Papa Francisko Asikitishwa na Kifo cha Padre Matteo Pettinari, Mmisionari wa Consolata
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika tarehe 21 Aprili 2024 kwa masikitiko makubwa alisema kwamba, amepokea kwa uchungu mkubwa taarifa za kifo cha Padre Matteo Pettinari, I.M.C wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, aliyefariki dunia tarehe 18 Aprili 2024 kwa ajali ya gari, huko nchini Pwani ya Pembe. Baba Mtakatifu anasema Padre Matteo Pettinari, I.M.C alifahamika na wengi kuwa ni “Msionari mchapakazi” ambaye katika maisha na utume wake kwa muda wa miaka 17 kama Mtawa na Miaka 13 kama Padre wa Consolata ameacha ushuhuda mkubwa wa huduma ya ukarimu wa Kiinjili. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kumkumuka na kumwombea, ili apate pumziko na maisha ya uzima wa milele.
Padre Matteo Pettinari, I.M.C., alizaliwa mwaka 1981 huko Chiaravalle, huko Ancona, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa mwaka 2006 akaweka nadhiri zake za daima na tarehe 11 Septemba 2010 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Novemba mwaka 2011 akatumwa na Shirika kwenda Dianra, Kaskazini mwa Pwani ya Pembe ambako alijihusisha sana na huduma kwa maskini na watu waliokuwa na changamoto ya afya ya akili. Alikuwa ameanza ujenzi wa Kanisa na hospitali kwa ajili ya maskini, lakini amekumbana na kifo cha ghafla.
Mheshimiwa Padre James Bhola Lengarin, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Consolata pamoja na Padre Pedro Louro, Katibu mkuu wa Shirika wanawaalika wanashirika pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumkumbuka na kumwombea Marehemu Padre Matteo Pettinari, I.M.C wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, aliyefariki dunia tarehe 18 Aprili 2024 kwa ajali baada ya gari lake kugonga uso kwa uso na Bus huko nchini Pwani ya Pembe ili apate maisha na uzima wa milele. Bikira Maria Mfariji, awafariji na kuwaombea amani. Wakati wa mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, mwaka 2022, alishiriki kikamilifu katika kampeni dhidi ya UVIKO-19 nchini Pwani ya Pembe na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Mashuhuda wanakiri kwamba, Marehemu Padre Matteo Pettinari, I.M.C ni mmisionari aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya huduma ili kuboresha maisha ya watu wa Mungu, alionesha moyo wa upendo na ukarimu wa kimisionari.