Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Jimboni Verona: Hotuba Kwa Mapadre na Watawa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Fumbo la Kanisa linalosafiri katika mawimbi mazito ya bahari ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Picha hii ya Kiinjili inawakumbusha waamini mambo makuu mawili yanayopaswa kuzingatiwa: Kwanza huu ni wito unaopokelewa na kukaribishwa kila mara na pili ni utume unaotekelezwa kwa ujasiri. Hivi ndivyo Kristo Yesu mwanzoni kabisa mwa maisha na utume wake alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya aliwaona ndugu wawili wakitupa jarife baharini, kwa maana walikuwa ni wavuvi, akawaambia nifuateni na mara wakaziacha nyavu zao wakamfuata. Mwanzo wa maisha ya Mkristo ni ule uzoefu wa kukutana na Kristo Yesu, anayewasogelea kwa huruma na upendo, akibisha hodi katika nyoyo za waja wake, kwa mwaliko wa kutaka kuanzisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu. Hali hii inajionesha kwa namna ya pekee katika maisha na wito wa Mapadre na Watawa anayewaangalia kwa jicho la huruma na upendo, anayeinama na kuwachagua ili kushiriki katika utume wake, hii ni neema inayotolewa bure; ni zawadi inayofungua nyoyo za waja wake ili kushiriki mshangao wa Mungu katika maisha yao. Huu ni mwaliko kwa Mapadre na Watawa kuhakikisha kwamba, kamwe hawapotezi mshangao wa wito wao ambao wameupokea kwa neena na kwamba, kumbukumbu hii inapaswa kupyaishwa kila wakati. Huu ni utangulizi uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji Jimbo Katoliki la Verona, Jumamosi tarehe 18 Mei 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “haki na amani zitabusiana.” Zab 85:10.
Msingi wa watawa kuwekwa wakfu na ushiriki wa Mapadre katika utume ni pale wanapokubali kupokea wito na zawadi hii kutoka kwa Mungu inayowashangaza, changamoto na mwaliko wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wao, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Injili na kwa Kanisa kwa kutambua kwamba, si wao waliomchagua, bali ni Kristo Yesu aliyewachagua, akawaweka ili waende kuzaa matunda na matunda yao yapate kukaa! Rej. Yn 15:16. Watawa na Mapadre wakikumbuka wito huu, hata kama watakabiliana na mchoko kiasi gani pamoja na hali ya kukata tamaa, wataendelea kubaki watulivu na wenye imani thabiti, kwa sababu Kristo Yesu hatawaacha waende mikono mitupu! Ili kukabiliana na changamoto za maisha na wito wa kitawa na kipadre, kuna haja ya kukuza na kudumisha uvumilivu wa ndani, ili kukabiliana na mabadiliko ya ghafla pamoja na hatari zinazofumbatwa katika maisha na utume wao kama watawa na mapadre na kwamba, Kristo Yesu, kamwe hatawaacha pweke kwani Yeye ndiye asili na chimbuko la miito na utume wao. Wawe ni watu wa imani inayoweza kuwaokoa kila wakati na hata zile nyakati za shida na changamoto za wito na maisha ya kitawa na kipadre.
Baba Mtakatifu anawataka watawa na mapadre kuwa jasiri katika kutekeleza utume wao, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, alipowatokea kando ya Bahari ya Tiberia, Mitume ambao walikuwa wamekata tamaa kwani usiku ule hawakupata kitu, lakini kwa neno la Kristo Yesu wakatupa nyavu zao upande wa kuume wa chombo, wala sasa hawakuweza kulivuta tena jarife kwa sababu ya wingi wa samaki. Rej. Yn 21:6. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza watawa na mapadre wa Jimbo Katoliki la Verona kwa kuwa na ujasiri, wabunifu na wenye uwezo wa kumwilisha unabii wa Kiinjili katika maisha na utume wao. Huu ndio msingi wa watawa na mapadre waliojisadaka katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na wengi wao leo hii wanaheshimiwa na Mama Kanisa kama wenyeheri na watakatifu wa Mungu. Hawa ni mashuhuda wa imani, waliofanikiwa kuunganisha Neno la Mungu na huduma makini kwa watu wa Mungu; wakaonesha huruma na upendo kwa maskini na wahitaji zaidi; wakajikita katika “ubunifu wa kijamii” chemchemi ya shule, hospitali, nyumba za wazee; nyumba za wageni na maeneo ya kujifunza tasaufi ya Kikristo.
