Tafuta

Kardinali Parolin amewakumbusha Askari wapya kwamba, muda wao wa huduma mjini Vatican ni kipindi cha kutolea ushuhuda wa furaha ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kardinali Parolin amewakumbusha Askari wapya kwamba, muda wao wa huduma mjini Vatican ni kipindi cha kutolea ushuhuda wa furaha ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.   (Vatican Media)

Askari Boresheni Maisha Yenu Kwa: Neno, Sakramenti na Ibada Kwa Bikira Maria na Watakatifu

Askari hawa wanaitwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ukarimu na uungwana; sanjari na moyo wa upendo kwa watu wote. Kati yao, wajenge na kudumisha mahusiano ya udugu wa kibinadamu kwa kujenga maisha ya kijumuiya; ili kushirikishana nyakati za furaha na majonzi; wakisaidiana na kufarijiana, ili kujenga urafiki wa kijamii. Askari waboreshe maisha yao kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa na Ibada kwa Bikira Maria pamoja na Watakatifu somo wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss Guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu kwa kuongozwa na kauli mbiu “Acriter et fideliter” yaani “Ujasiri na Uaminifu” na kilianzishwa na Papa Giulio wa Pili tarehe 22 Januari 1506. Jumatatu tarehe 6 Mei 2024 Wanajeshi 34 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswisi, wanafanya kumbukumbu ya Askari 189 kutoka Uswisi waliofariki dunia kunako mwaka 1527 wakati wa kumlinda Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa ni Papa Clement VII dhidi ya Mfalme Charles V wa Ufaransa. Ni Askari 42 tu ndio waliofanikiwa kuokolewa. Tangu wakati huo, hawa wamekuwa ni walinzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni Askari wakakamavu, nadhifu, wapole na waungwana wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji mkubwa kwa ajili ya Papa, waamini na mahujaji wanaofika mjini Vatican kwa shughuli mbalimbali! Walinzi hawa kila mwaka hula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro mbele ya Mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa Jumatatu tarehe 6 Mei 2024 ni Askofu mkuu Edgar Robinson Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican. Sherehe hizi zimeanza kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amewakumbusha Askari wapya kwamba, muda wao wa huduma mjini Vatican ni kipindi cha kutolea ushuhuda wa furaha ya imani yao kwa Kristo Yesu inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo kwa wale wote wanaofanya hija ya maisha ya kiroho ili kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Maaskari wapya wakielekea Kanisani ili kusali
Maaskari wapya wakielekea Kanisani ili kusali

Ni katika ushuhuda huu, Askari hawa wanaitwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ukarimu na uungwana; sanjari na moyo wa upendo kwa watu wote. Kati yao, wajenge na kudumisha mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu kwa kujenga maisha ya kijumuiya; ili kushirikishana nyakati za furaha na majonzi; wakisaidiana na kufarijiana, ili kujenga urafiki wa kijamii. Kardinali Parolin, amewataka Askari wapya kuboresha maisha yao kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kwamba, wajitahidi kujenga na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anamwangalia Bikira Maria aliyejitahidi kumwilisha “Heri za Mlimani” muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake! Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake mwanana, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala, lakini zaidi kwa njia ya tafakari ya Rozari Takatifu. Baba Mtakatifu anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sala ya Rozari ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Katika maisha na utume wao, wasikose kuwakimbilia watakatifu somo wao; walinzi na waombezi wao. Hawa ni akina Mtakatifu Martino, Mtakatifu Sebastiano na Mtakatifu Nicola wa Flùe: “Defensor pacis et pater patriae” yaani “Mlinzi wa amani na Baba wa Taifa” ili kutoka juu mbinguni aweze kuwaombea.

