Kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo wa VI: Furaha ya Kuwa ni Mfuasi wa Kristo Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Amewakumbusha mahujaji na wageni kwamba, tarehe 29 Mei ya kila mwaka Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo VI (26 Septemba 1897 hadi 6 Agosti 1978) aliyechaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 262, hapo tarehe 21 Juni 1963. Tarehe 19 Oktoba 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Na tarehe 14 Oktoba 2018 akatangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Mtakatifu. Ni kiongozi aliyetekeleza utume wake katika mazingira magumu ya Vita Baridi, akajitahidi kuwaganga na kuwafunga watu wa Mungu waliokuwa wamejeruhiwa, kwa haki na huruma.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mtakatifu Paulo wa VI alikuwa ni kiongozi aliyekuwa anawaka upendo angavu wa Kristo Yesu kwa Kanisa na kwa ajili ya binadamu. Maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo VI yaamshe na kupyaisha furaha ya kuwa ni mfuasi wa Kristo Yesu; apyaishe ari na mwamko wa ujenzi wa utamaduni wa upendo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanapopata nafasi kujisomea Waraka wa Kitume wa Papa Paulo VI “Evangelii nuntiandi” Waraka ambao bado ni muhimu sana katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.