Tafuta

Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hivyo ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hivyo ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza.  

Maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu

Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hivyo ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza. Hili ni fundisho la kweli ya imani. Imani Katoliki ndiyo hii: Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, ni umungu mmoja.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu Msikilizaji na Msomaji, leo tunaadhimisha Sherehe ya utatu Mtakatifu, yaani Mungu mmoja katika nafsi tatu. Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hivyo ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza. Hili ni fundisho la kweli ya imani. Imani Katoliki ndiyo hii: Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, nyingine ya Mwana na nyingine ya Roho Mtakatifu, ni umungu mmoja, wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu; utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele. Rej. KKK 222-266. Basi karibuni tukiongozwa na wazo hili: Utatu Mtakatifu ni Fumbo linafumbuliwa na huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 25 na 26 Mei 2024, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa litakuwa linaadhimisha pia Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni inayonogeshwa na kaulimbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote na watu wenye mapenzi mema kusindikiza hija hii kwa sala na sadaka na kwamba, anawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho haya.

Maadhimisho ya Siku ya kwanza ya Watoto Ulimwenguni, 25-26 Mei 2024
Maadhimisho ya Siku ya kwanza ya Watoto Ulimwenguni, 25-26 Mei 2024

UFANANUZI:Katika maisha ya kawaida ya kila siku kuna mambo ambayo tunaweza kuyaelewa kiurahisi na mengine kushindwa kuyaelewa vema, yanapita akili zetu za kibinadamu. Kwa mfano hatuwezi kuelewa kinaganaga siri ya Utatu Mtakatifu. Ni vigumu sana. Mtakatifu Augusitino alijaribu kwa akili yake yote kupembua siri kuu ya Utatu Mtakatifu alishindwa na hatimaye aliishia kusema inatupasa kusadiki kwa sababu Mungu ametufunulia Imani katika Utatu Mtakatifu imefunuliwa kwetu na Mungu mwenyewe katika Maaandikao Matakatifu. Tunayo mifano michache katika Biblia inayotudokeza fumbo hili la Utatu Mtakatifu. Mfano; Mwa. 1:2, “Roho ya Mungu ikatulia juu ya maji”, hii yamaanisha kwamba Roho yupo tangu mwanzo; Mwa2:26, “na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu." Mungu anaongea katika uwingi kwa sababu kuna nafsi zaidi ya moja; Mt. 28:19, “watu wa mataifa yote wabatizwe kwa jina la Utatu Mtakatifu – Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. 2Kor.13:14, “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote”, mtume Paulo anataja nafsi tatu za Mungu katika ufasaha wake. Hii ni mifano michache katika Biblia inayotudokezea fumbo hili la Utatu Mtakatifu, yaani katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu – Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, japo kila mmoja ni nafsi kamili, Mungu ni mmoja tu na nafsi zote tatu ni sawa. Mungu aliyejifunua kwetu katika nafsi tatu ni mwingi wa huruma na mapendo na fadhili, si mwepesi wa hasira, ni mwema na mwaminifu katika ahadi zake, anayesamehe makosa na dhambi za watu, ni baba anayejali wanae na kutupenda hata kama tunatenda dhambi (rej. Kut 34:6). Mungu huyu ni Upendo na chanzo halisi cha upendo na amani. (rej. 2Kor. 13 :11) Kwa upendo wake mkubwa kwa ulimwengu alimtuma mwanae wa pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele, alipenda kutushirikisha maisha ya umilele, maisha ambayo yanajionesha katika nafsi za utatu mtakatifu (rej Yoh. 3 : 16), na hatimaye akamtuma Roho wa mwanae mioyoni mwetu, Roho Mtakatifu, ambaye ni Roho wa Upendo na amani.

Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani, matumaini na mapendo
Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani, matumaini na mapendo

