Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Jimboni Verona:roho ya ujasiri na maelewano

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake katika hija ya kichungaji jimbo Kuu la Verona nchini Italia Jumamosi 18 Mei 2024,wazo kuu ni kazi ya Roho Mtakatifu hasa ya kuleta Ujasiri wa kuishi maisha ya Kikristo.Kwa ujasiri huo maisha yetu yanabadilika.Mitume waliokuwa na hofu baada ya kupokea Roho Mtakatifu,walisonga mbele kwa ujasiri kuhubiri Injili.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

“Wakati fulani, mtume Paulo alikwenda katika jumuiya ya Wakristo na kuwauliza, “Je, mmepokea Roho Mtakatifu?” Na walijibu nini? "Roho Mtakatifu ni nini?" Hawakujua Roho Mtakatifu ni nini. Nadhani leo hii, nikiuliza jumuiya nyingi za Kikristo Roho Mtakatifu ni nini, hawatajua jinsi ya kujibu. Ndivyo Baba Mtakatifu Francisko ameanza mahubiri yake mara baada ya Masomo yaliyosomwa katika maadhimisho ya Misa Takatifu, iliyofunga ziara yake ya kichungaji katika Jimbo Kuu Katoliki la Verona nchini Italia tarehe 18 Mei 2024, ikiwa tayari ni kesha la Siku Kuu ya Pentekoste kwa mwaka 2024.

Wakati wa ibada ya Misa Takatifu
Wakati wa ibada ya Misa Takatifu

Papa akiendelea alisema kuwa: “Siku moja, katika misa ya watoto, ikiwa ni siku kama hii ya Pentekoste; kulikuwa na watoto zaidi ya 200  au chini yake ambapo niliuliza: “Roho Mtakatifu ni nani?” na watoto walianza kusema: “Mimi! Mimi! mimi!” kwani  kila mtu alitaka kujibu. Na mimi nilisema: jibu wewe,” aliye jibu alisema “aliyepooza” kwa sababu alikuwa amesikia “Neno (Paraclito yaani mfariji” na yeye alisema paralitico yaani  kupooza. Na mara nyingi nikiuliza, sisemi kwamba jibu litakuwa “aliyepooza”, lakini hatujui Roho Mtakatifu ni nani.

Papa mbele ya Sanamu ya Bikira Maria
Papa mbele ya Sanamu ya Bikira Maria

Baba Mtakatifu Francisko amesema kuwa: "Kaka na dada Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa maisha yetu! Ni kile kinachotupeleka mbele, kinachotusaidia kusonga mbele, kinachotufanya tuendeleze maisha ya Kikristo. Roho Mtakatifu yu ndani yetu. Kuweni waangalifu: sisi sote tumempokea, kwa Ubatizo, Roho Mtakatifu, na hata zaidi kwa Kipaimara! Lakini je, ninamsikiliza Roho Mtakatifu aliye ndani yangu? Je, ninamsikiliza Roho ambaye anausukuma moyo wangu na kuniambia: “Usifanye hivi, ndiyo fanya hivi”? Au Roho Mtakatifu hayupo kwa ajili yangu? Leo hii tunaadhimisha sikukuu ya siku ambayo Roho Mtakatifu alikuja. Lakini fikirieni: Mitume wote walikuwa wamefungwa kwenye karamu kuu. Waliogopa, milango ilikuwa imefungwa ... Roho Mtakatifu alikuja, akabadilisha mioyo yao, na wakatoka kwenda kuhubiri kwa ujasiri.

Maadhimisho ya Misa katika ziara ya kichungaji huko Verona
Maadhimisho ya Misa katika ziara ya kichungaji huko Verona

Ujasiri: Roho Mtakatifu hutupatia ujasiri wa kuishi maisha ya Kikristo. Na kwa sababu hiyo, kwa ujasiri huo, maisha yetu yanabadilika. Wakati mwingine tunakwenda katika kitubio tukiwa na dhambi zile zile: “Lakini Padre, ningependa kubadilisha maisha yangu, sijui jinsi ya kufanya…” Papa ameongeza: “Lakini msikilize Roho! Omba kwa Roho naye atabadilisha maisha yako.” Mwamini Roho”. Papa anasema.  Ni  sawa, Padre lakini, nina umri wa miaka 90, siwezi kubadilika sasa…” – Papa Francisko ameongeza: “Lakini je umebakiza siku ngapi za maisha?” jibu: “Eh, sijui” .... “Kwa siku moja tu, Roho anaweza kubadilisha maisha yako. Anaweza kubadilisha moyo wako!” Baba Mtakatifu kwa hiyo amesisitiza tena kuwa "Kwanza kabisa “Roho ndiye anayebadilisha maisha yetu. Je, mmeelewa hili?  Amewaomba Papa, waamini katika Uwanja huo mkubwa wa Verona kwamba: “Hebu turudie pamoja: “Roho hubadilisha maisha yetu”. Na  tena wote warudie: “Roho hubadilisha maisha yetu”. Papa aliongeza "Na hii ni nzuri."

