Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Ureno 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Ekaristi Takatifu ni jibu la Mwenyezi Mungu kwa njaa kuu ya moyo wa mwanadamu, kwa njaa ya maisha ya kweli: ndani yake Kristo Yesu mwenyewe yu kweli kati ya waja wake ili kuwalisha, kuwafariji na kuwategemeza katika safari ya maisha, huku bondeni kwenye machozi. Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Kardinali José Tolentino de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu kuwa Mwakilishi wake maalum katika Maadhimisho ya Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Ureno kuanzia tarehe 31 hadi tarehe 2 Juni 2024 huko mjini Braga, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Partilhar o Pão, alimentar a Esperança. "Reconheceram-n'O ao partir o Pão" (Lc 24,35). Yaani “Kushiriki Mkate Kuna Rutubisha Matumaini. “Alitambulikana nao katika kuumega mkate.” Lk 24:35. Baba Mtakatifu katika barua aliyomwandikia Kardinali José Tolentino de Mendonça, anasema, Kristo Yesu ameliachia Kanisa ukumbusho wa mateso yake katika Sakramenti ya ajabu, hili ni tunda la ukombozi ndani ya waamini. Ni Kristo Yesu ambaye amejificha katika maumbo ya Mkate na Divai. Ni katika muktadha huu, Kanisa linayo furaha kubwa kuadhimisha Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Ureno na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno lilipenda maadhimisho haya yaweze kutajirishwa na maneno ya mtu mashuhuri na kwa fursa hii ni Kardinali José Tolentino de Mendonça, anayefahamu vyema: Maisha, utamaduni, hali ya kidini na kijamii ya watu wa Mungu nchini Ureno.
Baba Mtakatifu anamtaka Kardinali José Tolentino de Mendonça, kuwafikishia watu wa Mungu salam, matashi mema na kuonesha ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa watu wa Mungu nchini Ureno sanjari na kuwatia moyo, ili kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria, Mpatanishi wa neema, chanzo cha wokovu wa mwanadamu; Mlinzi wa imani waweze kukirimiwa roho ya upendo kwa kusambaza zawadi ya umoja wanaposhiriki katika kuumega mkate, huku wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali; na kudumu katika mafundisho ya Mitume, imani moja iwaangazie wanadamu, ili kuunganisha upendo na hatimaye waweze kuwa kitu kimoja. Baba Mtakatifu Francisko amewapatia baraka zake za Kitume, wale wote wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Ureno kuanzia tarehe 31 hadi tarehe 2 Juni 2024 huko mjini Braga. Kongamano la Kwanza la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Ureno liliadhimishwa kuanzia tarehe 2 hadi 7 Julai 1924.
Wakati huo huo habari kutoka Vatican zinabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, katika Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu “Corpus Domini”, Dominika tarehe 2 Juni 2024 majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Ulaya ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kutakuwepo na maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, kupitia barabara ya Merulana. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2022, Baba Mtakatifu Francisko hakuweza kuadhimisha Sherehe hii kutokana na mgogoro wa afya na mwaka 2023 hakufanya Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu hadharani.
Itakumbukwa kwamba, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi angavu na endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni zawadi; na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini ndani ya jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kimsingi, maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayofanywa na Jumuiya ya waamini wa Kanisa mahalia mintarafu Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia ya kuendelea kuzungumza na Kristo katika safari ya maisha ya waamini. Ni muda wa kuimarisha katekesi kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.