Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Sikukuu ya Eid El Fitr 1445 H./2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, majadiliano ya kidini yataweza kuzaa matunda mengi ya ushirikiano na mshikamano sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Hija ya pamoja katika majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya waamini wa dini mbalimbali ili kuweza: Kufahamiana, kuheshimiana na kwa pamoja, kuweza kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Huu ni mchakato wa ujenzi wa fadhila ya upendo wa kidugu kati ya watu kwani Mungu ni asili na hitimisho la upendo. Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano na waamini wa dini mbalimbali duniani, “Nostra aetate” ni msingi wa mahusiano mema ambayo yameendelea kujengeka na kuimarika kama ndugu wamoja kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Urithi mkubwa ambao waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuufanya katika maisha na utume wao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya upendo kwa Mungu na jirani. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani sanjari na Sikukuu ya 'Eid El Fitr 1445 H./2024 A.D.”, Baba Mtakatifu Francisko ameuandikia Mtandao wa Alarabiya, Ujumbe na Matashi Mema baada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sikukuu ya Eid El Fitr 1445 H./2024 A.D. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni amani na anatamani kuona amani ikitawala. Watu wana kiu ya amani ya kudumu itakayowawezesha kurejea tena makwao na watoto kuendelea na masomo. Ni muda muafaka wa kuhakikisha kwamba uhuru wa kuabudu unadumishwa na wote.
Itakumbukwa kwamba, Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka 2024 umekwenda sanjari na Mfungo wa Kwaresima na hatimaye, Sherehe ya Pasaka. Sikukuu ya Eid El Fitr 1445 H./2024 na Pasaka ni muhimu sana kwa waamini wa dini hizi mbili wanao mwabudu “Mungu mwenye huruma na nguvu”, lakini kwa masikitiko makubwa ya umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa dini hizi mbili kuondokana na matendo ya giza, chuki na uhasama na hivyo kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu, ili kukuza na kudumisha amani. Mwenyezi Mungu ni amani na anatamani kuona amani ikishamiri katika akili na nyoyo za watu, ili kuondokana na uadui usiokuwa na mvuto wala mashiko na kwamba, vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu na hivyo kufutilia mbali matumaini yote. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, anateseka sana kutokana na vita kati ya Israeli na Palestina na anawasihi kusitisha vita hii mara kwani inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Misaada ya kiutu iruhusiwe kupelekwa kwenye Ukanda wa Gaza ili kunusuru maisha ya Wapalestina wanaoteseka. Wafungwa na mateka wa vita wanaoshikiliwa tangu mwezi Oktoba 2023 waachiliwe mara moja. Baba Mtakatifu anakaza kusema, machafuko ya kisiasa pamoja na vita inayoendelea nchini Siria, Lebanon pamoja na Ukanda mzima Mashariki ya Kati ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani. Umefika wakati wa kusitisha vita na kwamba, huu ni ujumbe kwa wale wenye madaraka kwenye Jumuiya ya Kimataifa.
Ni muda wa kusimamisha vita na kuanza kuwafikiria watoto wanaoteseka kutokana na vita kiasi cha kufifisha matumaini ya watoto hawa. Jumuiya ya Kimataifa ijielekeze kuutafuta amani kwa jicho la watoto, ili kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii. Watoto hawa wanahitaji makazi yao, viwanja vya michezo pamoja na shule ili kuendelea kujipatia elimu na wala hawahitaji makaburi wala makuburi ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hata Jangwani kunaweza kuchanua maua. Lakini kwa bahati mbaya, kumekuwepo na jangwa la chuki na uhasama, lakini matumaini yanaweza kuzaliwa upya, kwa kuishi na kukua kwa pamoja; kwa kuheshimu na kuthamini imani ya watu wengine; kwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu na kwamba, watu wanaweza kujenga na kudumisha haki na amani bila kuwashutumu watu wengine. Baba Mtakatifu anasema, haya ndiyo matumaini ya Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati, hata katika magumu na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo. Daima amewasihi kuwa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia imani yao, wakijizatiti katika ujenzi wa amani na udugu wa kibinadamu.