Papa Francisko Azindua Mwaka wa Sala Kwa Katekesi Kwa Watoto wa Komunyo ya Kwanza
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mafundisho ya kina kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni chombo mahususi cha kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina; ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo la maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo na Adili unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama mhutasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo la Maadhimisho ya Jubilei ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024.
Ni katika muktadha huu, wa katekesi makini na maadhimisho ya Mwaka wa Sala kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 11 Aprili 2024 alitembelea na hatimaye, kutoa katekesi kwa watoto mia mbili wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney “San Giovanni Maria Vianney” iliyoko Ukanda wa Borghesiana, ulioko Mashariki wa Roma. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuzindua Maadhimisho ya Mwaka wa Sala kwa watoto wanaojiandaa kupokea Ekaristi Takatifu; amejibu maswali ya watoto hawa kwa muda wa saa moja na kwamba, waamini wajenge utamaduni wa kusali nyakati zote hata wakati wa giza la maisha. Baba Mtakatifu Francisko alipowasili amepokea na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu pamoja na Paroko Marco Gandolfo wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney “San Giovanni Maria Vianney.” Huu ulikuwa ni mwanzo wa Katekesi Kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Sala. Watoto wamemuuliza Baba Mtakatifu maswali kuhusu: kifo, umuhimu wa familia na marafiki; furaha na majonzi katika maisha na umuhimu wa sala katika maisha ya mwamini: wakati wa fuaraha na wimbi kubwa la majonzi, na giza la maisha na amewajibu kwa ufupi, huku akikazia umuhimu wa kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema. Wawe wepesi kushukuru kwa kusema, “Asante”, Kuomba Msamaha kwa kusema, “Samahani pamoja na neno: “Naomba.” Amewafundisha watoto kuwa na moyo wa shukrani kwa zawadi ya imani waliyokirimiwa nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watoto wajenge utamaduni wa kumshukuru Mungu kabla ya kulala.