Jumamosi tarehe 18 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kichungaji Jimbo la Verona, nchini Italia. Jumamosi tarehe 18 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kichungaji Jimbo la Verona, nchini Italia.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Jimbo Katoliki la Verona: Haki na Amani Zitabusiana!

Mkesha wa Sherehe ya Pentekoste, tarehe 18 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kichungaji Jimbo la Verona, nchini Italia. Wema na uaminifu zitakutana; haki na amani zitabusiana. Uaminifu utachipuka katika nchi; na haki itachungulia kutoka mbinguni. Naye Bwana atatoa yaliyo mema; na nchi yetu itatoa mazao. Haki itatangulia mbele ya Bwana, wokovu utafuata nyayo zake. Hija hii ya kichungaji inanogeshwa na kauli mbiu “haki na amani zitabusiana.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu; kutoka katika utimilifu wake Kristo Yesu, Bwana anammimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kwa ukamilifu. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya wale wanaomwamini na kumsadiki, katika hali ya unyenyekevu na imani wanashiriki ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni paji la Mungu na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wanaweza kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo: ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Rej. KKK 731-747.Ni katika muktadha wa mkesha wa Sherehe ya Pentekoste, Jumamosi tarehe 18 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kichungaji Jimbo la Verona, nchini Italia. Wema na uaminifu zitakutana; haki na amani zitabusiana. Uaminifu utachipuka katika nchi; na haki itachungulia kutoka mbinguni. Naye Bwana atatoa yaliyo mema; na nchi yetu itatoa mazao. Haki itatangulia mbele ya Bwana, wokovu utafuata nyayo zake. Hija hii ya kichungaji inanogeshwa na kauli mbiu “haki na amani zitabusiana.” Zab 85:10. Akiwa jimboni humo, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Mapadre pamoja na Watawa wanaoishi na kuhudumia Jimboni humo. Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na watoto na vijana kwenye Uwanja wa San Zeno.

Papa Francisko tarehe 18 Mei 2024 anafanya hija ya kichungaji Verona
Papa Francisko tarehe 18 Mei 2024 anafanya hija ya kichungaji Verona

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Watoto Ulimwenguni, kuanzia tarehe 25-26 Mei 2024 anawakumbusha watoto kwamba, wao wana thamani kubwa sana machoni pa Mungu na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kaulimbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5. Baba Mtakatifu anawaalika watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuguswa na historia ya watu mbalimbali katika maisha yao, bila kuwasahau watoto wanaoteseka kwa magonjwa, watoto ambao wamepokwa utoto wao na kwa sasa wanateseka sana. Hawa ni watoto wanaoathirika kutoka na vita na kinzani za kijamii; watoto wanaoteseka kwa baa la njaa na kiu; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto wanaolazimishwa kwenda kwenye mstari wa mbele kama chambo cha vita; watoto wanaokimbia kutoka kwenye familia zao kama wakimbizi na wahamiaji; watoto wanaotenganishwa na familia zao, kiasi cha kukosa fursa ya kuendelea tena na masomo.

Jengeni utamaduni wa kuwasikiliza watoto wadogo
Jengeni utamaduni wa kuwasikiliza watoto wadogo

Baba Mtakatifu anakaza kusema hawa ni: watoto wanaotumbukiwa kwenye magenge ya uhalifu Kitaifa na Kimataifa; watoto wanaoathirika kwa matumizi haramu ya dawa za Kulevya, Watoto wanaotumbukizwa kwenye mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Hawa ni watoto wanaopaswa kusikilizwa, ili kutolea sauti yao ushuhuda na hivyo kuonjeshwa tena huruma na upendo. Baba Mtakatifu anawatia shime watoto hawa kuwa na furaha kwa sababu wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Wajenge na kudumisha urafiki kwa kushirikishana na wengine, katika uvumilivu, ujasiri, ubunifu, hali ya kufikirika bila woga wala maamuzi mbele. Siri kuu ya maisha inasimikwa katika sala, ambayo Kristo Yesu amewafundisha wafuasi wake, ile Sala kuu, Sala ya Baba Yetu, itakayo wachangamotisha kuwa ni wajenzi wa dunia inayosimikwa, katika utu, haki na amani. Baba Mtakatifu atakutana na watu wa Mungu kutoka Verona kwenye Viwanja vya Michezo vya Arena ili kushiriki mkutano unaonogeshwa na kauli mbiu “haki na amani zitabusiana.” Zab 85:10. Baba Mtakatifu atajibu baadhi ya maswali yatakayoulizwa na wajumbe.

Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.
Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.

Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu baadaye atatembelea Gereza la Montorio la Verona na huko atapata nafasi ya kuzungumza na Askari Magereza, Wafungwa pamoja na watu wa kujitolea. Mama Kanisa katika maisha na utume wake kwa wafungwa magerezani anakazia hasa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wafungwa na askari magereza ni vyombo na mashuhuda wa Injili. Askari magereza wawe na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii. Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba, wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao.

Maisha ya gerezani ni magumu, yataka moyo!
Maisha ya gerezani ni magumu, yataka moyo!

Maisha ya gerezani ni magumu na mara nyingine yanaweza kukatisha tamaa, kwa mfungwa kuelemewa na upweke hasi, hali ya kukata tamaa na hatimaye kushindwa kuona hatima ya maisha yake. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasiwasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anawataka askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapasa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazopatikana kutokana na kazi na utume wao. Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha hija ya kichungaji Jimbo kuu la Verona kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Uwanja wa Michezo wa Bentegodi na baadaye atarejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake.

Papa Verona
16 May 2024, 15:33