Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 61 ya Kuombea Miito: Matumaini na Amani

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu watu walioko safarini mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa: Lengo ni kuishi kwa haki, amani na upendo.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar Es Salaaam

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu watu walioko safarini mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Sala kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 anasema sala ndiyo nguvu na ufunguo wa malango ya matumaini. Waamini ni mahujaji wa matumaini na wajenzi wa amani na kwamba, lengo kuu la safari ya maisha ni kuishi kwa haki, amani na upendo na kwamba, lengo na wito ni kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; umoja, amani na udugu. Kila mwamini ajitahidi kugundua wito wake sahihi katika Kanisa na Ulimwengu, kwa kuwa hujaji wa matumaini na wajenzi wa amani. Ndugu wapendwa! Kila mwaka, Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni inatualika kutafakari juu ya zawadi adhimu ya wito wa Bwana kwa kila mmoja wetu, kama sehemu ya mahujaji wake waaminifu, kushiriki katika mpango wake wa upendo na kumwilisha uzuri wa Injili katika hali mbalimbali za maisha. Kusikia mwito huo wa kimungu, ambao sio wajibu wa kulazimishwa - hata kwa jina la maadili ya kidini - ndiyo njia ya uhakika kwetu kutimiza tamaa yetu ya ndani zaidi ya furaha. Maisha yetu hupata utimilifu tunapogundua sisi ni akina nani, karama zetu ni nini, ni wapi tunaweza kuzifanya zizae matunda, na ni njia gani tunaweza kufuata ili kuwa ishara na vyombo vya upendo, kukubalika kwa ukarimu, uzuri na amani, popote pale tunapokuwa.

Majandokasisi wakishiriki Ibada ya Misa Takatifu
Majandokasisi wakishiriki Ibada ya Misa Takatifu

Hivyo, siku hii, daima ni wakati mzuri wa kukumbuka kwa shukrani kwa Bwana juhudi aminifu, za kudumu na mara nyingi zilizofichika za wale wote ambao wameitikia wito unaokumbatia maisha yao yote. Ninawafikiria akina mama na akina baba ambao hawajifikirii kwanza wao wenyewe au kufuata mitindo ya muda mfupi, lakini hutengeneza maisha yao kupitia mahusiano yaliyo na upendo na neema, uwazi kwa zawadi ya maisha na wajibu kwa watoto wao na ukuaji wao katika ukomavu. Ninawafikiria wale wote wanaofanya kazi zao kwa moyo wa ushirikiano na wengine, na wale wanaojitahidi kwa njia mbalimbali kujenga ulimwengu wa haki zaidi, uchumi thabiti zaidi, sera ya kijamii yenye usawa na jamii yenye utu zaidi. Kwa neno moja, juu ya wale wanaume na wanawake wote wenye mapenzi mema wanaojitolea maisha yao kufanya kazi kwa manufaa ya wote. Ninawafikiria pia wale wanaume na wanawake wote waliowekwa wakfu wanaotoa maisha yao kwa Bwana katika ukimya wa sala na katika shughuli za kitume, wakati mwingine pembezoni mwa jamii, bila kuchoka na kwa ubunifu wakitumia karama yao kwa kuwahudumia wale wanaowazunguka. Ninawafikiria pia wale wote waliokubali wito wa Mungu kwa ukuhani wa daraja, wakijitoa wenyewe katika kuhubiri Injili, wakifungua maisha yao wenyewe, pamoja na mkate wa Ekaristi, kwa ajili ya ndugu zao, wakipanda mbegu za matumaini na kudhihirisha kwa wote uzuri wa ufalme wa Mungu. Kwa vijana, na hasa wale wanaohisi kuwa mbali au kutokuwa na uhakika kuhusu Kanisa, nataka kusema hivi: Hebu Yesu awavute kwake; mleteeni maswali yenu muhimu kwa kusoma Injili; mwache awape changamoto kwa uwepo wake, ambao daima huchochea ndani yetu mgogoro wenye manufaa. Yesu anaheshimu uhuru wetu kuliko mtu mwingine yeyote. Yeye halazimishi, bali anapendekeza. Mpeni nafasi na mtapata njia ya kuelekea furaha kwa kumfuata. Na, ikiwa atawaomba hilo, kwa kujitoa kabisa kwake.

