Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mama Kanisa pia ameadhimisha Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day Rome 2024” Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mama Kanisa pia ameadhimisha Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day Rome 2024”  (Vatican Media)

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni 2024

Mama Kanisa anaadhimisha: Utukufu na Ukuu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli, na kuabudu Umoja wa Mungu katika enzi ya fahari yake. Kwa neema ya Ubatizo katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanashiriki uzima wa Utatu Mtakatifu hapa duniani katika giza la imani na baada ya kifo katika mwanga wa milele. Adhimisho hili ni ufunuo wa: wema, huruma, upendo, mamlaka na nguvu kutoka kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hivyo ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza. Hili ni fundisho la kweli ya imani. Imani Katoliki ndiyo hii: Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, nyingine ya Mwana na nyingine ya Roho Mtakatifu, ni umungu mmoja, wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu; utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele. Rej. KKK 222-266. Mama Kanisa anaadhimisha: Utukufu na Ukuu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli, na kuabudu Umoja wa Mungu katika enzi ya fahari yake. Kwa neema ya Ubatizo katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanashiriki uzima wa Utatu Mtakatifu hapa duniani katika giza la imani na baada ya kifo katika mwanga wa milele. Adhimisho hili ni ufunuo wa wema, huruma, upendo, mamlaka na nguvu zinazobubujika kutoka katika Fumbo la Utakatifu Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 25 na 26 Mei 2024, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mama Kanisa pia ameadhimisha Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day Rome 2024” inayonogeshwa na kauli mbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amesema: Mungu ni Familia inayoundwa na Baba, Mwana na Roho Mtakatifu chemchemi ya furaha na kwamba, Kristo Yesu katika maisha na utume wake alionesha upendo wa pekee kwa watoto, mwaliko na changamoto kwa watoto kujenga na kudumisha urafiki na Kristo Yesu kwa njia ya sala inayomwilishwa katika upendo dhidi ya vita, umaskini, magonjwa na njaa: watoto wajikite katika ujenzi wa upendo na mshikamano ili kuunda familia moja!

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya kwanza ya watoto ulimwenguni
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya kwanza ya watoto ulimwenguni

Baba Mtakatifu anasema, Mungu Baba Mwenyezi ndiye Muumba wa mbingu na dunia na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Waamini wanasali na kumtafakari Mungu Baba Mwenyezi kwa Sala ile kuu, yaani Sala ya Baba Yetu. Kristo Yesu ni Mwana pekee wa Baba wa milele, ambaye daima yuko pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahari. Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za walimwengu na daima hachoki kusamehe na kusahau, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma, upendo na msamaha wake bila kuchoka wala kukata tamaa, tayari kumletea mja wake mabadiliko ya ndani. Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana, anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana, aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Roho Mtakatifu ni mfariji na ndiye anayewakirimia waamini nguvu baada ya kumpokea katika Sakramenti ya Ubatizo na Sakramenti ya Kipaimara. Kwa imani na matumaini, Roho Mtakatifu anawakirimia waamini furaha ya maisha na uzima wa milele. Kumbe imani ya Kanisa Katoliki imesimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu: Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa. Mwenyezi Mungu ameumba vitu vyote, Kristo Yesu, amewakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti na Roho Mtakatifu anawatakatifuza waamini na kuwakumbusha yote aliyofundisha Kristo Yesu. Baba Mtakatifu amewaalika watoto kusali na kuwaombea wazazi na walezi wao; wasisahau kuwaombea watoto wagonjwa; waendelee kuombea haki na amani ulimwenguni, ili vita itoweke kwenye uso wa dunia, watoto wapate amani na utulivu.

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Familia inayoundwa na Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, ufunuo wa huruma na upendo usiokuwa na kikomo. Mwenyezi Mungu anaendelea kutembea na waja wake, ili kuwarimia furaha na kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao siku zote, hata ukamilifu wa dahari. Rej. Mt 28: 20. Hii ndiye chemchemi ya furaha inayowakutanisha watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ili kusherehekea Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini sana na kwamba, Kristo Yesu ni rafiki wa kweli na muhimu sana katika maisha na anayeendelea kutembea pamoja nao katika safari ya maisha yao huku Bondeni kwenye machozi. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionesha upendeleo wa pekee kwa watoto wadogo, alipowaona wakimzunguka na kucheza pembeni mwake; Jambo la msingi kwa watoto hawa ni kujenga na kudumisha urafiki wa kweli na Kristo Yesu ili waweze kupata furaha na utimilifu wa maisha. Katika maisha yao, watoto wanaweza kumwona Kristo Yesu miongoni mwa wazazi na walezi wao wanaowakirimia maisha, upendo, huruma na faraja; wanafunzi wenzao, walimu, makatekista pamoja na Maparoko wao, hawa ni watu wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao; hawa ni chemchemi ya furaha, siri kubwa ya maisha!

Watoto wameupamba Uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican
Watoto wameupamba Uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican

Ikiwa kweli watoto wanataka kujenga mahusiano, mafungamano na urafiki wa kweli hawana budi kujibidiisha kumtafuta kila siku katika maisha ya sala; kupendana wao kwa wao kama vile Kristo Yesu anavyowapenda na kwamba, Yesu ndiye kipimo cha upendo. Watoto wawe ni chachu ya mabadiliko na mageuzi katika maisha, ili yaweze kufanyika upya! Kuna watoto wanaoteseka kutoka na vita, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, umaskini; kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, na wengine wamebaki kuwa ni watoto yatima: Watu wote wa Mungu wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mabadiliko. Yote haya yanawezekana, ikiwa kama kuna upendo wa dhati kati yao na kwa njia hii, wataweza kujenga na kudumisha familia moja ya binadamu inayofumbatwa katika upendo kama ilivyo kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika watoto wote waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni kujitahidi kupendana wao kwa wao; kuwa ni watu wema; wenye heshima kwa wakubwa na kwamba, wajenge na kudumisha urafiki wa kweli katika Kristo Yes una kwa njia hii, wataweza kuunda familia kubwa ya binadamu na hivyo wapata furaha maisha mwao na kuwa ni watu wenye furaha. Kamwe wasisahau kujenga urafiki na mahusiano mema na Kristo Yesu, kwani anataka kuwa karibu sana na watoto wadogo, hadi utimilifu wa dahari.

Fumbo la Utatu Mtakatifu
26 May 2024, 14:39