Kikosi cha Walinzi wa Papa: Askari Wapya 34 Wala Kiapo cha Utii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss Guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu kwa kuongozwa na kauli mbiu “Acriter et fideliter” yaani Ujasiri na Uaminifu na kilianzishwa na Papa Giulio wa Pili tarehe 22 Januari 1506. Jumatatu tarehe 6 Mei 2024 Wanajeshi 34 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswisi, wanafanya kumbukumbu ya Askari 189 kutoka Uswisi waliofariki dunia kunako mwaka 1527 wakati wa kumlinda Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa ni Papa Clement VII dhidi ya Mfalme Charles V. Tangu wakati huo, hawa wamekuwa ni walinzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni Askari wakakamavu, nadhifu, wapole na waungwana wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji mkubwa kwa ajili ya Papa, waamini na mahujaji wanaofika mjini Vatican kwa shughuli mbalimbali! Walinzi hawa kila mwaka hula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro mbele ya Mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa Jumatatu tarehe 6 Mei 2024 ni Askofu mkuu Edgar Robinson Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican. Sherehe hizi zimeanza kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza kwa moyo wao wa ukarimu na sadaka kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Kanisa. Kila siku, anaonja majitoleo yao, weledi na upendo unaobubujika kutoka katika shughuli zao! Baba Mtakatifu anawapongeza wana familia wa wanajeshi hawa ambao wameridhia uamuzi wao wa kujisadaka kwa ajili ya Vatican na kuendelea kuwasindikiza kwa upendo na sala zao pamoja na kuwapatia elimu, malezi makini pamoja na mazingira muafaka yanayowawezesha kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Baba Mtakatifu aliwakumbusha kwamba, mwaka huu, wanajeshi hawa wanakula kiapo cha utii wakati ambapo Mama Kanisa anaendelea kushangilia Fumbo la Pasaka, changamoto na mwaliko hata kwa wao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Mfufuka, kwa kutangaza furaha ya Pasaka; kwa kueneza utamaduni wa Ufufuko wa wafu dhidi ya utamaduni wa kifo, unao onekana kutaka kuwameza watu wengi.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia sifa njema ya Askari hawa: mahusiano na mafungamano ya familia kubwa; ujenzi wa kambi mpya kwa ajili ya maisha ya kifamilia; umuhimu wa maisha ya kijumuiya. Baba Mtakatifu anasema, kambi ya Jeshi iwe ni mahali pa kujifunza kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha majadiliano, ukweli wa maisha, mahusiano mema pamoja na maelewano. Katika hali na mazingira kama haya, kutakuwepo na nyakati za furaha pamoja na nyakati za majonzi. Kipindi hiki, kiwe ni fursa ya kujenga urafiki mwema, kwa kuheshimu na kuthamini mawazo yanayotolewa na wengine; kwa kuendelea kujifunza kuona kwa mwingine yule ndugu na jirani ambaye ni mwadani wa safari ya pamoja. Tabia hii itawawezesha kuishi katika Jamii wakiwa na mwelekeo sahihi wa maisha, kwa kutambua tofauti za kitamaduni, kidini na kijamii kama amana na utajiri na wala si tishio la maisha. Hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo kutokana na uwepo wa makundi makubwa ya watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Kwa hakika wanaonesha utashi wa huduma, hali inayowataka kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano mema kati yao, wajitahidi kufanya mapumziko na kutembea kwa pamoja pale inapowezekana.
Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi hawa wajenge na kudumisha mahusiano na mafungamano mema kati yao kwani mwelekeo huu ni muhimu sana katika maisha ya Kanisa. Kristo Yesu ni shuhuda ya kwamba Mungu ni upendo na kwamba, mahusiano mema ni njia inayowaelekeza katika ukomavu wa kiutu na Kikristo, urithi na amana kutoka kwa wazazi wao, ndugu na jamaa, wanandani shuleni, marafiki na wafanyakazi wenzao. Wanajeshi hawa wanaishi kama ndugu wamoja kwa kipindi cha walau miaka miwili; ni muda wa kazi, maisha na ujenzi wa mahusiano na mafungamano sanjari na ushirika katika umoja na tofauti zake msingi na kwamba, kambi ya jeshi ni muhimu sana. Baba Mtakatifu amewaambia wanajeshi hawa kwamba, kuna ujenzi wa kambi mpya ya wanajeshi itakayowezesha kuishi pamoja na familia zao, kwani kwa sasa wanalazimika kuishi peke yao bila familia zao: Kumbe, kukamilika kwa ujenzi wa kambi mpya kutasaidia kujenga na kuimarisha mahusiano ya kifamilia kambini hapo. Baba Mtakatifu amewasihi wanajeshi hawa kujitahidi kujenga maisha ya kijumuiya, iwe ni fursa ya kuufahamu mji wa Roma, wajitahidi kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu, kucheza pamoja na kuendelea kushirikishana tunu msingi za maisha, zitakazowaambata katika hija ya maisha yao yote. Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka katika maadhimisho ya Sikukuu hii, kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na watakatifu walinzi na waombezi wao.
Itakumbukwa kwamba, Jumamosi tarehe 4 Mei 2024 Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na Rais Viola Amherd, wa Shirikisho la Uswisi ambaye amekuja kuhudhuria sherehe ya Wanajeshi 34 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswisi wakila kiapo cha utii. Baadaye Rais Viola Amherd amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu pamoja na Rais Viola Amherd, wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili; ukarabati wa nyumba za wanajeshi wanaoendelea kujisadaka kwa ukarimu kwa ajili ya Baba Mtakatifu ni mambo ambayo yalipewa uzito wa pekee. Baadaye, viongozi hawa wamejikita katika masuala ya kimataifa mintarafu vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine; Israeli na Palestina na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kulinda amani duniani; kwa kutumia diplomasi katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazoendelea kuwaandama watu wa Mataifa sanjari na kukomesha uhasama na uadui kati ya Mataifa.
Padri Thomas Widermer, Padri mshauri wa kiroho wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss anasema, wanajeshi hawa ambao wengi wao ni vijana, wenye matumaini makubwa mbele yao, wanaunda Parokia ya pekee na kumbe, kazi ya Padri mshauri ni kuhakikisha kwamba, anawasaidia katika majiundo na ukomavu wa maisha ya kiroho na kimwili. Wanatambua kwamba, hapa Roma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, kumbe, hata wao wanapaswa kuwa na mtazamo na mwelekeo kama huu wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anasema, kuna sababu mbalimbali ambazo zinaweza kuwasukuma vijana kutaka kujiunga na Kikosi cha Ulinzi wa Papa. Mosi ni kwamba, vijana wanataka kupata uzoefu, mang’amuzi na weledi kuhusiana na wito pamoja na taaluma ya kijeshi. Wengi wao, hii ni nafasi ya kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo, kwa kufanya utume wao karibu sana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wanatambua kwamba, ufahamu wa mazingira ya mji wa Vatican na lugha ya Kiitalia ni utajiri mkubwa ambao unaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo zao wakati wote! Padri mwongozi wa maisha ya kiroho amepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, anawasaidia vijana hawa wanaojiandaa kwa utume maalum, kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho na kiutu. Kwa mfano, wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, walijifunza kwa umakini mkubwa kuhusu dhana ya huruma ya Mungu kama inavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Uso wa huruma, “Misericordiae vultus”.
Katika majiundo yao, wanapata katekesi ya kina na endelevu kuhusu: uaminifu, maana ya sadaka na zawadi ya maisha; ulinzi na usalama; dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika Kanisa la Kristo. Hiki pia ni kipindi kinachowawezesha askari hawa kupata utajiri wa kitamaduni kwa kufanya hija katika maeneo muhimu ya kihistoria. Wanajeshi hawa wanajifunza kwa kina na mapana matendo ya huruma kiroho na kimwili, kwani ni sehemu ya vinasaba vya utume wao. Mara nyingi hawa ndio wanaomsindikiza mtunza sadaka mkuu wa Papa katika kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika mitaa ya Roma nyakati za usiku, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.