Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 11 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 11 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia   (Vatican Media)

Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia: Ugonjwa na Mateso Katika Biblia

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 11 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia Mwaka huu, inapembua tema kuhusu “Ugonjwa na Mateso Katika Biblia.” Huu ni utafiti unaomhusu kila binadamu kwani anakabiliwa na magonjwa, udhaifu na kifo. Hii ni kutokana na asili ya binadamu kujeruhiwa na hivyo kuwepo na mgongano kati ya uovu na maumivu. Umuhimu wa huruma na upendo kwa wagonjwa kama alivyofanya Yesu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia liliundwa na Papa Leo XIII kwa Waraka wake wa Kitume ujulikanao kama “Vigilantiae studiique” wa tarehe 30 Oktoba 1902. Baba Mtakatifu akaipatia Tume hii mpya kazi kuu tatu: Kukuza Masomo ya Biblia miongoni mwa waamini wa Kanisa Katoliki. Kupambana na maoni potovu kuhusu Maandiko Matakatifu kwa njia ya Kisayansi. Kusoma na kupembua maswali yanayojadiliwa, matatizo na changamoto zinazojitokeza katika uwanja wa Biblia. Miaka kadhaa baadaye, Papa Pio wa X, kwa Barua yake ya Kitume “Scripturae Sanctae” ya tarehe 23 Februari 1904, aliipatia Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia Kitivo cha kutoa shahada za kitaaluma za: Uzamili na Uzamivu katika Masomo ya Biblia. Papa Leo XIII na Pio X walikuwa wametoa kwa Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia uwezo wa kutosha kuhusiana na maswali ya kibiblia yaliyokuwa yakijitokeza na mabishano yaliyochochewa na uchunguzi wa kisasa wa uchanganuzi.  Mnamo tarehe 27 Juni 1971, katika muktadha wa kazi kubwa ya mageuzi baada ya maridhiano, Mtakatifu Paul VI, kwa barua yake binafsi “Motu proprio Sedula” alianzisha kanuni mpya za ushirika na utendaji kazi. Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia ili kufanya shughuli zake ziweze kuzaa matunda zaidi kwa Kanisa na kuendana vyema na hali ya sasa. Waraka huu wa kitume unaashiria mabadiliko makubwa kwa nafasi na mpangilio wa Tume.

Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia Iliundwa 30 Oktoba 1902
Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia Iliundwa 30 Oktoba 1902

Katika vifungu kumi na tano muundo mpya ukafafanuliwa: Wanachama si Makardinali tena, ambao wanasaidiwa na washauri, lakini walimu wa sayansi ya Biblia kutoka shule na Mataifa mbalimbali, ambao wanajulikana “kwa elimu yao, busara na heshima ya Kikatoliki kwa Mamlaka Fundishi ya Kanisa: “Magisterium.” Huu ukawa ni muundo uliopaswa kufuatwa. Makardinali wakaondolewa na kwamba, Tume hii ikawa ni chombo cha mashauriano, kinachowekwa kwenye huduma ya Mamlaka fundishi ya Kanisa kwa kuwekwa nchini Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Mwenyekiti wake ndiye aliyechukua nafasi hii. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 11 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia “The Pontifical Biblical Commission.” Mwaka huu Tume inapembua tema kuhusu “Ugonjwa na Mateso Katika Biblia.” Huu ni utafiti unaomhusu kila binadamu kwani anakabiliwa na magonjwa, udhaifu na kifo. Hii ni kutokana na asili ya binadamu kujeruhiwa na hivyo kuwepo na mgongano kati ya uovu na maumivu. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa kuwaonesha wagonjwa huruma kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake, kiasi cha kuinama na kuwagusa wagonjwa katika undani wa mahangaiko yao na hatimaye, kuwajumuisha.

