Tafuta

Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel unatoa huduma na kuchangia maendeleo ya wananchi walioko kwenye Ukanda wa Sahel. Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel unatoa huduma na kuchangia maendeleo ya wananchi walioko kwenye Ukanda wa Sahel.  (AFP or licensors)

Kumbukizi ya Miaka 40 ya Mfuko wa Yohane Paulo II Kwa Ajili ya Ukanda wa Sahel

Ukanda wa Sahel unakabiliwa na changamoto nyingi za maisha; hapa ni eneo ambalo lina misigano mikali ya kidini na kisiasa; mambo yenye changamoto kubwa katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na utulivu. Katika machafuko na kinzani za namna hii katika Ukanda wa Sahel, ushuhuda na mshikamano wa upendo ni mambo msingi sana yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina! Udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel unatoa huduma na kuchangia maendeleo ya wananchi walioko kwenye Ukanda wa Sahel pasi na ubaguzi wa kidini au wa kikabila, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mfuko huu ni kielelezo makini cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo kadiri ya maelekezo ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ukanda wa Sahel unakabiliwa na changamoto nyingi za maisha; hapa ni eneo ambalo lina misigano mikali ya kidini na kisiasa; mambo yanayoleta changamoto kubwa katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na utulivu. Katika machafuko na kinzani za namna hii katika Ukanda wa Sahel, ushuhuda na mshikamano wa upendo ni mambo msingi sana yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kwa kutambua kwamba, Kanisa linapenda kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho kati ya Watu wa Mataifa; ili kwa pamoja waweze kujifunga kibwebwe kupambana na Jangwa ambalo linazidi kutishia: maisha, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ukanda wa Sahel. Hili ndilo lengo kuu lililomsukuma Mtakatifu Yohane Paulo II kuamua kuanzisha Mfuko wa Sahel, ili kusaidia kukoleza mchakato wa maendeleo ya watu katika Ukanda huu tarehe 22 Februari 1980. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka wajumbe wa Mfuko huu kuhakikisha kwamba, wanajielekeza zaidi katika mafunzo makini kwa wadau ambao watasimama kidete kupambana vyema na: uchafuzi na uharibifu wa mazingira, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa Jangwa la Sahel. Ukame wa kutisha katika Ukanda wa Sahel ni matokeo pia ya mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mifugo yao.

Utunzanji bora wa mazingira nyumba ya wote
Utunzanji bora wa mazingira nyumba ya wote

Ukame wa kutisha umechangia pia ongezeko kubwa la watoto wenye utapiamlo wa kutisha pamoja na magonjwa ya milipuko. Tangu kuanzishwa kwake, Mfuko huu umepata mafanikio makubwa ambayo hayana budi kuendelezwa na wadau mbali mbali, ili kudhibiti kuenea kwa Jangwa la Sahel, lililosababisha maafa makubwa kati ya mwaka 1973 na mwaka 1974. Mtakatifu Paulo VI, Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Benedikto XVI na kwa sasa Papa Francisko ni viongozi wa Kanisa ambao wanajielekeza katika kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu pamoja na kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi, Mafanikio ya miradi inayosimamiwa na kuendeshwa na Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Ukanda wa Sahel katika kipindi cha miaka arobaini tangu kuanzishwa kwake yanapimwa kwa kuangalia udhibiti wa Jangwa la Sahel na kwamba, kuna haja ya kujenga mahusiano mema na Makanisa mahalia kwani huu ni mchango wa Kanisa kwa ajili ya: Ustawi, mafao na maendeleo ya Familia ya Mungu, Ukanda wa Sahel. Fedha ya Kanisa haina budi kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa katika ukweli, uwazi na uwajibikaji sanjari na kupima matokeo ya mradi husika. Wajumbe washirikishe tafiti, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika mapambano ya kudhibiti kuenea kwa Jangwa, Ukanda wa Sahel, ili kukoleza maendeleo endelevu ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Watu wa Mungu kutoka nchini Mali
Watu wa Mungu kutoka nchini Mali

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya kumbukizi ya Maadhimisho ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel, tarehe 22 Februari 1984 amemwandikia ujumbe Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu na katika ujumbe huu, anakazia kuhusu umuhimu wa kuendeleza majadiliano mintarafu athari za kuenea kwa Jangwa la Sahel; mshikamano unaowajibisha; changamoto ya haki, amani, usalama, ustawi na maendeleo pamoja na uwajibikaji wa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anakumbushia kilio cha watu wa Mungu kutoka Ukanda wa Sahel, walioshuhudia ndugu, jamaa na marafiki zao, wakifariki dunia kwa baa la njaa, ukame na magonjwa. Tangu wakati huo, Vatican inaendelea kufuatilia kwa karibu sana, ustawi na maendeleo ya Ukanda wa Sahel, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya utu na ustawi wa jamii Ukanda wa Sahel. Huu ni mshikamano unaofumbatwa katika uwajibikaji, kielelezo makini cha imani kwa Mwenyezi Mungu, Muumbaji pamoja na upendo kwa jirani. Huu ni mwaliko wa kuwatunza watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kama ushuhuda wa huduma ya upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake, ili hatimaye, kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, magonjwa na njaa; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mama Kanisa anataka kuwa ni sauti kwa watu wasiokuwa na sauti, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, ahadi zinazotolewa kwa ajili ya kuboresha Ukanda wa Sahel zinatekelezwa, vinginevyo hiki ni kielelezo cha unafiki mkubwa unaofanywa na Jumuiya ya Kimataifa.

Miaka 40 ya Mfuko wa Yohane Paulo II Kwa Ajili ya Sahel 2024
Miaka 40 ya Mfuko wa Yohane Paulo II Kwa Ajili ya Sahel 2024

Nchi zilizoko Ukanda wa Sahel zinakabiliana na ukosefu wa haki, amani, usalama; vitendo vya kigaidi, athari za uchumi pamoja na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, bila kusahau umaskini unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Matokeo yake, ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka katika Ukanda wa Sahel. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii ya kumbukizi ya Maadhimisho ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ajili ya Sahel, kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, usalama, ustawi na maendeleo vinapatikana Ukanda wa Sahel. Mtakatifu Paulo VI anasema, maendeleo ya kweli yanasimikwa katika udugu wa kibanadamu, haki na amani, kwani amani ni jina jipya la maendeleo ya kweli! Maendeleo fungamani yanakita mizizi yake katika ustawi na mafao ya wengi: kiroho na kimwili; kiutu na kimaadili. Lengo kuu ni kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, upendo kwa Mungu na jirani ni kielelezo makini cha imani tendaji. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kumbukizi hii itasaidia kunogesha mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukanda wa Sahel; sanjari na ujenzi wa misingi ya haki na amani.

Ukanda wa Sahel 40

 

 

11 May 2024, 15:14