KATIKA MAISHA YA KIJAMII TUJIFUNZE NINI? Tunapofanya ishara ya msalaba, tunaposali sala ya atukuzwe Baba, tunapokiri imani nk tunaungama Mungu mmoja katika nafsi tatu. Ila tatizo tunapofanya ishara ya msalaba au kusali hatutafakari zaidi. Leo tunapoadhimisha Fumbo la Utatu Mtakatifu tunamwomba Mungu anaishi katika Jumuiya na sio mpweke. Tunatakiwa tuige mfano wa Utatu Mtakatifu wa kuishi katika Jumuiya kwa upendo. Kuna watu wanaishi kwa upweke sana, labda kwa sababu wametengwa, hawapendwi nk. Wapendwa, Nafsi tatu za Mungu ni mfano wa umoja na mapendo makuu. Zinashirikiana na kufanya kazi kwa umoja na mapendo ya Kimungu. Sisi tunashirikishwa katika umoja huo wa mapendo ya kimungu kwa sababu katika Ubatizo tumetiwa Muhuri usiofutika kwa jina la Utatu Mtakatifu. Kwa hiyo inatupasa kuwa na umoja na mapendo kati yetu sisi wenyewe na kati yetu na Mungu katika Utatu wake. Mtakatifu Augustino anasema, ‘‘Roho Mtakatifu anatoka kwa Baba kama chanzo cha kwanza, na kwa paji la milele analolitoa Baba kwa mwana, anatoka katika umoja wa baba na mwana’’. Kupelekwa kwa Roho Mtakatifu ambaye Baba anamtuma kwa jina la Mwana na ambaye Mwana anamtuma toka kwa Baba, kunafunua kwamba yeye pamoja nao ni Mungu huyo huyo mmoja. Mipango yote ya Mungu ya wokovu ni kazi ya pamoja ya nafsi tatu za Mungu. Kama vile utatu una asili moja iliyo sawa, vile vile una utendaji mmoja ulio sawa.

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ufunuo wa upendo wa Mungu
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ufunuo wa upendo wa Mungu

Ndugu yangu mpendwa, hili ni Fumbo la imani tu. Tunajaribu kumchunguza Mungu ambaye achunguziki. Madhehebu mengi hujaribu kubishana kwa sababu uelewa wa Mungu ni tofauti na ni mdogo mno. Lakini mbona hata sisi wenyewe hatujielewi.  Kweli sisi Binadamu tunajielewa? Tunajielewaje wakati hatuishi kwa amani, hatuchukuliani, Kuvumiliana kwa upendo na saburi, unajielewaje wakati wapo wanaoongeza maumbile ya miili yao, wanaojichubua ngozi zao? Kijana Unapovaa milegezo na kuvaa hereni mtoto wa kiume unajielewa kweli? Unapokosa kuwajibika bado unajielewa? Angalieni sisi binadamu hatujielewi ila tunataka kumuelewa Mungu? Hata jirani yako,au mwenzako wa ndoa au mwanajumuiya mwenzako unamuelewa asilimia zote? Huoni wakati mwingine unamshangaa ivi hii tabia imetoka wapi. Mbona tulipofahamiana mara ya kwanza sikuiona. Kumbe hata mwenzako/jirani/rafiki yako hujamuelewa sasa utamuelewaje Mungu asilimia zote ?  Ukweli ni kwamba njia zake hazichunguziki na hazieleweki warumi 11 : 33. Tunapofanya ishara ya msalaba tunagusa kichwa huku tukisema kwa jina la Baba. Maanake Mungu Baba ni kichwa. Akina baba wanatakiwa kuwa na sifa kama ya Mungu Baba. Akina baba nyie ni vichwa vya Familia. Kuvaa suruali haitoshi ila nyie wanaume na hasa mlio kwenye ndoa, je, mna sifa ya kuitwa baba, kwa bahati nzuri hata sisi maklero tunaitwa baba? Baba ni cheo kikubwa sana mjue. Kama hujielewi, hutunzi Familia, hauwajibiki tusipindishe maneno huna sifa ya kuitwa baba. Si ajabu hata wengine hawajui wana watoto wangapi, si ajabu hata wengi hawajui watoto wao wanasoma darasa la ngapi, wanakula au wanavaa nini. Ila akisoma hata huoni aibu kusema Jembe langu hilooo, wewe umechangia nini kama baba? Ninavyoona ni kwamba wanaume wengi wamewaachia wake zao majukumu. Wanaume wengi wamechagua kuwa mikia na si vichwa tena. Poleni sana.

Umoja, ushirika, upendo na mshikamano katika sala
Umoja, ushirika, upendo na mshikamano katika sala

Mwisho Umoja na upendo kati yetu na Mungu katika Utatu wake, tunaweza kuonesha kwa njia ya sala, tukitambua kwamba sala ni moja ya nguzo muhimu ya maisha ya kiroho hapa seminarini. Na kwa watu wa ndoa sala ni muhimu kwa sababu inasaidia kuleta umoja katika familia na kudumisha uhusiano mzuri na mwenyezi Mungu, kwa hiyo ni muhimu kusali katika familia na katika jumuiya ndogondogo za Kikristo. Tunapoutukuza Utatu Mtakatifu katika siku ya leo, tutambue kwamba huruma na mapendo ya kimungu lazima vitawale katika nyanja ambalimbali za maisha yetu, kwa sababu palipo na upendo na umoja hapo upo utatu Mtakatifu, hapo yupo Mungu aliye mwingi wa huruma, mapendo na fadhili. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.

Fumbo Utatu Mtakatifu
24 May 2024, 15:19