Maaskari waboreshe maisha yao ya kiroho: Sala, Sakramenti na Ibada
Maaskari waboreshe maisha yao ya kiroho: Sala, Sakramenti na Ibada

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza kwa moyo wao wa ukarimu na sadaka kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Kanisa. Kila siku, anaonja majitoleo yao, weledi na upendo unaobubujika kutoka katika shughuli zao! Baba Mtakatifu anawapongeza wana familia wa wanajeshi hawa ambao wameridhia uamuzi wao wa kujisadaka kwa ajili ya Vatican na kuendelea kuwasindikiza kwa upendo na sala zao pamoja na kuwapatia elimu, malezi makini pamoja na mazingira muafaka yanayowawezesha kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Baba Mtakatifu aliwakumbusha kwamba, mwaka huu, wanajeshi hawa wanakula kiapo cha utii wakati ambapo Mama Kanisa anaendelea kushangilia Fumbo la Pasaka, changamoto na mwaliko hata kwa wao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Mfufuka, kwa kutangaza furaha ya Pasaka; kwa kueneza utamaduni wa Ufufuko wa wafu dhidi ya utamaduni wa kifo, unao onekana kutaka kuwameza watu wengi.

Askari wakila kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro
Askari wakila kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia sifa njema ya Askari hawa: mahusiano na mafungamano ya familia kubwa; ujenzi wa kambi mpya kwa ajili ya maisha ya kifamilia; umuhimu wa maisha ya kijumuiya. Baba Mtakatifu anasema, kambi ya Jeshi iwe ni mahali pa kujifunza kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha majadiliano, ukweli wa maisha, mahusiano mema pamoja na maelewano. Katika hali na mazingira kama haya, kutakuwepo na nyakati za furaha pamoja na nyakati za majonzi. Kipindi hiki, kiwe ni fursa ya kujenga urafiki mwema, kwa kuheshimu na kuthamini mawazo yanayotolewa na wengine; kwa kuendelea kujifunza kuona kwa mwingine yule ndugu na jirani ambaye ni mwadani wa safari ya pamoja. Tabia hii itawawezesha kuishi katika Jamii wakiwa na mwelekeo sahihi wa maisha, kwa kutambua tofauti za kitamaduni, kidini na kijamii kama amana na utajiri na wala si tishio la maisha. Hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo kutokana na uwepo wa makundi makubwa ya watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Kwa hakika wanaonesha utashi wa huduma, hali inayowataka kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano mema kati yao, wajitahidi kufanya mapumziko na kutembea kwa pamoja pale inapowezekana.

Ukarabati wa Kambi ya Wanajeshi ili waweze kuishi na familia zao.
Ukarabati wa Kambi ya Wanajeshi ili waweze kuishi na familia zao.

Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi hawa wajenge na kudumisha mahusiano na mafungamano mema kati yao kwani mwelekeo huu ni muhimu sana katika maisha ya Kanisa. Kristo Yesu ni shuhuda ya kwamba Mungu ni upendo na kwamba, mahusiano mema ni njia inayowaelekeza katika ukomavu wa kiutu na Kikristo, urithi na amana kutoka kwa wazazi wao, ndugu na jamaa, wanandani shuleni, marafiki na wafanyakazi wenzao. Wanajeshi hawa wanaishi kama ndugu wamoja kwa kipindi cha walau miaka miwili; ni muda wa kazi, maisha na ujenzi wa mahusiano na mafungamano sanjari na ushirika katika umoja na tofauti zake msingi na kwamba, kambi ya jeshi ni muhimu sana. Baba Mtakatifu amewaambia wanajeshi hawa kwamba, kuna ujenzi wa kambi mpya ya wanajeshi itakayowezesha kuishi pamoja na familia zao, kwani kwa sasa wanalazimika kuishi peke yao bila familia zao: Kumbe, kukamilika kwa ujenzi wa kambi mpya kutasaidia kujenga na kuimarisha mahusiano ya kifamilia kambini hapo. Baba Mtakatifu amewasihi wanajeshi hawa kujitahidi kujenga maisha ya kijumuiya, iwe ni fursa ya kuufahamu mji wa Roma, wajitahidi kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu, kucheza pamoja na kuendelea kushirikishana tunu msingi za maisha, zitakazowaambata katika hija ya maisha yao yote. Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka katika maadhimisho ya Sikukuu hii, kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na watakatifu walinzi na waombezi wao.

Parolin Mahubiri Ok
07 May 2024, 14:43