Mahujaji Kutoka Tanzania Wakutana na Papa Francisko Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” kama sehemu ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu anasema, uzoefu na mang’amuzi ya hija, yaani safari ya maisha ya kiroho ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Ikumbukwe kwamba, maisha ya mwanadamu ni hija kuelekea mbinguni kwa Baba wa milele. Hija inahitaji maandalizi, sadaka na majitoleo. Kimsingi hija inapania kuwa ni nyenzo ya toba na wongofu wa ndani, ili kuomba tena huruma, neema na baraka za Mwenyezi Mungu katika maisha na utume. Mahujaji 43 kutoka Parokia ya Mtakatifu Maria De Mattias, Mivumoni, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, tangu tarehe 21 Aprili 2024 hadi tarehe 27 Aprili 2024 wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria na maisha ya kiroho nchini Italia, ili kushuhudia huruma na upendo wa Mungu uliotangazwa na mashuhuda wa imani. Wamepata nafasi ya kushiriki katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 24 Aprili 2024 ambayo ilijikita katika fadhila tatu za Kimungu ambazo ni: Imani, Matumaini na Mapendo. Rej. KKK 1814. Mababa wa Kanisa wanasema, fadhila za kimungu zinaweka msingi, zinahuisha, na kuainisha utendaji adili wa Mkristo. Zinapasha habari na kuzihusisha fadhila zote za maadili. Zinamiminwa na Mwenyezi Mungu katika roho za waamini kuwawezesha kutenda kama watoto wake na kustahili uzima wa milele. Nazo ni amana ya uwepo na tendo la Roho Mtakatifu katika nguvu za binadamu. Rej. KKK 1813. Matendo makuu ya Mungu! Mahujaji wanasema wamemwona Baba Mtakatifu “mubashara.” Baba Mtakatifu amewaambia mahujaji na wageni waliofika kwenye Katekesi yake kwamba, anawaombea ili waendelee kuimarisha ndani mwao fadhila imani katika Kristo Yesu, upendo kwa watu wote wa Mungu pamoja na fadhila ya matumaini, kwa ajili ya maisha na uzima wa milele mbinguni.
Mahujaji kutoka Tanzania wamepata fursa ya kutembea mji wa Acuto, kwenye Nyumba Mama ya Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC. Hili ni Shirika lililoanzishwa kunako tarehe 4 Machi 1834 huko Acuto, Jimbo Katoliki la Anagni na Mtakatifu Maria De Mattias aliyezaliwa tarehe 4 Februari 1805. Katika maisha yake ya ujana aliguswa sana na mahubiri ya Mtakatifu Gaspar de Bufalo kuhusu tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo, chemchemi ya huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Akachomwa moyoni mwake kutaka kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika kazi ya ukombozi. Mtumishi wa Mungu Yohane Merlin alimsindikiza Mtakatifu Maria De Mattias katika maisha na utume wake. Mtakatifu Maria de Mattias aliishi wakati wa Mapinduzi ya Mfalme Napoleone Bonaparte wa Ufaransa. Katika hali na mazingira kama haya, kulikuwepo na umaskini mkubwa wa hali na kipato, bila kusahau kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Mtakatifu Maria De Mattias akajisadaka kwa ajili ya kusaidia upyaisho wa maisha ya watu wa Mungu nchini Italia kwa kutoa elimu makini na katekesi kwa wasichana, kama chachu ya ukombozi. Mtakatifu Maria De Mattias alifariki dunia tarehe 20 Agosti 1866, akiwa na umri wa miaka 61. Kunako tarehe 1 Oktoba 1950 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio wa XII. Hatimaye, Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2003 akamtangaza kuwa Mtakatifu Mtakatifu Maria De Mattias anasema katika Shirika hili misaada itapatikana muda wote na mahali popote. Hii ni ndoto ya Mtakatifu Maria De Mathias, ambayo inaendelea kujidhihirisha kwa kuongezeka kwa Masista Waabuduo Damu Takatifu, ambao wako tayari kutumwa na Yesu kukusanya mavuno yake ulimwenguni pote.
