Papa Francisko Asikitishwa na Mauaji Nchini Australia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Vyombo vya ulinzi na usalama nchini Australia vimefanikiwa kumpiga risasi na kumuua Bwana Joel Cauchi mwenye umri wa miaka 40 kutoka Queensland kwa kusababisha mauaji ya watu sita na wengine kumi na wawili kujeruhiwa vibaya, Jumamosi tarehe 13 Aprili 2024 huko Westfield Bondi Junction, kwenye duka kubwa mjini Sydney, nchini Australia. Inasemekana kwamba, Bwana Joel Cauchi alikuwa anakabiliana na changamoto ya afya ya akili na kwamba, shambulizi hili halina uhusiano wowote na vitendo vya kigaidi.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Anthony Fisher, anaeleza kusikitishwa kwake na mauaji haya na kwamba, anapenda kuonesha uwepo wake wakaribu kwa sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anapenda kuwafariji wale wote waliowapoteza ndugu, jamaa na wapendwa wao katika shambulio hili; anawaombea marehemu wapate pumziko la milele na majeruhi waweze kupata matibabu na hatimaye kurejea tena kuendelea na shughuli zao za kila siku. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anaiombea baraka, neema na faraja nchi ya Australia.