Papa Francisko Awapongeza Mapadre Wanaosherehekea Jubilei Zao: Yumo Pd. Mjigwa R.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Aprili 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba, kiasi ni fadhila adili inayoratibu mvuto wa furaha na hutoa usawa katika kutumia viumbe. Baba Mtakatifu amewapongeza mahujaji kutoka Poland, nchi ambayo inapambwa kwa kiasi kikubwa na wingi wa watakatifu. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi kubwa hii kwa ajili ya Kanisa lake, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukuza ndani mwao uhuru utakaomwezesha Roho Mtakatifu kuwasaidia kutumia vyema fadhila ya kiasi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika tamaduni na sanaa, kwa kukumbatia na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawachangamotisha waamini kuhakikisha kwamba, wanauvua utu wa kale, kwa kufanywa wapya rohoni na katika nia zao, tayari kuuvaa utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. Rej. Efe 4: 22-24. Kwa njia hii, wataweza kuona maisha mapya ambayo Kristo Mfufuka anapenda kuwashirikisha.
Huu ni mwaliko kwa waamini kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, wanaendelea kudumu katika uaminifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujitahidi kujenga na kudumisha fadhila ya kiasi, ili kuweza kudhibiti na hatimaye kutawala maneno na matendo yao, ili kuepukana na kinzani na migogoro isiyokuwa na kichwa wala miguu kwa jamii na badala yake, wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo wenye huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Mapadre kutoka Jimbo kuu la Milano na Andria, wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 na 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu anawatia shime ili waendelee kushikamana na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na katika huduma makini kwa ndugu zao. Nami nichukue fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani ilikuwa ni tarehe 17 Aprili 1999 nilipopewa Daraja Takatifu ya Upadre kwenye Kanisa la Mwili na Damu Azizi ya Yesu, Via Narni, Jimbo kuu la Roma. Ninawashukuru wazazi, ndugu, jamaa, marafiki na wajuani walionisindikiza katika kipindi chote cha miaka ishirini na mitano ya maisha na utume wangu kama Padre.
Ninawakumbuka: Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, watu wa Mungu Parokia ya Nyamiongo, Jimbo Katoliki la Musoma; Waamini wa Parokia ya Kunduchi, Mtakatifu Andrea, Bahari Beach, Bikira Maria Mama wa Huruma pamoja na Parokia ya Mtakatifu Gaspari, Mbezi Beach, enzi hizo maarufu kama Machakani, Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Ninawakumbuka pia wadau wa Radio Mwangaza FM, Dodoma kwa upendo na ushirikiano wao kwangu. Ninawakumbuka kwa moyo wa shukrani watanzania wanaoishi Italia na hasa wafanyakazi wa Radio Vatican, kwa wema, huruma na upendo wao kwangu. Lakini zaidi ninawakumbuka wale ambao sikuwataja, lakini ninathamini sana mchango wao katika maisha na utume wangu kama Padre na Mmisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wagonjwa, wazee, wanandoa wapya pamoja na vijana wa kizazi kipya, ili kwamba, wanaporejea makwao, waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji, tayari kuchangia, ili kuendelea kung’arisha mwanga wa Kristo Mfufuka. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie kwa maombezi yake, ili kweli waamini waweze kuwa ni alama ya imani na matumaini miongoni mwa jirani zao.