Mkutano Mkuu wa Shirika la Mabruda wa Shule za Kikristo: Huruma, Upendo na Ushuhuda
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Shirika la Mabruda wa Shule za Kikristo “Fratelli dell’Istruzione Cristiana di Ploërmel” na Kwa Lugha ya Kilatini linajulikana kama “Institutum Fratrum instructionis christianae de Ploërmel” lilianzishwa tarehe 6 Juni 1819 huko Saint-Brieuc na Padre Jean-Marie de La Mennais (1780-1860) pamoja na Padre Gabriel Dashayes (1767-1841) ili kukabiliana na kuenea kwa shule za kiraia huko Brittany. Shirika lilipata kibali cha sifa tarehe 7 Januari 1851 na Katiba ya Shirika ikaidhinishwa na Vatican tarehe 1 Machi 1910. Karama ya Shirika inajikita katika uinjilishaji wa watoto na vijana kwa njia ya elimu na kwamba, Shirika kwa sasa linajiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwake. Shirika limeenea sehemu mbalimbali za dunia na Barani Afrika linafanya utume wake nchini: Benin, DRC, Pwani ya Pembe, Kenya, Rwanda, Senegal, Tanzania na Togo. Waanzilishi wa Shirika la Mabruda wa Shule za Kikristo walijiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, wakajisadaka kwa ajili ya huduma ya maendeleo fungamani ya binadamu wote. Hii ni changamoto ya kuendelea kuhifadhi na kuendeleza lengo na waasisi wa Shirika.
Wajumbe wa Mkutano mkuu wa Shirika la Mabruda wa Shule za Kikristo “Fratelli dell’Istruzione Cristiana di Ploërmel”, Jumatatu tarehe 22 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuendelea kuwa kielelezo cha Mababa wenye huruma; Kanisa ni familia ya Mungu yenye karama na miito mbalimbali, kwa ajili ya wokovu wa binadamu ni mwaliko kwa wanashirika kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Baba Mtakatifu anasema, Shirika hili linatekeleza dhamana na wajibu wake katika ulimwengu ambao umegubikwa na umaskini, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na migogoro mbalimbali ya kijamii. Kumbe, huu ni mwaliko kwa wao kuwa ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu, kwa kujisadaka bila ya kujibakika kwa ajili ya huduma kwa watoto na vijana, kwa kuwa makini kwa matarajio yao ya baadaye, daima wakimwelekea Kristo Yesu, kama kanuni msingi ya maisha na utume wao.
Wito na maisha yao, yanawasukumwa kwenda mahali ambapo wengine hawapendi kwenda, pembezoni mwa jamii, kati ya watu wanaokataliwa na kutengwa na jamii, miongoni mwa wahanga wa vita, ili kweli uwepo wao uweze kuwa ni mng’ao wa matumaini kwa wengi. Hawa ni watoto, vijana na watu ambao ndoto yao ya maisha imeyeyuka na kupotea. Ni wajibu wa Shirika la Mabruda wa Shule za Kikristo kuwasaidia ili waweze kuishi ndoto yao, kuamini sanjari na kuitekeleza. Inashangaza na kusikitisha sana kuona watoto wakicheza hata kwenye mashambuzi ya kivita, lakini ni watoto ambao wamepokwa ile furaha ya utoto wao. Huu ni mwaliko kwa Mabruda hawa kuhakikisha kwamba, wanawasaidia watoto hawa kuwa na furaha tena. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, Kanisa ni familia moja yenye karama na miito mbalimbali, kumbe wanaalikwa kushirikiana kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, kwa kuonesha ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anawaalika wahakikishe kwamba, wanashirikiana na Makanisa mahalia pamoja na majimbo katika kutekeleza dhamana na wito wao miongoni mwa watu watakatifu na wateule wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na roho ya kiburi na majivuno; uchoyo na ubinafsi wa kutaka kujifungia wenyewe; mipasuko na migawanyiko na umbea usiokuwa na mvuto wala mashiko. Watu wateule na watakatifu wote wa Mungu wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuwa Kanisa kuna maanisha kuwa watu wa Mungu, kuendana na mpango mkuu wa upendo wake wa kibaba na chachu ya Mungu katikati ya wanadamu, tayari kutangaza na kuuleta wokovu wa Mungu katika ulimwengu. Kanisa linapaswa kuwa ni mahali pa huruma inayotolewa bure, mahali ambapo kila mtu anahisi kukaribishwa, kupendwa, kusamehewa na kuhamasishwa aishi maisha mazuri ya Injili. Rej. Evangelii gaudium, 114. Baada ya maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Shirika, wajumbe watajiweka wakfu kwa Moyo safi wa Bikira Maria, tayari kuitikia “ndiyo” kama alivyofanya Bikira Maria, tayari kujizatiti katika huduma inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, imani kwa Mungu sanjari na kutangaza na kushuhudia ile furaha ya kuwa wahudumu wa upendo, huruma na msamaha wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia baraka zake za kitume wao pamoja na vijana wanaowasindikiza.