Tafuta

Baba Mtakatifu amewafikiria wafungwa ambao wameshuhudia kwa mara nyingine tena kwamba, maisha, ubinadamu na matumaini yanazunguka nyuma ya kuta za magereza. Baba Mtakatifu amewafikiria wafungwa ambao wameshuhudia kwa mara nyingine tena kwamba, maisha, ubinadamu na matumaini yanazunguka nyuma ya kuta za magereza.   (Vatican Media)

Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Jimboni Verona: Hotuba Kwa Wafungwa

Katika hotuba yake kwa Askari magereza, wafungwa pamoja na watu wa kujitolea, amekazia kuhusu: Ufunuo wa Uso wa Mungu, mwingi wa huruma na mapendo; anayesamehe bila kuchoka; Mlango wa matumaini dhidi ya hali ya kukata na kujikatia tamaa, bali wawe na ujasiri wa kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu; Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu dhamana na utume wa Mama Kanisa Magerezani anakazia: Umuhimu wa Askari magereza kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili sanjari na kuwa na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Baba Mtakatifu anawapongeza Askari magereza kila wakati wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa maskini na wanyonge zaidi katika jamii, yaani wafungwa, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, ulinzi na usalama vinatawala ndani ya jamii. Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanatumia muda mrefu kuwa magerezani, ili kulinda na kudumisha ulinzi na usalama, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa barabara. Askari magereza wawe ni walinzi wa ndugu zao wafungwa, wawe ni madaraja kati ya magereza na jamii katika ujumla wake, kwa kuonesha upendo unaowawajibisha, ili kuondoa wasi wasi na kashfa ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anawataka Askari magereza kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kumbe, inawapaswa kusaidiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazojitokeza kutokana na kazi yao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Pentekoste, tarehe19 Mei 2024 ameyaelekeza mawazo yake kwenye hija ya kichungaji Jimboni Verona, Jumamosi tarehe 18 Mei 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “haki na amani zitabusiana.” Zab 85:10.

Papa Francisko: Wito: Boreshani maisha ya wafungwa na magereza!
Papa Francisko: Wito: Boreshani maisha ya wafungwa na magereza!

Baba Mtakatifu amewafikiria wafungwa ambao wameshuhudia kwa mara nyingine tena kwamba, maisha, ubinadamu na matumaini yanazunguka nyuma ya kuta za magereza. Katika hotuba yake kwa Askari magereza, wafungwa pamoja na watu wa kujitolea, amekazia kuhusu: Ufunuo wa Uso wa Mungu, mwingi wa huruma na mapendo; anayesamehe bila kuchoka; Mlango wa matumaini dhidi ya hali ya kukata na kujikatia tamaa, bali wawe na ujasiri wa kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu; Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru wale wote wanaosadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa wafungwa na mahabusu gerezani Montorio na kwamba, kila wakati anapoingia gerezani anaonja ule ubinadamu uliojaribiwa, watu wamechoshwa; watu wana shida, hisia za hatia, hukumu; hali ya kutoelewana; magumu na mateso; lakini wakati huo huo kuna nguvu ya ajabu, hamu ya msamaha; pamoja na hamu ya kusamehe. Lakini katika hali na mazingira kama haya kuna ufunuo wa Uso wa Kristo Yesu, Uso wa Mungu mwingi wa huruma na mapendo; anayesamehe kila wakati, changamoto na mwaliko kwa waamini ni kumwangalia Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo.

Askari Magereza wawe ni mashuhuda wa Injili ya matumaini
Askari Magereza wawe ni mashuhuda wa Injili ya matumaini

Hali ya magereza inatisha kutokana na magereza kufurika wingi wa wafungwa, na mwaliko unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wahusika ni kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe ili kuboresha hali na maisha ya wafungwa magerezani, ili daima kuwajengea mlango wa matumaini, dhidi ya utamaduni wa kifo na hali ya kujikatia tamaa. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini, dhidi ya utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kristo Yesu daima yuko pembeni mwao ili kuwafariji na kamwe hawezi kuwaacha watumbukie katika upweke. Wadau mbalimbali ndani ya magereza wawe na ujasiri wa kuwashika mkono wafungwa na kuwainua. Wafungwa wenyewe wasione aibu kuomba msaada na kwamba, wafungwa pia wajenge utamaduni wa kusaidiana, kwani watu wote wanayo haki ya kutumainia. Na kwamba, “tumaini halitahayarishi.” Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelelea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho wao na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku.

Askari Magereza wawe ni mashuhuda wa Injili ya matumaini
Askari Magereza wawe ni mashuhuda wa Injili ya matumaini

Baba Mtakatifu amewashukuru wote kutoka katika undani wa maisha yake na kuwataka waendelee kufanya hija ya maisha, kwani upendo unawaunganisha. Wajifunze katika maisha kwamba, kuna kuteleza na kuanguka, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanasimama na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mfungwa mmoja, kwa niaba ya wafungwa wenzake, amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hadi wakati huo, kulikuwa na wafungwa 592 wengi wao ni kutoka: Italia, Morocco, Albania, Nigeria, India, Pakistan, Romania, Tunisia, Poland, Pwani ya Pembe, Guatemala, Moldavia na Sri Lanka na kwamba, uwepo wa Baba Mtakatifu gerezani hapo ni ushuhuda kwamba, maisha yao yana thamani sana, hata kama katika uhalisia wa maisha yao wanahisi kutengwa na jamii, mwaliko kwa jamii, kuwapokea na kuwashirikisha tena katika jamii, mara baada ya kuhitimisha adhabu zao gerezani. Wafungwa wanasema, kwao familia ni kito cha thamani sana na alama ya matumaini, lingekuwa ni jambo jema, ikiwa kama wadau mbalimbali ndani ya magereza wangewasaidia wafungwa kuhisi mshikamano wa kifamilia, urafiki na udugu wa kibinadamu.

Mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wafungwa
Mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wafungwa

Naye Francesca Gioieni, Mkuu wa Gereza la Montorio lililoko mjini Verona katika hotuba yake ya utangulizi aliyoitoa mbele ya Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea gerezani hapo na kwamba, dhamana na wajibu wake msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wafungwa zinalindwa na kudumishwa. Ujumbe ambao wanapenda kuutangaza na kuushuhudia nje ya magereza ni kwamba, kuna wafungwa wanaoishi, licha ya kuvunja sheria, kanuni na taratibu za jamii, lakini utu na heshima yao vinapaswa kulindwa na kudumishwa; hawa ni watu wanaopaswa kusikilizwa na kuheshimiwa jinsi walivyo na kwamba, imani inarutubisha matumaini. Kazi ya Askari magereza inahitaji ujasiri, huruma na upendo na kwamba, hii ni changamoto pevu, inayohitaji kusindikizwa kwa njia ya sala. Mwishoni mwa hija yake kwenye gereza la Montorio mjini Verona, Baba Mtakatifu amependa kuwazawadia sifa kuu za Mungu: Ukaribu, Huruma na Upendo na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko karibu na waja wake na ni mpole. Bikira Maria akiwa amembeba Mtoto Yesu ni ishara ya huruma ya Mungu kwa waja wake.

Wafungwa Magerezani
20 May 2024, 14:21