Maadhimisho ya Siku ya 103 ya Waamini Wakatoliki Nchini Ujerumani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Familia ya Mungu nchini Ujerumani kuanzia tarehe 29 Mei hadi Dominika tarehe 2 Juni 2024 inaadhimisha Siku ya 103 ya Waamini Wakatoliki nchini Ujerumani, “Katholikentag” huko Erfurt, Turingia kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Wakati Ujao ni Wa Mtu wa Amani.” Chimbuko la maadhimisho haya ni huko Magonza, kunako mwaka 1848, mwanzo wa demokrasia nchini Uerumani. Katika Ulimwengu ambamo kumesheheni: Vita, kinzani, migogoro na majanga mbalimbali mazungumzo yanayokita mizizi yake katika msingi wa maafikiano na hata pengine hali ya kutokukubaliana, kwa lengo ya kukuza na kudumisha amani duniani, hayana budi kupyaishwa. Jumuiya ya Kimataifa inawahitaji viongozi watakaosimamia utekelezaji wa uhuru, ukweli, haki na upendo katika familia kubwa ya binadamu. Ulimwengu unakabiliwa na ongezeko kubwa la hatari zinazotishia uthabiti wa haki na amani na kwamba, amani sasa ni changamoto ya ustaarabu. Kumbe, kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu katika ujumla wake. Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Kumbe, wito wa kutafuta, kujenga na kudumisha amani ulimwenguni ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake.
Ndiyo maana watu wa Mungu nchini Ujerumani wanashiriki katika maadhimisho ya Siku ya 103 ya Waamini Wakatoliki nchini Ujerumani, “Katholikentag.” Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki katika maadhimisho ya tukio hili la kiimani, kwani huu ni ushuhuda wa imani tendaji na uwajibikaji wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Kati ya mada zinazopembuliwa ni pamoja na: Demokrasia; Umoja na Utofauti; Mchakato wa uimarishaji wa Jumuiya; Haki na Amani. Maadhimisho haya yanajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene nchini Ujerumani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 103 ya Waamini Wakatoliki nchini Ujerumani, “Katholikentag” anakazia kuhusu umuhimu wa waamini Wakatoliki kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kwa kujikita katika amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kipaumbele kwa maskini na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Kauli mbiu ya maadhimisho haya inachota amana na utajiri wake kutoka katika Zaburi ya 37 inayomwonesha mtu wa amani anayesimamia haki, ni mchamungu na kujiaminisha mbele ya Mungu. Lakini kwa bahati mbaya mwanadamu amekuwa na matumizi mabaya ya rasimali za dunia na matokeo yake ni athari za mabadiliko ya tabianchi, mateso na mahangaiko kwa binadamu na waathirika wakuu ni vijana, watoto na wanawake. Kumbe, kuna haja ya kufanya wongofu wa kiikolojia, ili kutoa mwelekeo mpya wa matumizi sahihi ya amana na rasilimali za dunia.
Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu ni dira, mwongozo na mwelekeo wa maisha mapya, anayetakasa mahusiano na mafungamano kati ya binadamu na mazingira nyumba ya wote na kusaidia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Kristo Yesu ni chimbuko la matumaini mapya, kwa kuwataka watu wa Mungu wajikite katika haki jamii, kwa kutoa kipaumbele kwa tunu msingi za maisha ya kijamii kama zinavyofafanuliwa kwenye Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amewakirimia wanadamu amani ya kweli, changamoto na mwaliko wa kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho, huruma, msamaha, majadiliano na amani ya kweli! Yote haya yanabubujika kutoka katika ukimya wa Fumbo la Msalaba. Siku ya Pasaka ya Bwana, Kristo Yesu alidhihirisha jinsi ambavyo mtu wa amani anavyotakiwa kuishi. Huu ni mwaliko kwa waamini kujihusisha kikamilifu katika medani mbalimbali za maisha, ili hatimaye, waweze kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti; wasaidie maboresho ya maisha ya watu na kwamba, bila haki, amani iko mashakani.
Amani inatishiwa na: Chuki dhidi ya Wayahudi, Mifumo mbalimbali ya kibaguzi na itikadi zinazochochea vita na mauaji. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kinzani za kimaadili, kijamii, kiuchumi na kisiasa; uharibifu wa mazingira nyumba ya wote na ukosefu wa haki ni mambo ambayo yanatishia: utu, heshima na haki msingi za binadamu; tunu bora za maisha ya ndoa na familia pamoja na amani. Changamoto na matatizo yote haya yanaweza kupatiwa ufumbuzi, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaamua kushirikiana kwa dhati, kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haya ni majadiliano yanayopaswa kuelekezwa pia kwenye maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho ya Siku ya 103 ya Waamini Wakatoliki nchini Ujerumani, “Katholikentag” ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, kama ilivyojitokeza kunako mwaka 1989, watu wa Mungu wakafanya mapinduzi ya amani. Huu ni mwaliko wa kudumisha maisha ya sala. Na kauli mbiu: “Wakati Ujao ni Wa Mtu wa Amani” iwasaidie watu wa Mungu nchini Ujerumani kuendelea kujikita katika maisha ya sala, ili kweli nguvu za Roho Mtakatifu ziweze kuwakirimia matumaini na furaha ya kweli. Tukio hili liwatajirishe sana katika maisha ya kiroho.