Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Jimboni Verona: Hotuba Kwa Watoto na Vijana
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Watoto Ulimwenguni, kuanzia tarehe 25-26 Mei 2024 anawakumbusha watoto kwamba, wao wana thamani kubwa sana machoni pa Mungu na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kaulimbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5. Baba Mtakatifu anawaalika watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuguswa na historia ya watu mbalimbali katika maisha yao, bila kuwasahau watoto wanaoteseka kwa magonjwa, watoto ambao wamepokwa utoto wao na kwa sasa wanateseka sana. Hawa ni watoto wanaoathirika kutoka na vita na kinzani za kijamii; watoto wanaoteseka kwa baa la njaa na kiu; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto wanaolazimishwa kwenda kwenye mstari wa mbele kama chambo cha vita; watoto wanaokimbia kutoka kwenye familia zao kama wakimbizi na wahamiaji; watoto wanaotenganishwa na familia zao, kiasi cha kukosa fursa ya kuendelea tena na masomo. Baba Mtakatifu anawataka watoto na vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha baada ya kukutana na Kristo Yesu, hata kama katika safari ya maisha yao wanakumbana na matatizo na changamoto za maisha; furaha ya kweli ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, hii ni faraja ya ndani hata kati kati ya magumu na changamoto za maisha; kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wanajaliwa uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha na kwamba, Roho Mtakatifu daima anaongozana na waamini katika safari ya maisha yao. Kristo Yesu ni rafiki wa kweli katika maisha, kwani yuko pamoja na waja wake, anawasaidia na kuwashika mkono na kuwakinga katika hatari mbalimbali za maisha, ili kuwakirimia amani na utulivu wa ndani.
Watoto wamemuuliza Baba Mtakatifu Francisko kuhusu: Jinsi ya kusikia wito wa kumfuasa Kristo Yesu katika maisha yao, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu; Je, ni kwa jinsi gani watoto wanaweza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani; ni kwa jinsi gani watoto wanaweza kusimama imara katika imani. Kristo Yesu katika Injili aliwaita baadhi ya wafuasi wake na kuwatuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hata watoto katika maisha yao wanaweza kusikia wito wa Mungu wanapoonja huruma na upendo kutoka kwa wazazi na walezi wao; katika ukweli, wanapoishi katika upendo na jirani zao. Kumbe, wanapaswa kujenga utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu anapozungumza nao kwa njia ya Maandiko Mtakatifu na wanapotenda mema. Kristo Yesu amewatuma wafuasi wake kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu na kwamba, hata katika udogo wao wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu, huku wakiwa ni vyombo vya amani kwenye maeneo ya vita, kinzani na mipasuko. Watoto na vijana wawe ni alama ya haki na amani; kwa kushirikishana, kusikilizana. Watoto na vijana wanaweza kuwa na ujasiri wa kulinda, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake hata nyakati za giza na magumu ya maisha. Watoto wasimame kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani; kwa kusikilizana na kuvunjilia mbali woga usiokuwa na mvuto wa mala mashiko; kwa kubariki badala ya kulaani.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji Jimboni Verona, Jumamosi tarehe 18 Mei 2024. Hija hii ya kichungaji inanogeshwa na kauli mbiu “haki na amani zitabusiana.” Zab 85:10. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu inawakirimia amani na utulivu wa ndani. Lakini katika ulimwengu mamboleo, kuna watoto wengi ambao wameathirika kwa vita: baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; ukosefu wa huduma bora za afya. Ukosefu wa haki na amani ni matokeo ya baadhi ya watu wachache katika jamii kutawaliwa na uchu wa mali na madaraka; dharau na kutaka kujimwambafai na matokeo yake ni mashindano yasiokuwa na mvuto wa mashiko, kinzani na magomvi na matokeo yake ni vita isiyokuwa na “miguu wa kichwa.” Baba Mtakatifu anawataka watoto na vijana kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa haki na amani, ili kujenga dunia ambamo: haki, amani na utulivu vinatawala, sanjari na kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Zawadi, karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu yawasaidie kujenga mahusiano na mafungamano na watu wengine, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kuhakikisha kwamba, wote wanakuwa ni ndugu na mafariki kwa kupendana na kutembea kwa pamoja. Hii ni changamoto inayoweza kuvaliwa njuga mara moja, kwa kusaidiana kwa hali na mali; kwa kutakiana mema na kuwafanya wengine kuwa na furaha zaidi; kwa kuwasaidia wenye shida na mahangaiko, kwa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha kwa jirani zao.