Maadhimisho Siku ya Kwanza Ya Watoto Ulimwenguni, Roma, 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kuu alitangaza kwamba, tarehe 25 na 26 Mei 2024 ni Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day Rome 2024” itakayoadhimishwa mjini Roma. Maadhimisho haya yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Ni shauku ya Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inakirithisha kizazi kipya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake kwa kutoa kipaumbele cha kwanza watoto, Mama Kanisa naye katika maisha na utume wake anataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto, kwa kuwapatia malezi makini, kwa kuwalinda na kuwaendeleza. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni kwa Mwaka 2024 anawakumbusha watoto kwamba, wao wana thamani kubwa sana machoni pa Mungu na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kaulimbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na kuwa kama watoto wadogo, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Fumbo la Umwilisho. Watoto ni matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Maadhimisho haya yanafanyika mjini Roma sanjari na kwenye Makanisa mahalia. Hii ni siku inayofumbatwa katika maisha ya kiroho, mshikamano pamoja na utamaduni, ili kuwakumbatia, kuwapokea na kuwalinda watoto wadogo; tayari kuwasindikiza katika shule ya haki na amani.
Baba Mtakatifu anawaalika watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuguswa na historia ya watu mbalimbali katika maisha yao, bila kuwasahau watoto wanaoteseka kwa magonjwa, watoto ambao wamepokwa utoto wao na kwa sasa wanateseka sana. Hawa ni watoto wanaoathirika kutoka na vita na kinzani za kijamii; watoto wanaoteseka kwa baa la njaa na kiu; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto wanaolazimishwa kwenda kwenye mstari wa mbele kama chambo cha vita; watoto wanaokimbia kutoka kwenye familia zao kama wakimbizi na wahamiaji; watoto wanaotenganishwa na familia zao, kiasi cha kukosa fursa ya kuendelea tena na masomo; watoto wanaotumbukiwa kwenye magenge ya uhalifu Kitaifa na Kimataifa; watoto wanaoathirika kwa matumizi haramu ya dawa za Kulevya, Watoto wanaotumbukizwa kwenye mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Hawa ni watoto wanaopaswa kusikilizwa, ili kutolea sauti yao ushuhuda na hivyo kuonjeshwa tena huruma na upendo. Baba Mtakatifu anawatia shime watoto hawa kuwa na furaha kwa sababu wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Wajenge na kudumisha urafiki kwa kushirikishana na wengine, katika uvumilivu, ujasiri, ubunifu, hali ya kufikirika bila woga wala maamuzi mbele. Siri kuu ya maisha inasimikwa katika sala, ambayo Kristo Yesu amewafundisha wafuasi wake, ile Sala kuu, Sala ya Baba Yetu, itakayo wachangamotisha kuwa ni wajenzi wa dunia inayosimikwa, katika utu, haki na amani. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wadogo, ili hatimaye, kujenga udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu; urafiki, amani na utulivu. Zaidi ya watoto 72, 000, wanashiriki, huku wakisindikizwa na wazazi pamoja na walezi wao.
Tamko la Udugu wa Kibinadamu Miongoni Mwa Watoto Wadogo: Baba Mtakatifu Francisko katika utangulizi wa tamko hili anakazia umuhimu wa watoto kukaa kwa pamoja kama marafiki wakiwa nyumbani, shuleni, parokiani, kwenye viwanja vya michezo, ili kucheza, kuimba pamoja na kugundua mambo mapya kwa pamoja. Wakati wakifurahia maisha, bila ya kumwacha mtoto yeyote nyuma. Hivi ndivyo urafiki wa kijamii unavyojengwa, kukua na hatimaye, kukomaa; katika kushirikishana mali za dunia; kwa kusameheana na kuishi katika hali ya utulivu na uvumilivu; ujasiri na ubunifu, bila wasiwasi, woga wala maamuzi mbele! Watoto wanasema, udugu wa kibinadamu unawawezesha kuishi kwa mshikamano ili kukabiliana na dhoruba mbalimbali za maisha, kwa kujikita katika mshikamano unaopaswa kupaliliwa ili kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; upendo na furaha ya kweli tayari kupandikiza mbegu ya matumaini itakayozaa: upendo na ukweli; mambo msingi yanayoweza kuvunjilia mbali kuta za utengano. Ndoto yao kama watoto ni kuwa na ulimwengu ambamo watoto wote wanaweza kujisikia kuwa wako nyumbani; mahali ambapo haki, amani na maridhiano vinatawala; mahali ambapo watoto wanapata fursa ya kukua, kusoma, kucheza na kuwa na furaha. Hapa ni mahali ambapo watoto watajisikia kweli, mahali wanapoweza kuonwa, kupokelewa sanjari na kuendelezwa.
Watoto wanataka kuona ulimwengu ambamo hakuna vita wala misigano ya kijamii, bali mshikamano wa upendo kwa maskini na wanyonge zaidi. Watoto wanataka kuwaona watu wazima wakijenga mahusiano na mafungamano yao katika mwelekeo chanya na wenye utulivu; mahusiano yanayosimikwa katika ukarimu, majadiliano, heshima, ushirikishi, msamaha na mshikamano. Wanataka kuona watu wazima wakijenga na kudumisha urafiki wa kweli pasi na woga wala wasiwasi, huzuni na upweke hasi. Watoto wanawataka watu wazima kuonesha kwamba wao ni ndugu wa wote kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, rafiki wa kweli anayewafunza watoto kujenga urafiki. Watoto wanatoa mwaliko kwa watu wazima kuwasaidia kutekeleza hii ndoto yao ya maisha, kwa kuonesha maboresho ulimwenguni, kwa kuonesha matumaini kwa siku zijazo, kwa kuwasindikiza watoto katika njia ya amani, maelewano, udugu wa kibinadamu; ukuaji, ukarimu na matumaini, ili hatimaye, kuonja furaha ya kweli inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Jarida la “Trenitalia la Freccia” anakazia kuhusu umuhimu wa elimu makini kwa watoto na vijana wa kizazi kipya; Umuhimu wa kuwasikiliza, kuwasindikiza, kuwalinda na kuwaendeleza watoto watoto na vijana, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani duniani. Watoto waelimishwe juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; pamoja na matumizi bora ya njia za mawasiliano ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote.