Tetemeko la Ardhi Lasababisha Maafa Makubwa Nchini Taiwan
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.4 katika kipimo cha Richter lilitokea kwenye Mwambao wa Pwani ya mashariki ya Taiwan, Jumatano tarehe 3 Aprili 2024 na hivyo kutoa tahadhari ya kutokea kwa Tsunami kisiwani hapo pamoja na nchi jirani. Watu zaidi ya 700 wamekwama nchini Taiwan wakisubiri kuokolewa na Kikosi cha Zima moto cha Taiwan. Taarifa zinasema kwamba, tayari watu 10 wamekwisha kufariki dunia, watu 1, 000 wamejeruhiwa na kwamba, majengo zaidi ya 100 yameharibiwa vibaya kutokana na tetemeko hilo. Hili ni tetemeko ambalo alijawahi kutokea nchini Taiwan kwa takribani miaka 25 iliyopita.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amemtumia salam za rambirambi Askofu John Baptist Lee Keh-Mean, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Taiwan, ili kuonesha mshikamano wake wa dhati na watu waliokumbwa na mkasa huu. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kiroho na kimwili kwa wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya makubwa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki katika maafa haya maisha ya uzima wa milele. Anawaombea wale waliojeruhiwa kupona haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku. Anawaombea watu wa kujitolea kwa msaada mkubwa na faraja waliyoitoa kwa ajili ya watu walioathirika na tetemeko la ardhi. Mwishoni, Baba Mtakatifu ametoa baraka na faraja kwa watu wa Mungu nchini Taiwan.