Roho Mtakatifu na Bibi Arusi: Roho Mtakatifu Anawaongoza Watu wa Mungu, Yesu Tumaini Letu

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha Katekesi kuhusu kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo, Jumatano tarehe 29 Mei 2024 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Katekesi hii itawazamisha waamini katika historia ya wokovu: Agano la Kale, Agano Jipya pamoja na nyakati za Kanisa kwa kumkazia macho Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo, Jumatano tarehe 29 Mei 2024 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Tafakari hii imenogeshwa na Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo 1: 1-2: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” Mwa 1: 1-2. Baba Mtakatifu anasema, katika Katekesi hii atawazamisha waamini katika hatua kuu tatu muhimu katika historia ya wokovu: Agano la Kale, Agano Jipya na Nyakati za Kanisa. Daima waamini wakimkazia macho Kristo Yesu ambaye ni tumaini lao. Kile ambacho kiliahidiwa kwenye Agano la Kale, kinapata utimilifui wake kwenye Agano Jipya na la Milele katika Kristo Yesu. Katekesi hii ni kama kufuata mzunguko wa jua tangu machweo hadi kuzama kwake. Ni katekesi inayojikita kwa Roho Mtakatifu katika kazi ya uumbaji, Mbingu na nchi zinatangaza utukufu wa Mungu na kwamba, kwa Katekesi hii, waamini na watu wenye mapenzi mema, wamtambua Roho Mtakatifu Muumbaji, “Veni creator Spiritus. “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” Mwa 1: 1-2. Nguvu ya Roho Mtakatifu inaiongoza dunia tangu kuumbwa kwake na hivyo kujenga utulivu katika maisha na kwamba, dunia “Kosmos” kwa Lugha ya Kigiriki na “Mundus” kwa lugha ya Kilatini ni kielelezo cha uzuri, mpangilio safi na wenye utulivu kwa sababu Roho Mtakatifu ni Roho wa utulivu.

Roho Mtakatifu na Bi Arusi
Roho Mtakatifu na Bi Arusi

Mzaburi anasema, “Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake” Zab 33:6 na kwamba “Waipeleka roho yako, wanaumbwa, nawe waufanya upya uso wa nchi. Zab 104:30. Hapa kazi ya Roho Mtakatifu inafafanuliwa kwa kina na mapana, kama chanzo cha uumbaji na kama ilivyokuwa siku ile ya Ubatizo wa Kristo Yesu na wakati Mitume walipokuwa chumba cha juu, akawavuvia Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa kwa Mwenyezi Mungu siku ile ya kwanza ya kazi ya Uumbaji. Mtakatifu Paulo Mtume anaunganisha nguvu ya Roho Mtakatifu na kazi ya uumbaji kwa kusema kwamba, viumbe vyote pia vinaugua kwa pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Rej. Rum 8:22. Viumbe vinateseka kwa sababu mwanadamu amejikabidhi kwenye utumwa wa uharibifu. Huu ni ukweli unaomsonga mwanadamu katika ulimwengu mamboleo na kwamba, Mtume Paulo anaona kabisa sababu za mahangiko ya kazi ya uumbaji, uharibifu pamoja na dhambi katika maisha ya mwanadamu, hali ambayo inamwondoa mwanadamu kutoka mbele za Mungu. Kama ilivyokuwa kwa nyakati zile, ukweli huu unaendelea kuonekana hasa sehemu zile ambazo zimeonesha uroho wa kukwapua rasilimali za dunia. Mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi katika hili ni mwaliko wa kumsifu Mungu sanjari na kuyatafakari matendo yake makuu kwani mbingu zahubiri utukufu wa Mungu na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Huu ni wimbo ambao waamini wanaourejea mara kwa mara wakati wanapoimba wimbo wa “Mtakatifu.” Huu ni mwaliko wa kuwa na furaha wakati wa kuyatafakari matendo makuu ya Mungu, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi ambaye hakutaka kumiliki chchote kile.

Roho Mtakatifu na Bibi Arusi, Roho Mtakatifu, Yesu Tumaini letu
Roho Mtakatifu na Bibi Arusi, Roho Mtakatifu, Yesu Tumaini letu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hapo mwanzo nguvu ya Roho Mtakatifu ilileta mageuzi makubwa na hivyo kuwamiminia waamini nguvu yake inayoleta mageuzi makubwa. Hata leo hii, dunia imegawanyika na kuikuta ikiwa na kinzani kutoka nje, yaani kinzani za kijamii na kisiasa; vita, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, bila kusahau ukosefu wa haki jamii. Haya ni mambo ambayo yako nje ya maisha ya mwanadamu, lakini pia kuna kinzani na mipasuko ndani ya sakafu ya moyo wa kila mwamini. Hapa waamini wanahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu ili kurekebisha hali hii ya vita na vurugu, jambo la msingi ni kwa waamini kumfungulia Roho Mtakatifu maisha yao. Mwishoni mwa Katesi yake, Baba Mtakatifu Francisko anatumaini kwamba, Katekesi hii itasaidia kuamsha tena tamaa, uzoefu na mang’amuzi ya Roho Mtakatifu, ndiyo maana katika Mapambuzuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, Mama Kanisa anaweka mdomoni kilio cha waja wake kikisema “Veni creator Spiritus” yaani “Njoo Roho Muumbaji, washa nyoyo zetu kwa mapendo yako; utuletee neema nyoyoni mwetu” ili tugeuke na kuwa watu wapya zaidi kwa njia ya nguvu yako. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwapongeza Mapadre kutoka Bergamo wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Katekesi
29 May 2024, 16:12

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >