Mtandao wa Shule za Amani Kitaifa Italia: Amani na Utunzaji Bora wa Mazingira
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Vita ina madhara makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, inakwenda kinyume kabisa cha misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wahusika wa vita inayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao ni wahalifu wa kimataifa wanapaswa kushughulikiwa kikamilifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, haki na amani ni amana inayosimikwa katika ujasiri na majadiliano katika msingi wa ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baadhi ya Mataifa kutaka kujimwambafai, kunyonya na kudhalilisha Mataifa mengine, kimekuwa ni chanzo cha migogoro ya kivita sehemu mbalimbali za dunia. Kuna haja ya kuondokana na dhana ya uadui na badala yake Jumuiya ya Kimataifa ijielekeze katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika umoja na utofauti, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa ni shuhuda na chombo cha haki na amani duniani. Huu ni wakati muafaka wa kusimama kidete anasema Baba Mtakatifu Francisko kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, bila kusahau utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Ni katika muktadha huu, amani ya kweli inajipambanua kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano na hofu ya Mungu. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini.
Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano. Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mchakato fungamanishi unaopania kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kuondokana na upweke hasi, kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini. Hali hii itawasaidia vijana wengi kuondokana na ugonjwa wa sonona; utumwa mamboleo, chuki, uhasama, matusi, ukatili pamoja na uonevu mitandaoni. Mtandao wa Shule za Amani Kitaifa Nchini Italia: “Rete Nazionale Scuole di Pace” ulizaliwa baada ya miaka mingi ya kazi iliyolenga kukuza ushirikishwaji wa kudumu wa elimu ya: amani na haki msingi za binadamu katika programu za shule katika ngazi mbalimbali. Uelimishaji wa amani ni mchakato mgumu sana katika maisha, lakini una umuhimu wa pekee. Changamoto zinazoletwa na msukosuko huo na ulimwengu unaobadilika kwa kasi unahitaji uwekezaji mpya, nishati mpya, ujuzi mpya, uwezo na tabia thabiti. Ndiyo maana ni muhimu sana kuunganisha nguvu na kuendeleza "muungano wa ufundishaji" wa vyama vyote vinavyohusika.
Ni katika muktadha huu pamoja na Uratibu wa Kitaifa wa Mamlaka za Mitaa kwa ajili ya Amani na Haki za Binadamu na Meza ya Amani, tangu mwaka 1995, wameamua kuhamasisha ujenzi wa mtandao wa shule na mamlaka za mitaa zinazohusika na kuwaelimisha vijana kwa ajili ya amani, kwa haki msingi za binadamu uraia, na wajibu. Ni katika muktadha wa haki, amani na elimu, Mtandao wa Shule za Amani Kitaifa nchini Italia, Ijumaa tarehe 19 Aprili 2024 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kupanda ndoto ya amani, itakayozaa matunda kwa siku za usoni. Watoto watambue kwamba, wao ni wadau wa amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mtandao usaidie kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, jambo ambalo wanapaswa kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao! Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaounda mtandao shule za amani Kitaifa nchini Italia, kwa ari na mwamko wao unaowawajibisha kupambana bila kuchoka na ukosefu wa haki na vita; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuendelea kuwa na ndoto kubwa, ili kuishi kwa kuwajibika, tayari kupandikiza mbegu ya amani itakayozaa matunda kwa siku za usoni. Mwezi Juni 2020, Jumuiya ya Kimataifa iliadhimisha kumbukizi ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa; kwa Tamko la Nchi Wanachama lililojumuisha ahadi 12 muhimu pamoja na ombi lililotolewa kwa Katibu mkuu la mapendekezo ya kushughulikia changamoto mamboleo na zile zijazo; mchakato wa kupyaisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu pamoja na kuendeleza ahadi zilizomo kwenye Azimio la UN75.
Ripoti hiyo, ilitoa wito kwa Mkutano wa Kilele wa Wakati Ujao kuunda makubaliano mapya ya kimataifa juu ya kujitayarisha kwa siku zijazo ambazo zimejaa hatari lakini pia fursa. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilikaribisha kuwasilishwa kwa ripoti katika mkutano utakao adhimishwa kuanzia tarehe 22-23 Septemba 2024, ukitanguliwa na mkutano wa Mawaziri ulioadhimishwa kunako mwaka 2023. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hili ni tukio kubwa kumbe, wanapaswa kushiriki kikamilifu, vinginevyo maamuzi haya mazito yanaweza “kubaki kwenye karatasi.” Kumbe, maamuzi haya yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia mabadiliko na kwamba, wao wanapaswa kuwa ni wadau wakuu katika mabadiliko, kwa kushirikiana na wengine, kwa kuhakikisha kwamba, watu wenye ridhaa ya kuwaongoza watu wa Mungu: kijamii na kisiasa wanatekeleza nyajibu zao msingi. Kumbe, kuna haja ya kujenga mtandao utakaojizatiti kwa kufanya kazi kwa pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anakaza kusema kunahitaji ujasiri ili kuweza kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika sura ya nchi. Changamoto hizi ni pamoja na: athari za mabadiliko ya tabia nchi, masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na utekelezaji kwa nguvu zao pamoja na msaada wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka kujikita katika kujenga na kudumisha amani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, kinzani wala mipasuko ya kijamii bali ni matunda ya haki, maendeleo, mshikamano wa udugu wa kibinadamu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko wa kusikiliza mahitaji msingi ya binadamu, tayari kuganga na kutibu madonda ya watu kama vyombo vya huruma na uponyaji; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini, ili kujenga jamii jumuishi inayofumbatwa katika msingi wa amani na majadiliano. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika kipindi hiki ambacho vita inatawala sehemu mbalimbali za dunia, kwamba, wanahamasishwa kuwa vyombo na mashuhuda wa amani; kwa kujenga kesho inayosimikwa katika mshikamano, ili mazingira nyumba yetu ya pamoja yanakuwa ni mahali pa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, mshikamano na amani kwa kuonesha kwamba, kila mtu anajali.