Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 5 Aprili 2024 alitembelea Parokia ya Mtakatifu Enrico, Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 5 Aprili 2024 alitembelea Parokia ya Mtakatifu Enrico, Jimbo kuu la Roma.  (Vatican Media)

Papa Francisko Atembelea Parokia ya Mt. Enrico: Jubilei, Wafungwa na Malezi

Kati ya tema zilizozungumzwa ni pamoja na maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, hali ngumu ya wafungwa magerezani, ongezeko la kiwango cha umaskini, fursa za ajira kwa wafungwa ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wamejadili kuhusu umuhimu wa wanawake katika mchakato wa malezi na makuzi ya majandokasisi pamoja na huruma ya Mungu, shughuli za kichungaji pamoja na vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 5 Aprili 2024 alitembelea Parokia ya Mtakatifu Enrico, Jimbo kuu la Roma na kukutana pamoja na kuzungumza na Maparoko 35, pamoja na Mapadre wahudumu wa maisha ya kiroho kutoka Gereza kuu la Rebibbia. Haya ni mazungumzo yaliyodumu takribani masaa mawili. Kati ya tema zilizozungumzwa ni pamoja na maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, hali ngumu ya wafungwa magerezani, ongezeko la kiwango cha umaskini, fursa za ajira kwa wafungwa ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wamejadili kuhusu umuhimu wa wanawake katika mchakato wa malezi na makuzi ya majandokasisi pamoja na huruma ya Mungu, Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko amewataka Maparoko hawa kutumia vyema kipindi hiki cha Maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa matumaini katika maisha ya Kikristo kwani kuna Mapadre wanaoelemewa na upweke hasi kiasi cha kushindwa kuvumilia kuendelea na maisha na utume wao wa Kipadre. Hii ni mara ya pili kwa Parokia ya Mtakatifu Enrico kutembelewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa mara ya kwanza ilikuwa ni mwezi Februari mwaka 2002.

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Maparoko 35
Papa Francisko akutana na kuzungumza na Maparoko 35

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024.

Jubilei ya Mwaka 2025 kiini cha huruma na upendo wa Mungu.
Jubilei ya Mwaka 2025 kiini cha huruma na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ameendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa wafungwa magerezani. Mara nyingi Baba Mtakatifu wakati wa hija zake za kitume, amependa kutembelea, kusali na kuzungumza na wafungwa, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kumwokoa mwanadamu, ili aweze kugeuka na kuwa mtu mpya zaidi. Baba Mtakatifu anafanya yote haya kuwaonesha na kuwaonjesha wafungwa uwepo wake wa kibaba kwa njia ya sala katika shida na mahangaiko yao ya ndani, ili waweze kuwa na matumaini mapya katika maisha yao kwa siku za baadaye. Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa wafungwa magerezani anakazia hasa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wafungwa na askari magereza ni vyombo na mashuhuda wa Injili. Askari magereza wawe na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa.

Utume wa Kanisa Magerezani: Haki, Utu na Heshima ya Wafungwa
Utume wa Kanisa Magerezani: Haki, Utu na Heshima ya Wafungwa

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii. Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba, wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Maisha ya gerezani ni magumu na mara nyingine yanaweza kukatisha tamaa, kwa mfungwa kuelemewa na upweke hasi, hali ya kukata tamaa na hatimaye kushindwa kuona hatima ya maisha yake. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasiwasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anawataka askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapasa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi na utume wao.

Malezi ya Majiundo ya Majandokasisi yapewe uzito wa juu
Malezi ya Majiundo ya Majandokasisi yapewe uzito wa juu

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” unajadili kwa kina na mapana kuhusu malezi: kiakili ni kumwezesha jandokasisi kuwa mahiri katika falsafa na taalimungu ili kupambana changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika masuala ya kitamaduni kwa kutoa malezi ya kina kwa milango yote ya fahamu za binadamu! Majiundo haya yazingatie pia utamaduni na historia ya nchi husika. Malezi ya kichungaji, mambo yanayomwezesha Padre kuwajibika na kutoa huduma makini zaidi kwa familia ya Mungu kwa njia ya upendo wa shughuli za kichungaji. Kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kuamua na kutenda; kwa kuwaheshimu na kuwajali watu; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kusimamia tunu msingi za maisha ya Kikristo, daima akionesha ari na utume wa kimisionari. Sura ya sita ya Mwongozo wa Malezi ya Kipadre inabainisha mihimili mikuu ya malezi kwa kuzingatia kwamba, mlezi mkuu ni Fumbo la Utatu Mtakatifu, Askofu mahalia, Mapadre, Waseminari wenyewe, Jumuiya ya walezi yaani Majaalimu na wataalam mbali mbali wanaoalikwa ili kusaidia kutoa malezi kwa majandokasisi. Familia na Parokia pia zinahusika kikamilifu katika malezi ya majandokasisi. Watawa na waamini walei wanaweza pia kuhusishwa katika malezi ya Mapadre wa baadaye. Makundi yote haya ni muhimu sana katika malezi endelevu ya Wakleri katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Hija Parokiani
06 April 2024, 15:26