Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anatambua dhamana na jukumu la michezo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anatambua dhamana na jukumu la michezo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  

Siku ya Kimataifa ya Michezo Kwa Ajili ya Maendeleo na Amani 2024: Urafiki na Udugu

Baba Mtakatifu Francisko anatambua dhamana na jukumu la michezo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Michezo kwa asili inaweza kujenga jamii iliyo wazi, inayosimikwa katika mshikamano pasi na maamuzi mbele. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na wadau wa michezo, ambao hawaangalii tu ushindi na faida, bali wadau watakaojielekeza katika michezo ili kukoleza urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa Ajili ya Maendeleo na Amani: “International Day of Sport for Development and Peace; IDSDP” inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Aprili. Itakumbukwa kwamba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 23 Agosti 2013 lilipitisha Azimio la Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa ajili ya Maendeleo na Amani. Tarehe 6 Aprili ilichaguliwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kuenzi ufunguzi wa Michezo ya Olympic iliyofanyika kunako tarehe 6 Aprili 1896 huko Athens nchini Ugiriki. Lengo la maadhimisho ya michezo Kimataifa ni kutambua na kuthamini majukumu ya michezo katika maisha ya watu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza wanamichezo duniani kote, kupitia shughuli zao za michezo wawe kweli ni mashuhuda wa udugu wa kibinadamu na wajenzi wa amani. Wawe ni mfano bora wa maadili na utu wema. Kwa hakika michezo inaweza kutekeleza dhamana na majukumu yake ulimwenguni kwa kukuza na kudumisha: maridhiano na maelewano kati ya watu wa Mataifa. Michezo iwe ni kwa ajili ya michezo na kamwe isigeuzwe kuwa ni biashara. Michezo ibaki katika maana yake halisi. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa Ajili ya Maendeleo na Amani: “International Day of Sport for Development and Peace; IDSDP” kwa Mwaka 2024, Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alikumbushia kwamba, tarehe 6 Aprili Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Michezo Kwa Ajili ya Maendeleo na Amani.

Michezo kwa ajili ya maendeleo na amani duniani
Michezo kwa ajili ya maendeleo na amani duniani

Baba Mtakatifu anatambua dhamana na jukumu la michezo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Michezo kwa asili inaweza kujenga jamii iliyo wazi, inayosimikwa katika mshikamano pasi na maamuzi mbele. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na wadau wa michezo, ambao hawaangalii tu ushindi na faida, bali wadau watakaojielekeza katika michezo ili kukoleza urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, aliridhia kuchapwa kwa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba ilianza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989. Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça T.O.S.D., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba hii ya Kitume, Ibara ya 154 anaonesha umuhimu wa utamaduni na michezo katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukabidhi dhamana hii kwa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Michezo ni fursa muhimu sana inayoweza kuwaunganisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ni mahali muhimu sana pa mazoezi yanayoweza kupyaisha na kuboresha maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Michezo ni shule muhimu sana ya maisha ya kiroho na kimwili na ndiyo maana Mji wa Vatican hata katika udogo wake duniani, bado una kikosi kazi katika michezo ya aina mbalimbali duniani. Michezo inasaidia kujenga utamaduni na madaraja ya watu wa Mungu kukutana hata katika tofauti zao msingi, ili kukamilishana.

Michezo ijenge urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu
Michezo ijenge urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di sè”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema kwamba, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbalimbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika.

Michezo ni furaha, nidhamu na mshikamano
Michezo ni furaha, nidhamu na mshikamano

Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, yamemekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Michezo ni njia ya mchakato wa utakatifu na mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Lakini, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja na kuwa na upendeleo kwa maskini.

Michezo ni shule ya upendo, mshikamano na udugu
Michezo ni shule ya upendo, mshikamano na udugu

Huu ni ushauri uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika kampeni kuhusu umuhimu wa michezo, ambayo sasa imeandikiwa kitabu kijulikanacho kama “Sport una lettera alla volta” chenye kurasa 144 na kimechapishwa na Malcor D’ na kwa sasa tayari kiko kwenye maduka ya vitabu. Lengo la kitabu na ushauri kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ni kutaka kurejesha tena dhana ya michezo katika uhalisia wake! Hii inatokana na ukweli kwamba, sehemu nyingi kwa sasa michezo imekuwa ni uwanja wa “masumbwi” mahali pa kuonesha ubabe unaoongozwa na falsafa ya mwenye nguvu mpishe! Michezo imevamiwa na wimbi kubwa la ukiukwaji wa kanuni maadili na utu wema, na kugeuka kuwa kama “kichwa cha mwendawazimu” mahali pa kupandikizia mbegu za utamaduni wa kifo na ukoloni wa kiitikadi. Michezo imegeuka kuwa ni uwanja wa rushwa na ufisadi kiasi hata cha kupoteza maana ya ushindani kwani kuna baadhi ya watu wenye “vijisenti vyao” wanaopanga matokeo ili kuweka faida kibindoni! Ubadhilifu wa fedha na mali ya umma katika tasnia ya michezo ni jambo ambalo linadumaza na kufisha juhudi za kufufua na kuendeleza michezo!

Michezo Kimataifa
08 April 2024, 15:15