Jubilei ya Miaka 750 ya Jiji la Amsterdam: Muujiza wa Ekaristi Takatifu wa Mwaka 1345
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” kama sehemu ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu anasema, uzoefu na mang’amuzi ya hija, yaani safari ya maisha ya kiroho ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Ikumbukwe kwamba, maisha ya mwanadamu ni hija kuelekea mbinguni kwa Baba wa milele. Hija inahitaji maandalizi, sadaka na majitoleo. Kimsingi hija inapania kuwa ni nyenzo ya toba na wongofu wa ndani, ili kuomba tena huruma, neema na baraka za Mwenyezi Mungu katika maisha na utume. Jiji la Amsterdam, nchini Uholanzi tarehe 27 Oktoba 2025 litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 750 tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho haya yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 27 Oktoba 2024. Haya ni maadhimisho yanayogusia historia ya Jiji la Amsterdam, matarajio yake kwa siku zijazo pamoja na mbinu mkakati wa kufikia malengo haya.
Ni katika muktadha huu, mahujaji kutoka Jijini Amsterdam, Jumamosi tarehe 4 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Miaka 750 tangu Jiji la Amsterdam lilipoanzishwa. Ustawi na maendeleo ya Jiji hili umechangiwa pia na imani ya Kanisa Katoliki, hususan Muujiza wa Ekaristi Takatifu uliotokea kunako mwaka 1345, hadi leo hii, watu wa Mungu wanaendelea kuadhimisha kumbukizi hii katika hali ya kimya kikuu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kila mwaka wakati wa Dominika ya Matawi. Ilikuwa ni tarehe 12 Machi mwaka 1345 siku chache kabla ya kuadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, yaani Dominika ya Matawi, Ysbrand Dommer aliyedhani kwamba, kutokana na ugonjwa uliokuwa unamwandama, siku zake za kuishi zilikuwa zinahesabika. Kumbe, akamwomba Paroko wa Kanisa la Oude Kerk ampelekee Mpako Mtakatifu pamoja na Ekaristi Takatifu. Ysbrand Dommer alipomaliza tu kukomunika, akatapika sana na matapishi yake, yakatupwa motoni.
Siku iliyofuata, Ysbrand Dommer alionekana kuwa na afya njema. Mmoja wa wauguzi wake alikwenda sehemu walikokuwa wamewasha moto na kugundua jambo la ajabu, kwamba, moto ulikuwa umeizunguka Ekaristi Takatifu bila ya kuteketea! Jambo ambalo lilimfanya yule muuguzi kupiga ukelele na mashuhuda walipofika mahali pake, wakaichukua ile Ekaristi Takatifu na kumpelekea Paroko. Muujiza huu uliendelea kwa muda wa siku tatu, na kila wakati Paroko ilimbidi aende nyumbani kwa Ysbrand Dommer, kiasi kwamba, ikaamriwa nyumba hii igeuzwe kuwa ni Kikanisa cha Ekaristi Takatifu na baada ya Askofu Jan van Arkel, wa Jimbo Katoliki la Utrech, kupewa taarifa rasmi, akaidhinisha kwamba, iwepo Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu nyumbani hapo. Kunako mwaka 1452 Kikanisa hiki kiliungua moto, lakini Monstranti iliyokuwa inahifadhi Ekaristi ya Muujiza, ilibaki salama. Muujiza wa Ekaristi Takatifu ni kati ya matukio yaliyokumbukwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na mahujaji kutoka Jijini Amsterdam. Amewapongeza kwa jitihada wanazofanya kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, dhamana inayotekelezwa kwa ushirikiano mkubwa na Shirika la Wamisionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta; Huduma ya kichungaji kwa wahanga wa matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Huu ni utume unaotekelezwa kwa ushirikiano na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao makuu yake mjini Roma. Jiji Amsterdam lina wakazi wengi kutoka katika Mataifa mbalimbali na kwamba, Makanisa ni mahali panapowakutanisha watu wa aina zote kijamii na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza kwa ushuhuda wa maisha yao yanayosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Anawatakia heri na baraka, ili waendelee kushirikiana kufanya kazi katika Jiji la Amsterdam, huku wakishirikiana na neema ya Mungu. Katika maisha na utume wao, waendelee kuwa ni mashuhuda wa furaha ya imani na upendo kwa jirani zao, huku wakiwa wanaimarishwa kwa Ekaristi Takatifu, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na mshikamano miongoni mwa wa wakazi wa Jiji la Amsterdam, nchini Uholanzi. Mwishoni, amewaweka mahujaji kutoka Amsterdam chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, iloi awasaidie kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na upendo.