Tafuta

Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil, kwa mwaka 2024 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil, kwa mwaka 2024 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. 

Kumbukizi ya Miaka 70 ya Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil

Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil, CRB Miaka 70: Kumbukumbu ya shukrani, Fumbo, Unabii na Matumaini. Papa katika barua yake kwa washiriki wa maadhimisho haya, anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana miongoni mwa Mashirika ya Kitawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wito wa Mungu ni chemchemi ya upendo unaojibiwa kwa upendo. Mwanzoni kabisa kuna watu kukutana na Kristo Yesu anayesimulia kuhusu Baba yake wa mbinguni na hivyo kuwasaidia kumfahamu na hatimaye, kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka. Maaskofu mahalia wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara mintarafu maisha ya kuwekwa wakfu, ili Kanisa la Kristo liweze kukua na kukomaa kwa kutambua kwamba, maisha ya wakfu ni zawadi kwa Kanisa, inayozaliwa na kukomaa ndani ya Kanisa lenyewe. Maisha ya wakfu yanachangia katika Ukuhani wa Daraja na Ukuhani wa Ubatizo kama sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Maisha ya kitawa ni nguzo muhimu sana inayochangia ustawi na maendeleo ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ari, moyo mkuu na furaha katika maisha, utume na utakatifu wake. Watawa wana uhuru wao kamili katika utekelezaji wa maisha na utume wao, lakini wanakumbushwa kwamba, hawajajitenga wala kutelekezwa pembezoni mwa Kanisa kama gari bovu! Watawa waishi vyema uhuru wao, kwa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ni Roho Mtakatifu anayelifanya Kanisa kuwa moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili karama mbalimbali za kiherakia na za kikarama ambazo huliongoza na kulipamba kwa matunda yake. Viongozi wa Kanisa wanaalikwa kuheshimu tofauti hizi msingi zinazoliunda na watawa wakumbuke kwamba, wao ni amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa na Kristo Yesu ndiye kiini chake!

Kumbukizi ya Miaka 70 ya Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Brazil
Kumbukizi ya Miaka 70 ya Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Brazil

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema, ile shauku ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa jirani inaibuka mara moja, kwa sababu mwamini amekutana na upendo na maana ya maisha. Kwa maneno machache kabisa ni kwamba, katika mchakato huu, mwamini amekutana na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuyageuza maisha yao, ili yaweze kuwa ni utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu mintarafu jibu la wito wa kutekeleza kwa dhati kabisa, kwa furaha na unyenyekevu wa moyo, mapenzi ya Mungu katika maisha! Kwa hakika kila mtu katika hija ya maisha yake, amekutana na Mwenyezi Mungu, akamwita kwa wito maalum. Hii ni fursa ya kuweza kufanya kumbukumbu ya tukio hilo, ili kuendelea kupyaisha mchakato wa kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha ya hapa duniani! Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil, kwa mwaka 2024 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil, CRB Miaka 70: Kumbukumbu ya shukrani, Fumbo, Unabii na Matumaini. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa washiriki wa maadhimisho haya, anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika jumuiya mbalimbali za kitawa na ndani ya Kanisa nchini Brazil.

Wito wa Mungu ni chemchemi ya upendo unaojibiwa kwa upendo
Wito wa Mungu ni chemchemi ya upendo unaojibiwa kwa upendo

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa idadi kubwa ya miito pamoja na karama mbalimbali za maisha ya kuwekwa wakfu zinazotajirisha ushirika wa Kanisa na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maisha na utume wa Kanisa. Kristo Yesu anawaita na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kila kiumbe. Rej. Mk 16:15. Zawadi ya wito wa maisha ya wakfu haina budi kulindwa na kudumishwa katika maisha ya watawa ndani ya Kanisa, changamoto na mwaliko wa kukaa katika pendo angavu la Kristo Yesu. Rej. Yn 15:9. Ili kukaa katika pendo la Kristo Yesu, watawa wanahimizwa kujenga na kudumisha majadiliano na mafungamano ya dhati kwa njia ya sala za kila siku, waaminifu katika nadhiri zao zinazoonesha na kushuhudia maisha ya wakfu katika: Ufukara, Utii na Usafi wa moyo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kumbukizi hii ya historia ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Nchini Brazil, itawasaidia kupyaisha karama za Mashirika mbalimbali ya Kitawa na Kazi za Kitume, kielelezo cha Unabii katika kutangaza na kushuhudia Injili, ili hatimaye, kuyaangalia yajayo kwa matumaini.

Watawa Brazil

 

30 May 2024, 15:00