Jumamosi tarehe 18 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kichungaji Jimbo la Verona. Jumamosi tarehe 18 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kichungaji Jimbo la Verona.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Jimboni Verona: Haki na Amani

Amani ya kweli haina budi kuendelezwa, kuandaliwa, kuhakikiwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Papa katika majibu yake kwa waandaaji wa Kongamano hili amekazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa kuwaweka maskini na wanyonge katika maisha na vipaumbele vya jamii kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Vijana waelimishwe na kuandaliwa kushiriki katika maisha ya kijamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ni katika muktadha wa mkesha wa Sherehe ya Pentekoste, Jumamosi tarehe 18 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kichungaji Jimbo la Verona, nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu “haki na amani zitabusiana.” Zab 85:10. Amani ya kweli haina budi kuendelezwa, kuandaliwa, kuhakikiwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu katika majibu yake kwa maswali aliyoulizwa na waandaaji wa Kongamano hili amekazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa kuwaweka maskini na wanyonge katika maisha na vipaumbele vya jamii kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Vijana waelimishwe na kuandaliwa kushiriki katika maisha ya kijamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungaman ya kijamii katika uhalisia wa maisha. Kinzani za kijamii, kitamaduni na kiuchumi zinapatiwa ufumbuzi wake kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi. Viongozi wasaidie kujenga mtandao wa ushirikiano na mshikamano kwa kutambua nguvu na udhaifu wao; pamoja na kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya katika mchakato wa demokrasia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, kuna haja ya kuwajibika katika kulinda na kutunza amani.

Haki, amani na utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Haki, amani na utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, maskini na wanyonge katika jamii wanapewa kipaumbele cha pekee katika maisha kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu aliyevunjilia mbali maamuzi mbele na kuwa ni kielelezo cha matumaini. Ili kuhitimisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kuna haja ya kutoa kipaumbele kwa maskini kwa kuondokana na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Mwelekeo huu unahitaji toba na wongofu wa ndani, tayari kutajirishana kwa tunu msingi za maisha. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga mazingira yatakayosaidia kukoleza maendeleo endelevu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, elimu makini ni ufunguo wa maendeleo ya kweli, kwa kutoa kipaumbele cha utu, heshima na haki msingi za binadamu; sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu mshikamano wa upendo na huduma. Kumbe, maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini; changamoto kwa waelimishaji miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa kutambua kwamba, vijana hawa ni sehemu jumuiya, historia na matumaini kwa siku za usoni.

Tangazeni na kushuhudia Injili ya matumaini
Tangazeni na kushuhudia Injili ya matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ulimwengu mamboleo kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadamu ni kutambua nguvu na udhaifu wako kadiri ya mpango wa Mungu. Katika utunzaji wa tamaduni za asili, hapo mwanadamu anaweza kugundua ndani mwake amana, utajiri, hekima na mang’amuzi.  Vita, kinzani na migogoro ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kitamaduni inaendelea kuzalisha ukosefu wa haki msingi kijamii, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kudumisha umoja unaosimikwa katika tofauti msingi; kwa kuondokana na tabia ya woga na wasi wasi; kwa kutafuta na kutambua vipaumbele, ili hatimaye, kujenga utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, haki na amani ni tunu zinazotishiwa na uchoyo na ubinafsi na kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wakati mwingine wanajisikia wanyonge au watu wenye nguvu kupita kiasi hata kuweza kujimwambafai, lakini wanapaswa kujenga umoja na ushirika; kwa kuwashirikisha vijana, ili waweze kujisikia kuwa ni wadau katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maendeleo. Kuna haja ya kuwekeza kwa vijana kwa njia ya elimu makini, malezi na majiundo sanjari na kuwarithisha tunu msingi za kijamii, kila mtu akihakikisha kwamba, anashiriki kikamilifu. Walimwengu wanapaswa kutoa pia upendeleo wa pekee kwa wanawake katika kuchangia mchakato wa ujenzi wa amani; washirikishwe katika majadiliano. Amani haiwezi kuwa ni matunda ya kutoguswa na mahangaiko ya wengine, kwa kujenga kuta za utengano pamoja kuwatishia watu. Kuna haja ya watu wa Mungu kuwa ni mashuhuda na vyombo vya kupandikiza Injili ya matumaini. Kamwe waamini wasichoke kutafuta na kudumisha amani duniani.

Haki na amani
18 May 2024, 15:48