Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake. Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake. 

Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima: Ibada, Toba, Wongofu na Utakatifu wa Maisha

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake; Unahimiza Ibada kwa Bikira Maria, Toba, Wongofu wa ndani, Utakatifu wa maisha na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani. Huu ni ujumbe wa matumaini, safari ya wokovu, amani, upendo na mshikamano duniani na kwamba, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika tarehe 12 Mei 2024, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Siku ya Mama Duniani na Waswahili wanachombeza kwa kusema “eti ni nani kama Mama”? Hii ni siku muhimu sana ya kuwaheshimu na kuwaenzi wanawake kutokana na mchango wao mzito katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni changamoto ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri mapenzi ya Mungu. Ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea akina mama ambao wamepewa dhamana ya kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai. Kwa wale wanawake ambao wamepitia kipindi kigumu wakati wa ujauzito, wafarijike kwa sala na sadaka inayotolewa na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Bikira Maria awe ni mfano bora wa kuigwa katika kutimiza wajibu wao kama akina mama ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Awe ni mwombezi wa akina mama wote wenye ujauzito kwa wakati huu, ili waweze kuwalinda na kuwatunza watoto wao ili hatimaye, waweze kuzaliwa salama salimini. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 12 Mei 2024 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea akina mama waliotangulia mbele za haki, wakiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Amewakabidhi akina Mama wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Ujumbe wa Bikira Maria Kwa Watoto wa Fatima ni endelevu
Ujumbe wa Bikira Maria Kwa Watoto wa Fatima ni endelevu

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 13 Mei anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima. Hii ni kumbukumbu ya Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos, tarehe 13 Mei 1917 na kujitambulisha kuwa ni Bikira Maria wa Rozari Takatifu, kwa kuwakabidhi watoto hawa ujumbe wa matumaini kwa binadamu wote, akiwataka wajizatiti katika kupambana na ubaya, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumilia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa! Bikira Maria anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani! Hii ni cangamoto endelevu hata kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo! Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unafumbatwa kwa kiasi kikubwa katika Injili, kiasi kwamba, Fatima inakuwa ni shule ya imani na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, na Bikira Maria ndiye Mwalimu wake mkuu! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani kwa Kristo Yesu na kamwe wasikatishwe tamaa na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia; majanga katika maisha ya watu; tawala za kifashisti na kikomunisti, tawala ambazo zimedhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kiasi hata cha kutaka kumng’oa Mungu katika maisha na vipaumbele vya waamini. Kilio cha waamini kilikuwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu asimame mwenyewe na kujitetea!

Tarehe 13 Mei 1981 Jaribio la kutaka kumuua Mt. Yohane Paulo II
Tarehe 13 Mei 1981 Jaribio la kutaka kumuua Mt. Yohane Paulo II

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ulijikita zaidi katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na Vita Kuu ya Pili ya Dunia; vita ambavyo vimesababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia. Siri zote za Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima zikafunuliwa hadharani kunako Mwaka 2000 kwa kuonesha madhara makubwa yaliyosababishwa na Urusi kwa wakati ule kwa kupandikiza “ndago” za Ukanimungu; dhuluma, nyanyaso na mauaji ya kikatili dhidi ya Wakristo! Katika kipindi hiki cha utawala wa giza na chuki dhidi ya imani ya Kikristo, hapa kukaibuka makundi ya Wakristo waliosimama imara kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Jeuri ya maisha yao ya kiroho! Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako tarehe 13 Mei 1981 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican akapigwa risasi katika jaribio la kutaka kumuua na kumfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia! Lakini akasalimika na kwamba, huu ni muujiza wa pekee kabisa aliotendewa na Bikira Maria wa Fatima. Akaamuru hata ile Siri ya Tatu ya Fatima iwekwe hadharani! Ni siri ambayo ilionesha kwamba kulikuwa na mapambano makali dhidi ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II akachukua risasi iliyotoka mwilini mwake na kuiweka kwenye taji ya nyota kumi na mbili zinazopamba kichwa cha Bikira Maria wa Fatima.

Watoto watatu wa Fatima: Francis, Yacinta na Lucia
Watoto watatu wa Fatima: Francis, Yacinta na Lucia

Tarehe 25 Machi 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II akauweka ulimwengu na kwa namna ya pekee kabisa, Urusi chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake; Unahimiza Ibada kwa Bikira Maria, Toba, Wongofu wa ndani, Utakatifu wa maisha na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani. Waamini watambue daima kwamba, hata katika shida na mahangaiko yao, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali! Bikira Maria anataka kuwaachia watoto wake, ujumbe wa matumaini, wokovu, amani na kwamba, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha ya mwanadamu! “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” 1 Pet 3:15. Ni ushuhuda kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, aweze kuwaongoza watu kwa Mungu Baba Mwenyezi.

B. Maria wa Fatima
13 May 2024, 15:04