Vijana katika uwanja wa Verona wakati wa ibada ya misa
Vijana katika uwanja wa Verona wakati wa ibada ya misa

Pili. "Mitume waliokuwa na hofu hiyo, walipopokea Roho Mtakatifu, walisonga mbele kwa ujasiri kuhubiri Injili. Na kwa njia hiyo  Roho Mtakatifu hutupatia ujasiri wa kuishi kikristo. Wakati mwingine tunakutana  na Wakristo ambao ni kama maji ya uvuguvugu: si moto wala baridi. Wanakosa ujasiri. Na wanauliza 'Padre ni wapi unaweza kuchukua kozi ya kuwa na ujasiri?' Papa ameongeza: “Hapana, ombeni kwa Roho. Mwamini Roho. Kwa sababu Roho hutupatia ujasiri wa kuishi kikristo." Kwa kusisitiza zaidi Papa ameomba kama wameelewa wote: “Je, mmeelewa hili? Wote kwa pamoja: “Roho hutupatia ujasiri.” Walirudia waamini, Papa aliongeza: "Na tazama! tuombe hivyo kwamba  Roho atusaidie kusonga mbele. Papa aliendelea kubainisha kuwa: “Na halafu, kuna jambo zuri sana ambalo Roho alifanya katika siku hiyo ya Pentekoste. Kulikuwa na watu wa mataifa yote, wa lugha zote, wa tamaduni zote na Roho, pamoja na watu hao, hujenga Kanisa."

Wakati wa kutoa vipaji
Wakati wa kutoa vipaji

Papa Francisko alisema: Roho hulijenga Kanisa. Je ina maana gani? Ni kitu cha kufanya ili kila mtu awe sawa? Hapana! Wote ni tofauti, lakini kwa moyo mmoja, kwa upendo unaotuunganisha. Roho ndiye anayetuokoa kutokana na hatari ya kutufanya sisi sote kuwa sawa. Hapana. Sisi sote tumekombolewa, sote tunapendwa na Baba, sote tulifundishwa na Yesu Kristo. Na Roho anafanya nini? Anafanya jambo hilo: yote kwa kila mtu." Na kuna neno linaloelezea hili vizuri kwamba: "Roho hutengeneza maelewano! Maelewano ya Kanisa."

Altare ya Misa Takatifu
Altare ya Misa Takatifu

Kila mmoja ni tofauti na mwingine, lakini ni katika mazingira ya maelewano. Papa tena ameomba waamini wote warudie kwa pamoja neno hilo: "Roho hutufanya kupatana." Kwa njia hiyo alisisitiza kwamba:"huo ndio muujiza wa siku hizi: kuchukua watu waoga na wenye hofu na kuwafanya wawe wajasiri; kuwachukua wanaume na wanawake wa tamaduni zote na kuwafanya kuwa na umoja wa wote na kuunda Kanisa. Kuwachukua watu hawa bila kuwafanya wawe sawa. Je Roho anafanya nini? Anafanya Maelewano." Kwa njia hiyo Papa amewaomba warudie kwa pamoja tena sentensi hiyo kuwa:  “Roho anaunda maelewano.

Huu ni Mwili wa Bwana wetu Yesu kwa ajili yetu
Huu ni Mwili wa Bwana wetu Yesu kwa ajili yetu

Katika hilo Baba Mtakatifu aliomba kila mmoja afikirie juu ya maisha yake mwenyewe. Kwa sababu: “Sote tunahitaji maelewano. Sote tunamhitaji Roho atupatie maelewano katika nafsi zetu, katika familia, katika jiji, katika jamii, mahali pa kazi.” “Kinyume cha maelewano ni vita, ni kupigana dhidi ya kila mmoja. Na vita vinapofanyika, mtu anapopigana na mwenzake, Je, Roho hufanya hivvyo, ndiyo au hapana? Wote walijibu: “Hapana”. Kwa hiyo “Roho huunda maelewano. Na pamoja na Mitume, siku aliyokuja, alikuwepo Mama, Bikira Maria. Tumwombe atupatie neema ya kumpokea Roho Mtakatifu; yeye, kama Mama, atufundishe kupokea Roho Mtakatifu." Papa Francisko amehitimisha mahubiri yake.

Mabuhiri ya Papa huko Verona 18 Mei 2024
18 May 2024, 17:58