Jubilei ya Miaka 350 ya Ibada Kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu: Chemchemi ya Huruma na Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Toba na upatanisho ni wazo linalojitokeza mara nyingi katika Maandiko Matakatifu na katika Agano la Kale limechukua mwelekeo wa kijamii wa fidia kwa ovu lililotendwa. Hi ndiyo Sheria ya Musa inayotoa fursa ya kurejesha kile kilichoibiwa au kujenga tena uhusiano uliosababishwa na ovu lililotendwa au kulipa fidia kwa kumtia mtu hasarani. Rej. Kut 22: 1-15 na Law 6:1-7. Hiki kilikuwa ni kitendo cha haki kilichojenga na kulinda maisha jamii. Katika Agano Jipya mwelekeo huu unakuwa ni sehemu ya mchakato wa maisha ya kiroho ndani ya mfumo wa Ukombozi ulioletwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, akawa ni fidia ya dhambi za walimwengu. Hiki ni kieleelzo cha neema, rehema na upendo wa Mungu kwa wenye dhambi. Kumbe, malipizi huchangia kukoleza upatanisho kati ya watu wenyewe, na pia upatinisho na Mwenyezi Mungu kwa sababu uovu unaotendwa dhidi ya jirani zako ni dhambi inayotendwa pia dhidi ya Mwenyezi Mungu. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari mmoja wapo alipomchoma Kristo Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama ya Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002 akatenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre. Yote haya ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko mjini Paray-le-Monial, nchini Ufaransa na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Maadhimisho haya yalianza kutimua vumbi tarehe 27 Desemba 2023 na kuhitimishwa tarehe 27 Juni 2025 katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Maadhimisho haya yananogeshwa na kaulimbiu “Kurejesha upendo kwa upendo” tema inayomwilishwa katika hija mbalimbali, maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa pamoja na mikutano ambayo imekuwa ikiendeshwa kama sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la kumbukizi ya miaka 350 tangu Kristo Yesu alipotokea huko mjini Paray-le-monial, nchini Ufaransa. Katika hotuba yake kwa washiriki wa Kongamano la Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko Paray-le-Monial, na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, amekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazoendelea kusiginwa katika ulimwengu mamboleo. Ni vyema waamini wakajitambua kwamba, wao ni wadhambi, tayari kukiri udhaifu wao na kuomba msamaha. Sadaka ya Kristo Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa binadamu mdhambi, chachu ya upatanisho kati ya Mwanadamu na Mwenyezi Mungu na kati ya binadamu wenyewe. Mwenyezi Mungu anaendelea kutoa machozi kutokana na kusiginwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbalimbali za dunia na hata kati ya watu wateule na watakatifu wa Mungu.
Kauli mbiu ya mkutano huu, inaonesha kwamba, makovu yanaweza kugangwa na kuponywa, ikiwa kama kuna utashi wa kutenda hivyo kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho, ili kurejesha amani na utulivu wa moyo! Toba na wongofu wa ndani pamoja na mambo mengine, inafumbatwa katika maisha ya mwamini kwa kutambua kwamba, ni mdhambi na anapaswa kuomba msamaha wa dhambi alizotenda na kwamba, Mwenyezi Mungu yuko tayari kumpokea mwamini aliyevunjika na kupondeka moyo, ili aweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Toba na msamaha ni kutambua dhambi zilizotendwa kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu aliyetambua ndani mwake kwamba, amekosa juu ya mbingu na mbele ya Baba yake Mwenye huruma. Rej. Lk 15:21. Kuomba msamaha kunafungua majadiliano yanayopania pamoja na mambo mengine, kurejesha mahusiano na mafungamano katika upendo wa kidugu, tayari kuonja faraja, pamoja na kupokea msamaha unaotolewa na huo ni mwanzo wa kuchipua tena fadhila ya upendo ili kuganga madonda ya moyo! Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko Paray-le-Monial, alimwomba, watu wafanye toba na malipizi kwa maondoleo ya dhambi zinazoendelea kuutesa Moyo wake Mtakatifu. Hii ndiyo dhamana na wajibu wa wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, waamini wanaendeleza ibada ya toba na maondoleo ya dhambi, kama sehemu ya hija ya toba na wongofu wa ndani inayotekelezwa na kila Mbatizwa ndani ya Kanisa.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko Paray-le-Monial, na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, yataibua upendo kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakaza kusema: Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma na upendo wa Mungu. Ni matumaini yake kwamba, Madhabahu ya Paray-le-Monial nchini Ufaransa yataendelea kuwa ni kitovu cha faraja, upendo na huruma ya Mungu kwa watu wanaotaka kutubu na kumwongokea Mungu ili awakirimie amani na utulivu wa ndani!