Tume ya Kipapa ya Taaluma inasaidia kufafanua Maandiko Matakatifu
Tume ya Kipapa ya Taaluma inasaidia kufafanua Maandiko Matakatifu

Hii ni changamoto kwa wataalamu wa Maandiko Matakatifu kutekeleza dhamana, wajibu na huduma hii kwa ari na moyo wa udugu wa kibinadamu. Ugonjwa na mateso katika Biblia ni tema inayopaswa kushughulikiwa kikamilifu ili kuondokana na miiko inayoweza kuwatumbukiza watu katika upweke hasi, hali ya kutengwa na hatimaye kukata tamaa. Kuna shuhuda za waamini ambao kutokana na imani yao thabiti wameweza kuwashirikisha jirani zao mambo msingi katika maisha, kwa kuiga mfano wa Kristo Yesu anayeonesha njia na kuwataka waja wake, kuwasaidia wagonjwa, ili kuweza kupambana kikamilifu na changamoto ya ugonjwa. Huu ni mwaliko pia kwa wagonjwa kuhakikisha kwamba, wanaunganisha mahangaiko yao pamoja na mateso ya Kristo Yesu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alikuwa na huruma sana kwa sababu walikuwa kama Kondoo wasiokuwa na mchungaji. Aliwaonea huruma watu zaidi ya elfu, akawalisha kwa mikate saba na samaki wawili. Aliwahudumia wagonjwa bila kuchoka; akasimama na kusikiliza kilio chao kama ilivyotokea kwa wale vipofu wawili wa Yeriko. Kwa hakika kulikuwa na umati mkubwa sana wa wagonjwa walioomba huruma yake, kama ilivyotokea kwa wakoma kumi na kama alivyomfufua kijana wa Naini, Mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane. Huruma hii ilimwezesha Kristo Yesu kuwa karibu na wagonjwa hata kiasi cha kujitambulisha nao akisema, “nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama.” Kristo Yesu aliguswa na ugonjwa na mateso ya watu wengi, kiasi cha kuwashughulikia kikamilifu, ili kuwaokoa na kuwashirikisha upendo wake usiokuwa na kikomo; upendo uliomfanya hata akatundikwa Msalabani na hivyo kutoa maana mpya ya mateso katika maisha ya mwanadamu.

Mwenyekiti Mafundisho Tanzu ndiye mkuu wa Taasisi hii ya Kipapa
Mwenyekiti Mafundisho Tanzu ndiye mkuu wa Taasisi hii ya Kipapa

Kristo Yesu alikabiliana na mateso yake katika hali ya unyenyekevu, utulivu na upole. Kristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyetwaa mwili, akaonesha ukaribu na wokovu kwa vitendo. Aligusa mateso na mahangaiko ya binadamu kwa vitendo na hivyo kusahihisha uelewa wa mateso katika Maandiko Matakatifu, siyo kama walivyokuwa wanadhani rafiki zake Ayubu katika Agano la Kale. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwahusisha na kuwajumuisha wengi; akajitaabisha kuwatafuta wadhambi na wale waliokuwa wametengwa na jamii kwa mfano wa kondoo aliyepotea, mfano wa shilingi iliyoonekana tena na hatimaye ni mfano wa Baba mwenye huruma dhidi ya Mwana mpotevu; pamoja na mkoma aliyetakaswa. Ilikuwa ni hamu ya moyo wa Kristo Yesu kuganga na kumtibu mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kuwaondolea dhambi zao. Baada ya Kristo Yesu kuwajumuisha wale waliokuwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, aliwashirikisha pia utume wake kama alivyofanya kwa Mitume wake akiwaagiza kuwaponya wagonjwa huku wakiwakumbusha kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia. Kutokana na uzoefu na mang’amuzi ya ugonjwa na mateso katika maisha ya mwanadamu, Mama Kanisa anahimizwa kuhakikisha kwamba, anatembea na watu wote, kwa kuwashirikisha mshikamano wa Kikristo na kiutu, kwa kujikita katika majadiliano na hivyo kupandikiza mbegu ya majadiliano na matumaini. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kwa kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Taaluma ya Biblia kwa huduma nzuri wanayo itekeleza na kwamba, waitende kazi hii kwa ari na moyo wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwaangazia waamini na watu wote wenye mapenzi mema mwanga wa Neno la Mungu unaokuza na kuimarisha imani na hivyo kuongeza ari na mwelekeo kwa Mungu na jirani zao kwa njia ya Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma ya kichungaji, daima Mama Kanisa akiendelea kuchota kutoka katika kisima cha Neno la Mungu.

Ugonjwa na mateso
11 April 2024, 15:41