Mashuhuda wa huruma na imani: Hawa ni kama akina Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, Mtakatifu Rita wa Cascia na Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mlinzi na Mwombezi wa Italia pamoja na Mtakatifu Clara wa Assisi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina aliwasaidia watu wa Mungu kugundua hazina ya maisha ya upendo wa Mungu kwa kuonja na kuguswa na msamaha na huruma ya Mungu. Padre Pio amekuwa ni mtumishi mwaminifu wa huruma ya Mungu, mtume aliyesikiliza kwa makini, akaganga na kuponya madonda ya dhambi katika maisha ya kiroho kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kusaidia kurejesha amani mioyoni mwa watu wengi. Padre Pio alikuwa ni fundi mkubwa wa kuwapatia waamini harufu ya msamaha wa Mungu, uliokuwa unabubujika kutoka kwa Kristo Yesu mteswa, njia ya huruma ya Mungu. Padre Pio alibahatika kuwapatia watu wengi waliokuwa wanateseka, upendo na huruma ya Mungu. Akafanikiwa kubeba ndani mwake Fumbo la mateso akawa kweli ni mfereji wa huruma ya Mungu uliolowanisha majangwa ya nyoyo za watu, akawajengea watu wengi chemchemi ya maisha mapya.
Kila mwaka ifikapo tarehe 22 Mei, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Rita wa Cascia aliyezaliwa kunako mwaka 1381 huko Roccaporena. Akafariki dunia tarehe 22 Mei 1457 na kutangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 24 Mei 1900 na Baba Mtakatifu Leo XIII. Ni mwanamke wa shoka, aliyeweza kuvumilia ndoa shuruti kwa muda wa miaka 18, akiwa anamwombea mumewe ili aweze kutubu na kuongoka! Katika kumbukumbu ya miaka 18 ya ndoa yao, mumewe akauwawa kikatili katika ugomvi! Kifo hiki kiliacha machungu katika familia ya Mtakatifu, ambaye, watoto wake walitaka kulipiza kisasi, ili “kumwonesha cha mtema kuni” yule aliyesababisha kifo cha baba yao! Mawazo haya yakeleta majonzi makubwa tena katika maisha ya Mtakatifu Rita wa Cascia, akawaombea watoto wake ili wasilipize kisasi, akafanikiwa na watoto hawa wakawa ni mashuhuda wa huruma na msamaha katika maisha yao, kiasi hata cha kuitupa mkono dunia wakiwa katika hali ya neema! Katika hali ya upweke na majonzi makuu, Rita wa Cascia akajiunga na maisha ya kitawa, akawa kweli ni chemchemi ya huruma na upendo kwa jirani pamoja na watawa wenzake. Mtakatifu Rita wa Cascia ni mfano bora wa kuigwa katika kusamehe na kusahau bila kulipiza kisasi. Ni mfano wa upendo wa kidugu unaofumbatwa katika msamaha wa kweli; sala na toba ya ndani! Waamini wanahamasishwa kushinda ubaya kwa wema, kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Mtakatifu Rita wa Cascia aliupenda sana Msalaba, akaukumbatia katika maisha yake! Alijifunza kwamba, Msalaba ni ufunuo wa hekima, huruma na upendo wa Mungu na kwake ukawa ni kimbilio la maisha na chechemi ya upendo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanahamasishwa kuwa ni wajenzi na mashuhuda wa Ufalme wa Mungu. Mtakatifu Rita wa Cascia awe ni mwombezi wa familia zinazokabiliana na changamoto na matatizo mbali mbali. Mtakatifu Rita wa Cascia awawezeshe waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kujenga mtandao wa mshikamano wa upendo, katika kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mtakatifu Rita wa Cascia awe ni mfano bora wa kuigwa katika imani, ukarimu, amani na maridhiano kati ya watu!
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 4 Oktoba anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mlinzi na Mwombezi wa Italia, aliyeishi kati ya Mwaka 1181 hadi tarehe 3 Oktoba 1226. Alibatizwa na kupewa jina la Yohane, akachezea ujana wake kwa kupenda sana anasa na matanuzi ya “kufa mtu.” Lakini baadaye alitubu na kumwongokea Mungu, kiasi cha kusadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa maskini na wakoma waliokuwa wametengwa. Akajitahidi kumfuasa Kristo Yesu, Mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Katika maisha yake, Mtakatifu Francisko wa Assisi alishangazwa sana na huruma, upendo na unyenyekevu wa Mungu, uliopelekea hata akatungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akazaliwa na Bikira Maria Pangoni, mahali pa kulishia wanyama. Safari hii ya unyenyekevu, ya Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ikapata maana ya pekee kama “Njia ya Msalaba” hata akatundikwa na kufa Msalabani, kifo cha aibu. Hii ni sadaka inayoendelezwa na Mama Kanisa katika Ibada ya Misa Takatifu inayotolewa sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Francisko wa Assisi alijisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu kwenye nchi za Kiislam huku akitumia silaha ya IMANI na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kidini na kwamba, alikuwa tayari kuyamimina na maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.