mahalia. Ni katika muktadha wa hija za kitume, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linafanya hija wakati huu na Jumatano tarehe 10 Aprili 2024 Maaskofu kutoka Sardegna, wakiwa wameandama na watu wa Mungu kutoka Sardegna wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kila mtu ajitahidi kuishi kadiri ya wajibu na utume wake ndani ya Kanisa na kwamba, mchakato wa malezi, makuzi na elimu uendane na tunu msingi za Kikristo. Waamini wawe mstari wa mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, amani ya waja wake, na kwamba, amewakirimia fadhila ya nguvu na wala si woga ili kupambana na maadui wa ndani, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa ari na moyo mkuu. Vijana, wazee, wagonjwa na wanandoa wapya, wakuze ndani mwao mwanga wa faraja, ili kutangaza Fumbo la Pasaka, kwa kuimarisha imani na matumaini kwa Kristo Mfufuka tayari kuanza safari na utimilifu wa maisha. Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza mawazo yake kwa watu wa Mungu nchini Ukraine, Palestina na Israeli, ili Kristo Mfufuka aweze kuwakirimia amani ya kudumu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba vita imeenea sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Myanmar pamoja na wale wote wanaoteseka kutokana na madhara ya vita sehemu mbalimbali za dunia. Amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kamwe wasichoke kusali na kuombea haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ad Limina

 

11 April 2024, 14:54