Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Aprili 2024 anakita mawazo yake kwa kuangalia dhamana ya wanawake katika jamii. Wanawake sehemu mbalimbali za dunia hawapewi uzito unaostahili. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Aprili 2024 anakita mawazo yake kwa kuangalia dhamana ya wanawake katika jamii. Wanawake sehemu mbalimbali za dunia hawapewi uzito unaostahili. 

Nia za Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mwezi Aprili 2024: Dhamana ya Wanawake

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Aprili 2024 anakita mawazo yake kwa kuangalia dhamana ya wanawake katika jamii. Wanawake sehemu mbalimbali za dunia hawapewi uzito unaostahili. Kuna nchi ambazo wanawake wamekatazwa kupata misaada, kufungua biashara au kwenda shule. Katika maeneo kama haya wanawake wako chini ya sheria zinazowafunga wavae na kuonekana kwa njia fulani. Bado ukeketwaji unafanywa kwa baadhi ya nchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kuona kwamba, bado mfumo dume unaendelea kutawala na kuwanyanyasa wanawake kana kwamba, wao ni watu wa daraja la pili duniani! Kuna wanawake wengi ambao wanatumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Haya ni mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki zao msingi. Wanawake wanayo dhamana na utume katika jamii na Kanisa katika ujumla wake. Wana utajiri na karama nyingi zinazopaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Chuki, uhasama na mauaji ya wanawake ni mambo ambayo yamepitwa na wakati. Wanawake wana karama ya kuvumilia mateso kwa ajili ya ustawi wa watoto wao pamoja na kuendeleza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anasema kuna mifano ya wanawake wengi ambao wanaendelea kujisadaka kama vyombo na mashuhuda wa upendo kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake sehemu mbalimbali za duniani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia umuhimu wa waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kushirikiana na kufungamana na viongozi wa Kanisa na kwamba, vyama vya kitume vina mchango mkubwa katika kuimarisha Jumuiya za Kikanisa. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, kati ya wafuasi wake wa karibu, walikuwepo pia wanawake waliofuatana naye katika mahubiri yake. Wanawake waliokuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa. Kati yao ni Mariamu aitwaye Magdalena aliyekuwa na imani na upendo mkuu kwa Kristo Yesu, kiasi cha kuwa ni mfuasi wa kwanza kushuhudia Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Akawa ni Mtume kwa Mitume wa Yesu ili kuwatangazia kwamba, Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kuzikwa, amefufuka.

Uwepo wa wanawake katika medani mbalimbali za maisha ni muhimu sana
Uwepo wa wanawake katika medani mbalimbali za maisha ni muhimu sana

Baba Mtakatifu anasema, dhamana na wajibu wa wanawake katika kuelimisha udugu wa kibinadamu ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa udugu na amani; changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Dhamana na wajibu wa wanawake kama waelimishaji wa udugu wa kibinadamu bado haijatambuliwa na kuthaminiwa sana kutoka na matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo wanawake; changamoto ambazo kimsingi zinajikita katika utu na dhamana yao. Wanawake na watoto ni waathirika wakuu wa machafuko, vita na kinzani za kijamii. Pale ambapo kuna chuki na uhasama waathirika wakuu ni familia na jamii husika kiasi cha kuwazuia wanawake kutekeleza dhamana na wajibu wao, hata kama wana nuia mamoja; vitendo vya wanaume wakati mwingine vinakwamisha juhudi za wanawake kutekeleza dhamana yao ya kuelimisha udugu kwa ufasaha zaidi. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuwathamini na kuwaenzi wanawake katika jamii na ulimwengu mamboleo kwa kutambua uwezo wao wa kuelimisha udugu duniani, kwani wana uwezo mkubwa wa kurithisha karama na mapaji yao kwa jamii kwa kukazia umoja wa familia ya binadamu. Uwepo wa wanawake katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu ni msaada mkubwa katika ngazi: mahalia, kitaifa na kimataifa bila kusahau nafasi yao katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake wana haki ya kutekeleza dhamana na wajibu wao katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu; kwa kuhakikisha kwamba, haki zao zinalindwa na kudumishwa kisheria. Wanawake washirikishwe kikamilifu katika uhalisia wa maisha.

Dhamana na wajibu wa wanake katika maisha ya kijamii
Dhamana na wajibu wa wanake katika maisha ya kijamii

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Aprili 2024 anakita mawazo yake kwa kuangalia dhamana ya wanawake katika jamii. Wanawake sehemu mbalimbali za dunia hawapewi uzito unaostahili. Kuna nchi ambazo wanawake wamekatazwa kupata misaada, kufungua biashara au kwenda shule. Katika maeneo kama haya wanawake wako chini ya sheria zinazowafunga wavae na kuonekana kwa njia fulani. Bado ukeketwaji unafanywa kwa baadhi ya nchi. Baba Mtakatifu anasema, jamii isiwanyime wanawake sauti zao. Wanawake walionyanyasika, wakanyonywa na kutengwa kamwe wasinyang’anywe sauti zao. Kwa nadharia jamii inakubali kwamba wanaume na wanawake wana hadhi sawa ya utu na heshima ya binadamu. Lakini jambo hili halifanyiki kwa vitendo. Serikali zinapaswa kujizatiti kikamilifu ili kuondoa sheria za kibaguzi kila mahali na hivyo kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba haki, utu na heshima ya wanawake zinalindwa na kuendelezwa. Wanawake wanapaswa kuheshimiwa, hii ni pamoja na kuheshimu utu na haki zao msingi. Kwa kushindwa kufanya hivi, jamii itashindwa kuendelea. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali ili kwamba, utu, heshima na haki msingi za wanawake zitambulikane katika kila tamaduni na hivyo kukomesha ubaguzi wanaokumbana nao sehemu mbalimbali za dunia.

Nia za Papa Mwezi Aprili
16 April 2024, 16:48