Tafuta

Kimsingi Injili ya Marko ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Petro, Mtume! Injili ya Marko inafikia kilele chake katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kimsingi Injili ya Marko ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Petro, Mtume! Injili ya Marko inafikia kilele chake katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.   (Vatican Media)

Sikukuu ya Mtakatifu Marko Mwinjili: Kiri ya Imani: Yesu Mwana wa Mungu

Injili ya Marko ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Petro, Mtume! Injili ya Marko inafikia kilele chake katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Utukufu wa Kristo unajionesha katika Fumbo la Ufufuko wake! Kiri ya imani ya yule akida aliyesema “Hakika mtu huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu” Mk. 15:39, kwa Mwinjili Marko, hiki kipeo cha hali ya juu kabisa cha Injili yake na kwa hakika Kristo Yesu ni “Mwana wa Mungu.” Mk 1:1.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili, anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Marko, Mwinjili, Mtoto wa Maria wa Yerusalemu, mahali ambapo Mtakatifu Petro Mtume alipata hifadhi baada ya kufunguliwa kutoka gerezani: “Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba.” Mdo 12:12. Huyu alikuwa ni binamu yake Mtakatifu Barnaba, Mtume. Katika hija ya maisha yake ya kimisionari, alifuatana sana na Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa katika safari yake ya kwanza ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Historia inaonesha kwamba, baadaye alifuatana na Mtume Paulo katika safari yake hadi Roma. Alikuwa ni mwanafunzi mpendwa sana wa Mtakatifu Petro, Mtume. Akajibidiisha kuandika mafundisho ya Mtakatifu Petro katika Injili yake. Rej. Mdo 12:25; 15:37-38. Mwinjili Marko alipendwa sana na Mtakatifu Petro kiasi cha kumwita “Marko mwanangu.” 1Pt 5:13. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 24 Aprili 2024 amesema, Mwinjili Marko amefafanua kwa kina, mapana na uthabiti wa Fumbo la Nafsi ya Yesu wa Nazareti, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanavutwa na Kristo, ili kuweza kushirikiana kwa ari na uaminifu mkubwa katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: kweli na uzima. Huu ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Kimsingi Injili ya Marko ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Petro, Mtume!

Kiri ya Imani: Hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu
Kiri ya Imani: Hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu

Injili ya Marko inafikia kilele chake katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Utukufu wa Kristo unajionesha katika Fumbo la Ufufuko wake! Kiri ya imani ya yule akida aliyesema “Hakika mtu huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu” Mk. 15:39, kwa Mwinjili Marko, hiki kipeo cha hali ya juu kabisa cha Injili yake na kwa hakika Kristo Yesu ni “Mwana wa Mungu.” Mk 1:1. Liturujia ya Neno la Mungu, Somo la kwanza kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa Watu wote Sura 5: 5-14 na Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Marko, Sura ya 16: 15-20 inayomwonesha Kristo Mfufuka akiwatokea wafuasi wake na kuwaagiza kwenda Ulimwenguni kote kuhubiri Injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Baba Mtakatifu anasema, Injili ya Marko ilikuwa ni ya kwanza kuandikwa ili kusimulia maisha na utume wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, aliyejifunua kwa Mitume wake. Kwa muda wa miaka mitatu, Kristo Yesu alitekeleza utume wake katika maisha ya hadhara. Baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, akawatokea Mitume wake na kuwapatia Amri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Injili ya Kristo ni chemchemi ya ukuaji wa imani inayopaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Baba Mtakatifu anaitaka Mihimili ya Uinjilishaji kuwa kweli ni mashuhuda wa Kanisa la Kimisionari kama utambulisho wao katika ulimwengu mamboleo. Ushuhuda wa kimisionari uiwezeshe Mihimili ya Uinjilishaji kutoka katika ubinafsi wao, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Wongofu wa ndani unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji
Wongofu wa ndani unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji

Ni katika muktadha huu, hakuna wongofu wa shuruti hata kidogo, bali watu wanavutwa kumfuasa Kristo kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko anasema Baba Mtakatifu Francisko. Wakristo wafikiri, watende na kusema kama wafuasi wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Ushuhuda wa maisha ya Kikristo hauna budi kusimikwa katika unyenyekevu, uthabiti katika imani na huduma kwa kuondokana na kiburi kwa sababu Mwenyezi Mungu huwapa wanyenyekevu neema. Wawe ni watu wa kiasi na wanaokesha daima kwani mshitaki wao Ibilisi, kama Simba angurumaye, huzungukazunguka akitafuta mtu ammeze. Imani thabiti ndiyo silaha ya kupambana na Shetani, Ibilisi. Katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, watambue kwamba, daima Kristo Mfufuka yuko pamoja nao! Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu ili awawezeshe kuwa ni mashuhuda amini wa imani wanayoitangaza na kuimwilisha katika matendo, ili watu wengi zaidi, waweze kupokea na kuambata zawadi ya ukombozi!

Mwinjili Marko
25 April 2024, 14:48