Watu wa Mungu wakishuhudia Ibada ya Upadrisho
Watu wa Mungu wakishuhudia Ibada ya Upadrisho

Watu walio katika mwendo: Muunganiko mzuri wa karama na miito mbalimbali ambayo jumuiya ya Kikristo inatambua na kuandamana nayo hutusaidia kuthamini kikamilifu zaidi maana ya kuwa Wakristo. Kama watu wa Mungu katika ulimwengu huu, tukiongozwa na Roho wake Mtakatifu, na kama mawe yaliyo hai katika Mwili wa Kristo, hatimaye tunatambua kwamba sisi ni washiriki wa familia kubwa, watoto wa Baba na kaka na dada kila mmoja kwa mwenzake. Sisi sio visiwa vilivyojifunga vyenyewe bali ni sehemu ya jumla kubwa zaidi. Kwa maana hii, Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni ina tabia ya kisinodi: katikati ya aina mbalimbali za karama zetu, tunaitwa kusikilizana sisi kwa sisi na kusafiri pamoja ili kuzitambua na kutambua mahali ambapo Roho anatuongoza kwa manufaa ya wote. Katika wakati huu, basi, safari yetu ya pamoja inatufikisha kwenye Mwaka wa Jubilei ya 2025. Tusafiri kama mahujaji wa matumaini kuelekea Mwaka Mtakatifu, kwani katika kugundua wito wetu wenyewe na nafasi yake kati ya karama mbalimbali zinazotolewa na Roho, tunaweza kuwa wajumbe na mashahidi kwa ulimwengu wetu wa ndoto ya Yesu ya familia moja ya kibinadamu, tukiunganishwa katika upendo wa Mungu na katika kifungo cha upendo, ushirikiano na udugu. Siku hii imetengwa mahususi kwa ajili ya kumwomba Baba zawadi ya miito mitakatifu kwa ajili ya kujenga Ufalme wake: “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake” (Lk 10:2). Sala - kama sisi sote tujuavyo - inahusu zaidi kumsikiliza Mungu kuliko kuzungumza naye. Bwana anazungumza na mioyo yetu, na anataka kuikuta ikiwa wazi, minyofu na yenye ukarimu. Neno lake lilifanyika mwili katika Yesu Kristo, ambaye anatufunulia mapenzi yote ya Baba. Katika mwaka huu wa sasa, uliotengwa kwa ajili ya sala na maandalizi ya Jubilei, sisi sote tunaitwa kugundua tena baraka isiyokadirika ya uwezo wetu wa kuingia katika mazungumzo ya dhati na Bwana na hivyo kuwa mahujaji wa matumaini. Kwa maana “sala ndiyo nguvu ya kwanza ya matumaini. Unaomba na matumaini yanakua, yanasonga mbele. Ningeweza kusema kwamba sala hufungua mlango wa matumaini. Matumaini yapo, lakini kwa sala yangu nafungua mlango” (Katekesi, 20 Mei 2020).

Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani
Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani

Mahujaji wa matumaini na wajenzi wa amani: Hata hivyo inamaanisha nini kuwa mahujaji? Wale wanaokwenda kuhiji wanatafuta zaidi ya yote kukaza macho yao kwenye lengo, kuliweka daima katika akili na mioyo yao. Ili kufikia lengo hilo, hata hivyo, wanahitaji kuzingatia kila hatua, ambayo ina maana ya kusafiri wakiwa na mizigo michache, kuondokana na kile kinachowaelemea, kubeba tu yaliyo ya muhimu na kujitahidi kila siku kuweka kando uchovu wote, hofu, kutokuwa na uhakika na kusita. Kuwa hujaji kunamaanisha kuondoka kila siku, daima kuanza upya, kugundua tena shauku na nguvu zinazohitajika ili kufuatilia hatua mbalimbali za safari ambayo, ingawa inachosha na ngumu, daima hufungua mbele ya macho yetu upeo mpya na mandhari zisizojulikana hapo awali. Hii ndiyo maana kuu ya hija yetu ya Kikristo: tunaanza safari ili kugundua upendo wa Mungu na wakati huo huo kujigundua wenyewe, shukrani kwa safari ya ndani inayostawishwa na mahusiano yetu na wengine. Hija yetu hapa duniani ni zaidi ya safari isiyo na ukomo au kuzurura kusiko na lengo; kinyume chake, kila siku, kwa kuitikia wito wa Mungu, tunajaribu kupiga kila hatua inayohitajika ili kuuendea ulimwengu mpya ambapo watu wanaweza kuishi kwa amani, haki na upendo. Sisi ni mahujaji wa matumaini kwa sababu tunasonga mbele kuelekea mustakabali bora zaidi, tukidhamiria katika kila hatua kuufanya uweze kufika. Hili ndilo, hatimaye, lengo la kila wito: kuwa wanaume na wanawake wa matumaini. Kama watu binafsi na kama jumuiya, katikati ya karama na huduma mbalimbali, sisi sote tunaitwa kumwilisha na kuwasilisha ujumbe wa Injili ya matumaini katika ulimwengu ulio na changamoto nyingi. Hizi ni pamoja na mzuka mbaya wa vita vya tatu vya dunia vilivyopiganwa vipande vipande; mafuriko ya wahamiaji wanaokimbia nchi zao kutafuta maisha bora ya baadaye; idadi inayoongezeka ya maskini; tishio la kuhatarisha kabisa afya ya sayari yetu. Bila kusema chochote kuhusu matatizo yote tunayokumbana nayo kila siku, ambayo nyakati fulani huhatarisha kutuingiza katika kujiuzulu au kushindwa.

