Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar: Umoja na Ushirika wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar ni mojawapo kati ya madhehebu ya Ukristo wa mashariki yenye ushirika kamili na Baba Mtakatifu pamoja na Kanisa Katoliki lote. Hili ni dhehebu linalofuata Mapokeo na Liturujia ya Mesopotamia lakini linapatikana hasa India na katika nchi mbalimbali ambapo waamini wake wamehamia, kama vile Marekani, ambako lina majimbo mawili, na Canada, Australia na Uingereza ambako kuna jimbo mojamoja. Kwa jumla Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar, lina waamini milioni 4-5, wakiongozwa na Askofu mkuu wa Ernakulam-Angamaly na maaskofu wengine 63, mapadri 9,121 katika parokia 3,224. Huu ni utume wa Mtakatifu Thoma, Mtume. Hivi karibuni waamini wa Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar wamempata Kiongozi wao, Askofu mkuu Mar Raphael Thattil, wa Jimbo kuu la Ernakulam-Angamaly, ambaye Jumatatu tarehe 13 Mei 2024 akiwa ameambata na viongozi waandamizi pamoja na wawakilishi wa Jumuiya ya Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar mjini Roma, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo yafuatayo: Historia, amana na urithi wa watu wa Mungu, umuhimu wa kuepuka kishawishi cha utengano na badala yake wajenge umoja na ushirika wa Kanisa; wajizatiti kudumisha matumaini katika uvumilivu. Amewapongeza kwa kujitosa kimasomaso katika malezi ya kifamilia sanjari na katekesi makini na kwamba, Jumuiya ya Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar mjini Roma inao wajibu wa kukuza na kudumisha ushirika katika upendo. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar linafahamika sana nchini India, kielelezo makini cha utume wa Mtakatifu Thoma; ni Kanisa linalokabiliana na changamoto mamboleo, zinazotishia umoja na ushirika wa Kanisa.
Baba Mtakatifu amewataka waamini hawa kutambua umuhimu wa asili ya Kanisa lao kujitegemea kisheria “Sui iuris” na hivyo kuwa tayari kuchukua hatua kutatua matatizo na changamoto zilizoko mbele yao. Wajibu huu utekelezwe kwa kuwajibika, kwa kuendelea kujikita katika ujasiri wa kiinjili, daima wakiwa wameungana na Askofu mkuu na Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar. Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni aliwaandikia barua pamoja na kuwatumia ujumbe kwa njia ya video, akiwaonya juu ya kishawishi cha kutaka kujitenga. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwahimiza waamini kujikita katika ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa, kwani huu ni wajibu msingi na hasa kwa Mapadre ambao wameahidi utii na kwa waamini wanatakiwa kuwa ni mfano wa upendo na unyenyekevu. Mahali penye utii hapo kuna Kanisa na mahali pasipokuwa na utii hapo kuna utengano. Huu ni wajibu wa Kanisa kuhakikisha kwamba, linajenga na kudumisha umoja na ushirika kwa njia ya sala na kwamba, milango ya Kanisa iko wazi kwa wale waliokengeuka na kutaka kujitenga, wapate fursa ya kutubu na kurejea tena kama ilivyokuwa kwenye Injili ya Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu. Rej. Evangelii gaudium, 46.
Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuachana na kiburi na hivyo kuendelea kujikita katika ujenzi wa amani na maelewano; kwa kuheshimu Ekaristi Takatifu kama Sakramenti ya upendo, umoja na imani, ili kujenga ushirika wa Kanisa na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa amani, kwa kuheshimu na kuthamini karama na mapaji mbalimbali waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu. Katika shida, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kanisa, watu wa Mungu wasimame kidete katika fadhila ya matumaini, kwa kuwa na jicho la pekee kwa maskini, watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii nchini India na Diaspora bila kuwasahau waathirika wa mgogoro huu katika ujumla wao. Waamini wawe na ujasiri wa kujibu ubaya kwa kutenda wema, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amewapongeza waamini wa Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar kwa kujikita katika malezi makini ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya kifamilia sanjari na Katekesi makini; utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na azma ya kukuza na kuendeleza miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, haya ni mambo msingi ambayo anaendelea kuwaombea kila siku katika sala zake na ametumia fursa hii, kuwatia shime ili wasonge mbele kwa ari na moyo mkuu. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, awaunganishe tena kuzunguka Altare ya Bwana, tayari kuyatafakari Madonda Mtakatifu ya Kristo Yesu kama alivyofanya Mtakatifu Thoma, Mtume.
Hata leo hii, Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu yanajionesha miongoni mwa watu wenye njaa na kiu ya haki; wagonjwa hospitalini na wafungwa magerezani; watoto na watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Wote hawa wanapaswa kuguswa na kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu; msamaha na upatanisho wa kweli. Ni mshangao wa huruma na upendo wa Kristo Yesu, uliomsukuma Mtakatifu Thoma, Mtume kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yake; imani ikawa ni nguvu ya kuweza kuvuka vikwazo vyote vya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Jumuiya ya Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar mjini Roma inao wajibu wa kukuza na kudumisha ushirika katika upendo sehemu mbalimbali za dunia.