Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii: Utu, Heshima na Haki Msingi za Walemavu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo tarehe 11 Februari 1994, katika Barua binafsi “Motu proprio” ya “Vitae mysterium” yaani “Fumbo la maisha anasema, lengo la taasisi hii ni kusimama kidete kulinda na kutetea thamani ya maisha na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Taasisi hii ina dhamana ya kutafiti, ili hatimaye, kuunda utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo na kuhabarisha wadau mbalimbali changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai duniani! Taasisi hii ina dhamana na wajibu wa kufanya tafiti za kitaaluma na kisayansi, ili kusaidia kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya binadamu. Ina kazi maalum ya kusaidia kuwafunda waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika utamaduni wa maisha mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni wajibu wa taasisi katika hali ya uwazi na kwa haraka, inapaswa kuwajulisha viongozi wa Kanisa, taasisi za elimu maumbile na sayansi ya biolojia ya binadamu; taasisi za kiafya; vyombo vya mawasiliano ya jamii na jumuiya za kiraia kuhusu shughuli na tafiti zake kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii inawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, utu na heshima yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kudumisha heshima kati ya vizazi.
Taasisi ya Kipapa za Sayansi Jamii katika mkutano wake wa mwaka huu wa 2024 pamoja na mambo mengine imejadili kuhusu: uzoefu wa binadamu wenye ulemavu mambo ya kijamii yanayobainisha ulemavu huo sanjari na ujenzi wa utamaduni wa utunzaji na ushirikishwaji. Taasisi hii ya Kipapa inaitwa kushughulikia, kulingana na vigezo mbalimbali mwingiliano wa taasisi ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Huu ni mwingiliano wa teknolojia na athari zake katika tafiti mbalimbali katika maeneo kama vile dawa; Mawasiliano, Mabadiliko ya Kiikolojia pamoja na ukuzaji wa teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) pamoja na haja ya kupata mifumo mipya ya kiuchumi. Katika siku za hivi karibuni Jumuiya ya Kimataifa imepata maendeleo makubwa katika nyanja ya haki za watu wenye ulemavu. Nchi nyingi zinaonekana kufuata mwelekeo huu, lakini utambuzi huu bado ni sehemu ya hatari kubwa, kwani bado kuna vivuli katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na mshikamano. Ushuhuda wa watu wenye ulemavu unaonesha kwamba, wanaathirika: kitamaduni, kisheria, kiuchumi na kijamii, kiasi hata cha kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii. Kumbe, utu, heshima na haki msingi za mtu mwenye ulemavu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanabainisha wazi kwamba, binadamu mwenye ulemavu ni binadamu kamili, mwenye haki na wajibu. Rej. No. 148.
Kila mtu ana haki ya kupata maisha bora sanjari na kujiendeleza, ili kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu na maisha ya watu. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 11 Aprili 2024 kwa wajumbe wa Taasisi ya Kipapa za Sayansi Jamii. Mababa wa Sinodi ya Kumi na Sita ya Maaskofu wamewakumbuka walemavu wanaounda ukweli wa maisha ya mwanadamu na kwamba, wanaweza kuchangia kuigeuza jamii kuwa ya kiutu zaidi na yenye ukarimu. Kumbe, ulemavu wao ni sehemu halisi ya binadamu na kwamba, walemavu wanaosimuliwa kwenye Injili wanaweza kuwa ni sehemu ya msaada mkubwa katika kufanya tafakari katika uhalisia wa mambo ya sasa. Huu ni mwaliko kwa walemavu kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu pamoja Jamii katika ujumla wake, kama ilivyokuwa kwa Bartimayo kipofu aliyeponywa na Kristo Yesu. Rej. Mk 10: 46-52. Jambo la kusikitisha hata katika ulimwengu mambloeo kuna watu wanatengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na ulemavu wao; Ulemavu kwa baadhi ya nchi unafananishwa na majanga binafsi, Baba Mtakatifu anakaza kusema utamaduni wa kutupwa hauna mipaka na kwamba, vitendo vya namna hii vinakiuka haki msingi za binadamu wenye ulemavu kwa kutaka kukuza na kudumisha utamaduni wa faida kubwa, ufanisi na mafanikio, chanzo cha ujenzi wa utamaduni wa kifo unaosimikwa katika sera za utoaji mimba, kifo laimi pamoja na wazee kuonekana kwamba ni mzigo mzito katika jamii. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukuza na kudumisha utamaduni jumuishi pamoja na haki jamii. Hata walemavu wana haki ya kupata elimu bora sanjari na huduma bora afya, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati. Huu ni mwaliko wa kujenga jamii shirikishi ili kuwashirikisha katika maisha, ili waweze kuwa ni wadau katika maendeleo ya jamii, kama sehemu ya ushiriki wao kijamii. Huu ni mwaliko wa kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, kama kielelezo makini cha upendo pamoja na upendo wa kisiasa.