Watawa wakiandamana kwenda kwenye Ibada ya kuweka nadhiri
Watawa wakiandamana kwenda kwenye Ibada ya kuweka nadhiri

Katika nyakati zetu, basi, ni jambo la muhimu kwamba sisi Wakristo tusitawishe muono uliojaa matumaini na kufanya kazi kwa ukamilifu katika kuitikia wito tuliopokea, katika huduma kwa ufalme wa Mungu wa upendo, haki na amani. Tumaini hili - Mtakatifu Paulo anatuambia - "halitahayarishi" (Warumi 5:5), kwa kuwa limezaliwa kutoka katika ahadi ya Bwana kwamba atakaa pamoja nasi daima na kutujumuisha katika kazi ya ukombozi ambayo anataka kuikamilisha katika moyo wa kila mtu binafsi na katika “moyo” wa viumbe vyote. Tumaini hilo linapatikana katika ufufuko wa Kristo, ambao “una nguvu kuu ambayo imeenea katika ulimwengu huu. Mahali ambapo vyote vinaonekana kuwa vimekufa, ishara za ufufuko hutokea ghafula. Ni nguvu isiyozuilika. Mara nyingi inaonekana kwamba Mungu hayupo: kote kote, tunaona udhalimu unaoendelea, uovu, kutojali na ukatili. Lakini pia ni kweli kwamba katikati ya giza kitu kipya kila mara huchipuka na kutoa matunda mapema au baadaye” (Evangelii gaudium, 276). Tena, Mtume Paulo anatuambia kwamba, “kwa tumaini tuliokolewa” (Warumi 8:24). Ukombozi unaotimizwa katika Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya matumaini, tumaini la uhakika na la kutegemewa, kwa sababu hiyo tunaweza kukabiliana na changamoto za sasa. Kuwa mahujaji wa matumaini na wasatawishaji wa amani, basi, ina maana ya kuweka maisha yetu juu ya mwamba wa ufufuko wa Kristo, tukijua kwamba kila jitihada inayofanywa katika wito ambao tumeukubali na kutafuta kuuishi, hazitakuwa bure kamwe. Kushindwa na vikwazo vinaweza kutokea njiani, lakini mbegu za wema tunazopanda zinakua kwa utulivu na hakuna kitu kinachoweza kututenganisha na lengo la mwisho: kukutana kwetu na Kristo na furaha ya kuishi milele katika upendo wa kindugu. Wito huu wa mwisho ndio ambao lazima tuutazamie kila siku: hata sasa uhusiano wetu wa upendo na Mungu na kaka na dada zetu unaanza kutimiza ndoto ya Mungu ya umoja, amani na udugu. Mtu yeyote asijisikie kutengwa kwenye wito huu! Kila mmoja wetu kwa njia yake ndogo, katika hali yetu mahususi ya maisha, anaweza, kwa msaada wa Roho Mtakatifu, kuwa mpanzi wa mbegu za matumaini na amani.

Jandokasisi akipewa Daraja Takatifu ya Ushemasi
Jandokasisi akipewa Daraja Takatifu ya Ushemasi

Ujasiri wa kujituma: Kwa mtazamo huu, ningesema tena, kama nilivyosema katika Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Lisbon: “Simama!” Tuamke usingizini, tuache nyuma kutojali, tufungue milango ya gereza ambamo mara nyingi tunajifungia, ili kila mmoja wetu aweze kugundua wito wake sahihi katika Kanisa na ulimwenguni, na kuwa hujaji wa matumaini na mjenzi wa amani! Hebu tuwe na shauku kuhusu maisha, na tujitoe kuwajali kwa upendo wale wanaotuzunguka, katika kila sehemu tunamoishi. Ngoja niseme tena: "Uwe na ujasiri wa kujituma!" Padre Oreste Benzi, mtume asiyechoka wa ukarimu, aliyekuwa daima upande wa maskini na wasio na ulinzi, alizoea kusema kwamba hakuna mtu aliye maskini kiasi cha kukosa cha kutoa, na hakuna aliye tajiri kiasi cha kutohitaji kitu cha kupokea. Basi, tuinuke na tuanze safari kama mahujaji wa matumaini, ili kama vile Bikira Maria alivyokuwa kwa Elizabeti, sisi pia tuweze kuwa wajumbe wa furaha, vyanzo vya maisha mapya na mafundi wa udugu na amani.

Umetolewa Roma, Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane Laterano, 21 Aprili 2024,

Dominika ya Nne ya Pasaka.

PAPA FRANCISKO

[Umetafrisiwa na Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (PMS) – Aprili, 2024]

Siku ya Miito 2024
18 April 2024, 16:04