Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatui tarehe 27 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na Wamonaki wa Kibudha kutoka nchini Thailand. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatui tarehe 27 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na Wamonaki wa Kibudha kutoka nchini Thailand.  (Vatican Media)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Wamonaki wa Kibudha Kutoka Thailand

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu amekutana na kuzungumza na Monaki wa Kibudha. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii; elimu makini, sala na tafakari ya kina. Baba Mtakatifu anasema, katika mkutano wao wa Mwezi Novemba 2023 walikazia umuhimu wa kujenga mahusiano na mafungamano katika kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika uso wa nchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko alikubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand pamoja na Serikali ya Thailand wa kutembelea nchini humo kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019. Kauli mbiu iliyoongoza hija hii ya kitume ni “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume.” Hija hii ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Siam kuanzia mwaka 1669 hadi mwaka 2019. Wakatoliki nchini Thailand wakaungana na vijana wa kizazi kipya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wanahimizwa kuzaa matunda ya ushuhuda wa imani yao, kwa kutambua kwamba, wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu alibahatika kukutana na kuzungumza na Patriaki wa Wabudha wa Thailand. Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa dhati katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani. Waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja, udugu na urafiki kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Vatican na Thailand kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia
Vatican na Thailand kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia

Ni katika muktadha huu, Mwezi Novemba, 2023 kulifanya majadiliano awamu ya saba kati ya Wakatoliki na Wabudha, tukio ambalo liliwashirikisha wajumbe zaidi ya 150 kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Asia. Mkutano huu ulinogeshwa na kauli mbiu “Karuna na Agape katika Mazungumzo ya Uponyaji wa Binadamu Waliojeruhiwa na Dunia." Leo hii ubinadamu na mazingira nyumba ya wote imejeruhiwa sana kutokana na vita, kiasi cha watu kulazimika kuyakimbia makazi yao. Kuna watoto wengi ambao wameathirika kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii pamoja na ukatili mkubwa dhidi yao. Licha ya changamoto zote hizi kwa watu ambao wamekita mizizi yao katika Mapokeo yao ya kidini na ambao wako tayari kufanya kazi kwa ushirikiano na kila mtu, wanaweza kuleta mwanga wa matumaini kwa wanadamu waliokata tamaa.

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Thailand 19-23 Novemba 2019
Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Thailand 19-23 Novemba 2019

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 27 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na Wamonaki wa Kibudha kutoka nchini Thailand. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii; elimu makini, sala na tafakari ya kina. Baba Mtakatifu anasema, katika mkutano wao wa Mwezi Novemba 2023 walikazia umuhimu wa kujenga mahusiano na mafungamano katika kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika uso wa nchi. Kumbe, kuna umuhimu wa kushirikiana na dini mbalimbali duniani, Serikali, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Wasomi na Wanasayansi ili kujenga urafiki wa kijamii unaodumisha: haki na amani, udugu wa kibinadamu na ulimwengu jumuishi. Pili ni elimu makini hasa miongoni mwa watoto na vijana wa kizazi kipya, ili kujenga na kudumisha mahusiano bora zaidi kati yao na katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wajumbe wa Mkutano huo walikazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa sala na tafakari, kama sehemu ya mchakato wa waamini kutakasa nyoyo na akili zao; ili kuibua upendo, huruma na msamaha pale penye chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipiza kisasi. Wajumbe hawa watapata nafasi ya kusali na kuombea amani kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria in Trastevere lililoko mjini Roma. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza kwa kumtembelea mjini Vatican na kwamba, wataendelea kuimarisha majadiliano ya kidini na ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki nchini Thailand kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Wamonaki wa Kibudha
27 May 2024, 14:24