Wenyeheri na watakatifu kutoka Verona ni watu ambao wamepitia katika: matatizo na changamoto mbalimbali za maisha, wakakirimiwa na Mwenyezi Mungu upendo kutoka kwa Roho Mtakatifu na hivyo kuanzisha udugu mtakatifu; imani ikatafsiriwa katika ujasiri wa utume, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, changamoto kwa Kanisa katika ulimwengu mamboleo kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa hali na kipato: Watu wenye kiu ya matumaini; watu waliojeruhiwa katika maisha yao kutokana na makosa waliyotenda au ukosefu wa haki jamii, ambayo waathirika wake wakuu ni wanyonge ndani ya jamii. Watawa na mapadre watambue kwamba, wamerithi imani hai inayomwilishwa katika matendo kutoka katika historia ya maisha yao. Kamwe wasikatishwe tamaa kutenda mema, bali wawe na ujasiri katika utume wao kwa kutambua kwamba, Kanisa halina budi kujenga ujirani mwema na maskini, watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; waendelee kuganga na kuponya madonda ya watu wa Mungu, huku wakishuhudia huruma na upendo wa Mungu na kwa njia hii mtumbwi wa Kristo Yesu, yaani Kanisa unaweza kuokoa maisha ya watu wengi wanaokumbana na dhoruba katika maisha yao na kwamba, dhoruba hizi kamwe hazikosekani katika ulimwengu mamboleo. Dhoruba hizi zinakita mizizi yake katika ubakhili na uchoyo alama ya ukosefu wa imani; ulafi, utafutaji wa mali usiozuilika wa kuridhisha nafsi ya mtu na kwamba, mambo haya yanarutubishwa katika utamaduni wa uchoyo na ubinafsi; hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine pamoja na jeuri.
Dhoruba, kama tujuavyo, hazikosekani katika ulimwengu mamboleo; dhoruba nying zina mizizi yao katika ubakhili, ulafi, katika utafutaji usiozuilika wa kuridhisha nafsi yako, na wanalishwa katika utamaduni wa ubinafsi, usiojali na wa jeuri. Mtakatifu Zeno anawataka watawa kutojiruhusu kunaswa na minyororo ya uchoyo, ubakhili, mafanikio mabaya na hivyo kuna ukosefu wa haki, hatari kwa maisha ya watawa na mapadre. Mtakatifu Zeno anawataka watawa na mapadre kuhakikisha kwamba, nyumba zao zinakuwa wazi kwa wasafiri, wajitoe sadaka kwa ajili ya maskini na kwamba, haya ni maneno wanayopaswa kuyamwilisha katika maisha na utume wao na kamwe wasizoee kuogelea katika maovu! Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza kwa maisha na utume wao, anawataka wasonge mbele kwa ari na moyo mkuu, kwani wanayo neema na furaha ya kukaa katika Merikebu ya Kanisa, bila wasi wasi wala woga kwani Kristo Yesu, daima yuko pamoja nao, jambo la msingi ni kupokea wito na kuwa na ujasiri katika utume; kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirika kwani mbinguni wanapaswa kwenda wote, lakini motoni kila mtu “kivyake vyake.” Kumbe utakatifu wa maisha yao unapaswa kusimikwa katika upendo. Ni utakatifu unaosimikwa katika upendo wenye ujasiri tayari kupandikiza Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili; kwa kupandikiza upendo dhidi ya chuki, uhasama na utamaduni wa kifo. Verona ni mji wa upendo.